Arusha. Madiwani wa Jiji la Arusha wanatarajia kufanya mapitio ya kina ya Sheria ya Usafi wa Mazingira ili kudhibiti utupaji hovyo wa taka ngumu, hususan plastiki na nailoni.
Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude, ambaye amewataka madiwani kuhakikisha sheria inapitiwa upya ili kubaini kama inakidhi changamoto zinazotokana na taka ngumu.
Mkude amesisitiza kuwa kama kutabainika mapungufu, vipengele muhimu vitahimizwa kuongezwa mara moja ili sheria hiyo iwe na ufanisi wa hali ya juu katika kulinda mazingira na afya ya jamii.
“Endapo sheria itabainika kuwa na mapungufu, basi vipengele muhimu viongezwe na taratibu za kuzipitisha zianze mara moja ili ziweze kutumika kwa ufanisi hasa kuchukua hatua kwa watupaji taka hovyo,” amesema Mkude.
Mkude ameyasema hayo leo Januari 3, 2026, katika muendelezo wa utekelezaji wa Kampeni ya Usafi wa Mazingira iliyoanzishwa na madiwani wa viti maalumu wa Jiji la Arusha chini ya kaulimbiu “Ng’arisha Jiji la Arusha”, iliyozinduliwa jana na Meya wa Jiji la Arusha.
Mkuu wa wilaya ya Arusha Joseph Mkude (katikati) akizungumza kuhusu kampeni ya ng’arisha jiji la Arusha, kulia kwake ni mratibu wa kampeni hiyo Aminata Toure.
Amesema utupaji hovyo wa taka ngumu katika maeneo mbalimbali ya jiji umeendelea kusababisha madhara makubwa, ikiwemo kuibuka kwa magonjwa ya mlipuko, kuziba kwa mitaro, mifereji na mito, na kuchochea mafuriko hasa katika kipindi cha mvua.
“Nawaagiza katika vikao vya robo ya pili ya mwaka vinavyoanza hivi karibuni mfanye mapitio ya kina ya Sheria ya Usafi wa Mazingira, hususan vipengele vinavyohusu utupaji hovyo wa taka, ili kuhakikisha sheria inakuwa imara, inatekelezeka na inalinda mazingira yetu,” amesema Mkude.
Ameongeza kuwa licha ya sheria iliyopo kupiga marufuku utupaji hovyo wa taka, bado utekelezaji wake hauridhishi hivyo basi kuanzia sasa anataka wahusika wachukuliwe hatua.
Kwa upande wake, Mratibu wa kampeni hiyo na Diwani wa Viti Maalumu, Aminata Salesh Toure, amesema kampeni hiyo inalenga kuhamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika usafi wa mazingira yao, hususan katika kipindi hiki cha mvua kinachoambatana na ongezeko la hatari za kiafya.
Amesema awamu ya kwanza ya kampeni imeanza katika Kata ya Sokoni One, ikihusisha eneo la Soko la Dampo, Engutoto pamoja na Hospitali ya Wilaya, na inatarajiwa kuhitimishwa kesho Januari 4, 2026, katika Soko la Mbauda lililopo Kata ya Sombetini.
Naye Diwani wa Kata ya Engutoto, Hamza Juma Njiku, amesema kila Jumamosi kutakuwa na shughuli za usafi katika maeneo mbalimbali ya kata hiyo, na kuahidi kuifanya kuwa ajenda endelevu inayohitaji ushirikiano wa wananchi wote.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Udhibiti wa Taka na Usafi wa Mazingira wa Jiji la Arusha, James Lobikoki amesema kampeni hiyo inatarajiwa kulisaidia jiji hilo kufanya vizuri katika mashindano ya usafi wa mazingira yanayoendeshwa na Serikali kila mwaka.
Amewataka mawakala wa kuzoa taka kuzingatia ratiba na muda sahihi wa ukusanyaji wa taka katika mitaa ili kufanikisha malengo ya kampeni hiyo.
Kampeni ya “Ng’arisha Jiji la Arusha” inatekelezwa wakati ambapo Tanzania inakadiriwa kuzalisha zaidi ya tani milioni 20 za taka ngumu kila mwaka, sawa na wastani wa kilo 300 kwa mtu mmoja kwa mwaka, huku maeneo ya mijini yakiongoza kwa uzalishaji wa taka hizo.
Takwimu zinaonesha kuwa asilimia 70 ya taka hizo zinaweza kurejelezwa, zikiwemo plastiki, lakini ni takribani asilimia 10 pekee ndizo zinazorejelewa kwa sasa.