Unguja. Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Zanzibar, Dk Khalid Salum Mohamed ameishauri Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi Zanzibar kufanya mapitio ya sheria ya mipango miji ili ziendane na mahitaji ya makazi kwa miaka 30 ijayo.
Amesema hayo jana Alhamis Januari mosi, 2026, katika hafla ya ufunguzi wa nyumba za makazi, zilizopo Kiembesamaki Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.
Dk Khalid amesema sheria ya sasa inapaswa kupitiwa upya ili kuendana na mahitaji halisi ya wananchi pamoja na kasi ya ukuaji wa miji.
“Wizara inapaswa kupitia sheria ya mipango miji kwa lengo la kuendana na mahitaji ya wananchi wa sasa na baadaye,” amesema.
Ameeleza kuwa miji inayojengwa kwa sasa inapaswa kuonyesha hadhi, haiba na utambulisho wa Zanzibar, hali itakayosaidia kuifanya kuwa kivutio cha watalii.
Amesema mpangilio wa nyumba unapaswa kuzingatia uwepo wa maeneo ya kutosha kwa ajili ya shughuli nyingine za kimaendeleo, ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya barabara na huduma za kijamii.
Kwa mujibu wa waziri huyo, matumizi sahihi ya ardhi yataiwezesha nchi kutumia eneo dogo kwa shughuli kubwa za maendeleo na kuifanya miji iwe ya kuvutia na yenye mpangilio mzuri.
Aidha, amesema Zanzibar kwa sasa imekuwa na changamoto ya vumbi kutokana na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, lakini kuwa hali hiyo ni ya muda mfupi.
“Matunda ya mateso haya yataonekana baada ya kukamilika kwa miradi inayotekelezwa kwa lengo la kujenga uchumi imara wa nchi,” amesema.
Ameongeza kuwa dhamira ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kuwakomboa wanyonge na kuweka usawa miongoni mwa wananchi, lengo ambalo amesema limefanikiwa kwa kiwango kikubwa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba Zanzibar (ZHC), Sultan Said Suleiman, amesema mradi wa nyumba za makazi Kiembesamaki umegharimu Sh3.4 bilioni na umejengwa na Kampuni ya KMKM Engineering Limited ndani ya miezi nane.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Zanzibar, Dk Khalid Salum Mohamed akikata utepe katika ufunguzi wa Nyumba za Makazi Kiembesamaki, jana Januari Mosi 2025. Mkoa wa Mjini Magharibi.
Amesema mradi huo una jumla ya ghorofa tano zenye nyumba 22, ambazo tayari zimeshauzwa.
Ameeleza kuwa ZHC itaendelea kujenga nyumba zenye hadhi na ubora ili kuhakikisha wananchi wanapata makazi bora na salama.
“Miradi ya nyumba inayotekelezwa kwa sasa ni ushahidi wa utekelezaji wa vitendo na siyo maneno,” amesema.
Naye Naibu Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi Zanzibar, Salha Mwijuma, amesema shirika hilo lina uwezo wa kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo endapo litapewa nafasi.
Ameongeza kuwa nyumba hizo zimezingatia mahitaji ya watu wote, wakiwemo wenye mahitaji maalumu, hivyo kila mwananchi ana haki ya kuishi katika makazi yenye staha.