Bajaber aing’arisha Simba Mapinduzi Cup, Chamou mchezaji bora

SAFARI ya Simba kulisaka taji la tano la Mapinduzi, imeanza vizuri baada ya kiungo wa timu hiyo, Mohamed Bajaber kufunga bao pekee katika ushindi wa 1-0.

Simba imepata ushindi huo katika mechi ya kundi B dhidi ya Muembe Makumbi City iliyochezwa leo Januari 3, 2026 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Unguja.

Bajaber amefunga bao hilo dakika ya 21, kufuatia mabeki wa Muembe Makumbi City kujichanganya walipokuwa wakipambana kuokoa hatari.

Kocha wa Simba, Steve Barker, leo aliamua kumuanzisha Baraka Mwangosi katika eneo la ushambuliaji ambapo alionekana kuisumbua safu ya ulinzi ya Muembe Makumbi.

Kipindi cha pili, kadiri muda ulivyokuwa unakwenda, mechi ilionekana kuwa ya ushindani ambapo kila upande ulifanya mabadiliko ya wachezaji, lakini hakukuwa na mabadiliko ya ubao wa matokeo, ikaisha Simba 1-0.

Ushindi huo unamaanisha kwamba, Simba inaongoza kundi B ikiwa na pointi tatu, inafutiwa na Fufuni kisha Muembe Makumbi City zenye pointi moja moja.

Muembe Makumbi City imeshaondoshwa mashindanoni, huku Fufuni ikiwa na nafasi ya kufuzu nusu fainali endapo tu itaifunga Simba.

Kwa Simba, inahitaji sare ya aina yoyote ifuzu nusu fainali kwani kundi hili linatoa timu moja.

Wakati huohuo, beki wa Simba, Chamou Karaboue, amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa mechi hiyo na kukabidhiwa kitita cha Sh1 milioni, huku Yakoub Said Mohamed akipewa Tuzo ya Fair Play iliyoambatana na kiasi cha Sh500,000.