Japan. Waziri Mkuu wa Japan, Sanae Takaichi ameongeza nguvu kushawishi kutaka vyoo vya wanawake viongezwe katika jengo la Bunge nchini humo ili kupunguza foleni.
Katika taarifa iliyochapishwa Mtandao wa BBC Januari 1, 2026 imeeleza kuwa, Takaiche ni miongoni mwa wabunge wanawake 60 waliowasilisha ombi la kuongezwa kwa vyoo vya wanawake katika jengo la Bunge ili kuendana na ongezeko la uwakilishi wa wanawake katika mhimili huo wa kutunga sheria.
Wanawake 73 ilichaguliwa kuingia katika Baraza la Chini lenye viti 465 katika uchaguzi wa Oktoba 2024, idadi iliyozidi rekodi ya awali ya wanawake 54 iliyowekwa mwaka 2009.
Mmoja wa wabunge wa upinzani, Yasuko Komiyama amesema kuwa mara nyingi kumekuwa na foleni chooni kabla ya kuanza vikao vya Bunge huku wabunge wengine wanawake wakishindwa kupata huduma hiyo kwa wakati.
Komiyama kutoka Chama cha Kidemokrasia cha Kikatiba cha upinzani amesema kukosekana matundu ya choo ya kutosha pia kunaleta usumbufu kwa kuwa wafanyakazi wanawake na wageni pia hutumia vyoo hivyo hivyo.
“Nataka kuinua sauti yangu na kujitayarisha kwa siku ambayo wanawake watashikilia zaidi ya asilimia 30 ya viti vya Bunge katika siku zijazo,” amesema.
“Iwapo utawala una nia ya dhati ya kukuza uwezeshaji wa wanawake, naamini tunaweza kutegemea uelewa na ushirikiano wao,” amesema Komiyama.
Mwenyekiti wa Kamati ya Baraza la Chini, Yasukazu Hamada ameonyesha utayari wa kuzingatia pendekezo la kuongeza vyoo vya wanawake.
Karibu na ukumbi wa vikao vya jumla kuna choo kimoja cha wanawake chenye vibanda viwili, ingawa jengo lote la bunge lina jumla ya vyoo tisa vya wanawake vyenye vibanda 22.
Kwa upande mwingine, kulingana na ripoti za vyombo vya habari vya ndani, kuna jumla ya vyoo 12 vya wanaume vilivyo na vibanda na vyoo vya kusimama 67 katika jengo lote.
