TIMU ya Alliance FC ya jijini Mwanza imemrejesha kocha wake wa zamani, Mirambo Camil kuongoza benchi la ufundi baada ya mwenendo usioridhisha katika First League.
Kocha huyo ambaye amekabidhiwa timu tangu Desemba 30, 2025 akiwa na leseni ya Diploma A ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF), anachukua mikoba ya Chikaka Julius ambaye ametupiwa virago kutokana na matokeo mabaya.
Mirambo aliyekuwa kocha mkuu wa Fountain Gate Princess amewahi pia kuzifundisha Rhino Rangers na Singida United.
Chikaka aliyejiunga na Alliance FC msimu huu akitokea Songea United ameiongoza katika michezo mitatu ya First League ikishinda mmoja, sare moja na kupoteza moja.
Katika michezo hiyo, Alliance imevuna alama nne na kukamata nafasi ya tano katika kundi B, huku ikifunga mabao manne na kuruhusu matatu.
Akizungumza na Mwanaspoti, meneja wa Alliance, Nelson Marwa amesema wamemrejesha Mirambo ili kuboresha timu na kusaidia kuipandisha daraja kwenda Championship.
“Tumebadilisha benchi la ufundi, mwalimu tuliyekuwa naye kwenye hizi mechi nne tulizocheza tumeachana naye. Kwa sasa tuna mwalimu mwingine anaitwa Mirambo Camil. Tumemrejesha Mirambo ili atusaidie kupandisha timu,” amesema Marwa na kuongeza:
“Amekuja tayari ameona hayo maeneo na pia ana sehemu ambazo ameona kwamba hao wachezaji wakija watatusaidia, na hizo sehemu ndizo tunataka tuziongeze.”
