Baada ya kuanza kazi Yanga, kiungo mpya atema cheche

YANGA imeanza kushusha vyuma huko katika dirisha hili dogo la usajili lililofunguliwa rasmi juzi, Januari mosi, kufuatia kumtambulisha rasmi kiungo mpya, Mohammed Damaro ambaye amejiunga na klabu hiyo kwa mkopo wa miezi sita akitokea Singida United.

Mara baada ya utambulisho wake, Damaro ambaye kwa sasa ni raia wa Tanzania, amezungumza na Mwanaspoti kuhusu uhamisho huo huku akiwa na hesabu za kuisaidia timu hiyo kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Bara.

“Nipo tayari kwa ushindani. Nitajitahidi kuhakikisha kila mechi nitakayocheza nachangia kwa kiwango cha juu. Lengo langu ni kushirikiana na wachezaji wenzangu, kuboresha kiwango cha timu na kuifanya Yanga kutetea ubingwa wa ligi,” amesema na kuongeza:

“Najua ukubwa wa Yanga na presha iliyopo, hivyo nipo tayari kukabiliana na hilo, nimekuwa na marafiki kwenye klabu hii naamini watakuwa msaada kwangu wakati ambao napambana kuzoea maisha mapya.”

Damaro ambaye huu ni msimu wake wa pili kucheza soka nchini, anaweza kuisaidia Yanga kuwa na uwiano mzuri katika eneo la kati kutokana na uwezo wake wa kuzuia mbele ya mabeki wawili wa kati na kusukuma mashambulizi. Wataalamu wanasema kuwa ni mchezaji ambaye anaweza kubadilisha mwendo wa mechi kutokana na uwezo wake kupiga pasi ndefu, jambo linalomfanya kuwa nyongeza muhimu kwa kikosi cha Yanga.

Nyota wa zamani wa Yanga, Jerson Tegete anaamini usajili wa Damaro utapanua chaguo la kocha, Pedro Goncalves raia wa Ureno kwenye safu ya kiungo mkabaji na kuongeza ushindani ndani ya kikosi.

“Ni mchezaji mzuri na mwenye nguvu. Anaweza kucheza kwenye nafasi mbalimbali za kiungo, naamini atakuwa msaada. Ushindani ndani ya kikosi ni mzuri sana kwa timu na nina uhakika Damaro ataongeza kitu,” amesema.

Katika eneo la kiungo, Damaro atakuwa na kibarua cha kupigania namba mbele ya Duke Abuya, Mudathir Yahya na Aziz Andabwile.

Damaro atakuwa mchezaji wa nne kutoka Singida Black Stars kutua Yanga kwa mkopo, awali Israel Mwenda na Andabwile waliichezea timu hiyo kwa mkopo kabla ya kusajiliwa jumla mwingine ni Frank Assinki ambaye bado anatumikia mkataba wake wa mkopo hadi mwisho wa msimu.

Mbali na Damaro, inatajwa kuwa Yanga tayari imemalizana tayari na Singida Black Stars kuhusu Marouf Tchake ambaye naye mwenzake kwa ajili ya kuichezea timu hiyo ya Wananchi kwa mkopo.

Katika dili hilo, inatajwa kuwa Singida Black Stars yenyewe itawachukua Mohamed Doumbia na Balla Moussa Conté ambao hata hivyo inaelezwa wamegomea hilo na wanashikinikiza kuwa tayari kumalizana na Yanga ili kwenda sehemu nyingine nje ya Tanzania kwa ajili ya kuendelea na maisha yao ya soka.