Ahoua akisepa Simba, mrithi wake ni huyu

KIKOSI cha Simba usiku wa leo kipo uwanjani kupepetana na Muembe Makumbi katika pambano la kwanza la Kundi B la michuano ya Kombe la Mapinduzi 2026, huku mabosi wa klabu hiyo wakiwa bize kusaka mashine mpya zitakazoimarisha timu hiyo hasa baada ya kuwepo kwa tetesi za Jean Charles Ahoua kujiandaa kusepa Msimbazi.

Mfungaji huyo bora wa Ligi Kuu Bara msimu uliopita akifunga mabao 16 inadaiwa ameomba kuondoka klabuni hapo akiwa ni kati ya wachezaji ambao bado hawajaripoti kikosini wakati timu ikiwa Zanzibar kushiriki mechi za Mapinduzi, huku klabu ya Raja Casablanca ya Morocco inayonolewa na Fadlu Davids ikihusishwa naye.

Hata hivyo, pengine kwa kujua nyota huyo aliyebakisa mkataba wa miezi sita Msimbazi hana mpango wa kuitumikia timu hiyo, mabosi wa Simba wameanza mchakato wa kushusha kiungo mshambuliaji anayekipiga Singida Black Stars, Idriss Diamonde.

Kiungo huyo raia wa Ivory Coast alitua Singida msimu huu akitokea Zoman FC ya nchini kwao, Agosti 20 mwaka jana, kwa mkataba wa miaka mitatu na Simba inataka imchukue kwa mkopo, jambo linaloelezwa tayari kuna mazungumzo yameanza baina ya klabu hizo mbili zilizopo katika michuano ya Kombe la Mapinduzi 2026.

Simba inadaiwa inamtaka Diamonde kwa ajili ya kuimarisha kikosi hicho kilichopoteza mechi mbili mfululizo za Kundi D za Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Petro Atletico ya Angola na Stade Malien ya Mali pamoja na kupoteza ile ya mwisho ya Ligi Kuu Bara mbele ya Azam FC. Diomande anamudu kucheza kama kiungo mkabaji, lakini pia winga wa kulia kitu kitakachoipa faida klabu hiyo kama itamnasa dirisha dogo.

Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Simba kimeliambia Mwanaspoti, mchakato wa kuongeza nguvu eneo hilo umekuja siku chache baada ya kubaini inahitaji nguvu ya ziada katika nafasi hiyo ya kiungo yenye wachezaji wengine kadhaa wakiwamo kina Yusuf Kagoma, Alassane Kante, Awesu Awesu, Mohammed Bajaber, Neo Maema na kiraka Naby Camara.

“Ukiondoa Kagoma na Kante hakuna mchezaji mwingine mwenye uhakika wa namba kikosi cha kwanza na tayari tuna mashindano mengi tunayoshiriki, lakini tutakaporudi baada ya mapumziko hatutakuwa na kiungo mwingine ambaye atacheza nafasi hiyo baada ya Kante kuanza kutumikia adhabu ya kadi nyekundu,” amesema mmoja wa vigogo wenye ushawishi ndani ya Simba.

“Kikosi kinatakiwa kuongezwa ili kuweka mizani sawa na kuongeza ushindani. Ukiangalia Simba ina wachezaji wengi lakini wanaopata nafasi ya kucheza mara kwa mara ni wachache. Hii ni kutokana na kukosa usawa wa ushindani, hilo limeonekana na limeanza kufanyiwa kazi.”

Kigogo huyo amesema suala la Diomande kutua Simba ni baada ya makubaliano ya pande mbili kwenda sawa, lakini jina lake limepitishwa na wanaamini anaweza kuwa msaada katika nafasi hiyo.

Akizungumzia suala la Ahoua, amesema kiungo huyo mshambuliaji na mfungaji bora wa msimu uliopita ameomba kutorudi kikosini ili aweze kutafuta changamoto nyingine nje ya Simba baada ya kupoteza nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza tangu msimu huu uanze.

“Ahoua amebakiza mkataba wa miezi sita kabla haujamalizika mwisho wa msimu huu. Lakini, hajaonyesha nia ya kuendelea kubaki hii ni baada ya kupoteza nafasi na tayari ana ofa mezani. Kama mambo yake yataenda vizuri basi anaweza asiwe sehemu ya kikosi chetu,” amesema na kuongeza:

“Kila hatua tumekuwa tukiwasiliana naye, endapo mambo yake yataenda vizuri, basi hatarejea kikosini lakini dili lake likikwama ataungana nasi hapo baadaye, hadi sasa (jana) bado hajarudi.”

Ahoua aliyesajiliwa msimu uliopita na Fadlu aliyerudi Raja Casablanca, ameanza msimu huu vibaya tangu aondoke kocha huyo kwa kushindwa kupata nafasi katika kikosi cha kwanza chini ya Dimitar Pantev aliyeondolewa mwezi uliopita na hata Seleman Matola, jambo linalomfanya kutaka kuondoka huku Raja ikitajwa.