Dereva aliyefungwa Sudan arejea nchini, asimulia

Dar es Salaam. Nderemo na machozi ya furaha vilitawala jijini Dodoma, wakati wa mapokezi ya Juma Maganga, dereva Mtanzania aliyekuwa amefungwa nchini Sudan Kusini.

Maganga alikuwa kizuizini tangu Februari 14, 2025 baada ya gari alilokuwa anaendesha kumgonga na kusababisha kifo cha mwanajeshi.

Alitakiwa kulipa faini ya ng’ombe 51 (sawa na Sh36 milioni) kwa mujibu wa mila na desturi za Sudan kwa ajali inayosababisha kifo.

Ilielezwa mwanajeshi huyo aliacha wake watatu, hivyo wote walitakiwa kupata mgawo pamoja na wazazi wake.

Alipowasili jijini Dodoma leo Januari 3, 2026, Maganga aliangua kilio, akiwakumbatia ndugu na jamaa waliofika kumlaki stendi ya mabasi.

“Nimejisikia faraja nalia kwa uchungu na furaha kwa sababu sikutegemea kama nitakuja kukutana na familia yangu au Watanzania wenzangu, kwani nilikiwa nusu ya jehanamu,” amesema katika video iliyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii.

Amesema ameachiwa baada ya kulipa fidia ya Sh36 milioni iliyotokana na michango kutoka kwa wananchi, viongozi wa Serikali na vyama vya madereva wa magari makubwa.

“Nimeishi maisha magumu, mahabusu niliyokuwapo hawapiki chakula, hakuna msaada wowote hadi uwe na hela. Nilipopata shida ya chakula nilirudi kuomba msaada wa hela huku, nashukuru hawakunichoka,” amesema.

Amesema alipata msaada wa fedha kwa kuwa waliruhusiwa kukaa na simu ambazo walizitumia kupiga kwa ajili kuomba. Anaeleza hali hiyo haikuwa kwake tu, bali kwa wote waliokuwa wameshikiliwa.

“Mle ndani tulikuwapo watu wa kutoka maeneo mbalimbali, walikuwapo Waganda, Wasomali na Wakenya.  Wasomali walikuwa wanakamatwa kwa kukosa hati za kusafiria,” amesema akieleza:

“Nilikuwa naiwaza familia, nimekaa na minyororo miguuni kwa miezi minane. Septemba 2025 ndipo nimefunguliwa.”

Amesema jambo hilo lilimfanya kuendelea kutafuta namna ya kupata msaada aweze kuachiwa, ikiwamo kuomba msaada kutoka kwa watu mbalimbali, akiwamo Waziri wa Madini, Antony Mavunde.

“Ilifika wakati nilikuwa nikienda mahakamani wanakuja wanajeshi kama wanaenda vitani kwa sababu nilimuua mwanajeshi. Baada ya rufaa ya kwanza familia iliondoka ikaliachia jeshi,” amesema.

Anasema siku ya ajali alikuwa akijaribu kulipita gari lililoharibika upande wake wa kulia, hivyo alipohamia kushoto iliingia pikipiki iliyokuwa ikiendeshwa na mwanajeshi, hivyo alipunguza mwendo kumkwepa ili kurudi kulia, upande anaopaswa kuutumia.

“Nilipokuwa nahama naye akahama, mwisho wa siku nilimsukuma akaangukia pembeni. Niliposimama ili nikamwangalie kama ameumia, nilianza kushambuliwa na wananchi,” amesema na kuongeza:

“Sikuweza kujua kama mwanajeshi huyo alikufa au hakufa kwani sikumuona kama ni mzima au si mzima. Mara zote nilikuwa naonana na ndugu wa marehemu mahakamani.”

Maganga amesema awali alipokwenda mahakamani hakuwa anaelewa chochote kutokana na lugha iliyotumika.

Baadaye kampuni anayofanya kazi ilitafuta mwanasheria wa Sudan amsaidie lakini alipotea katika mazingira ya kutatanisha.

Anaeleza Nickson Massawe, Mtanzania aliye nchini humo aliposikia kuna raia wa Taifa lake anashikiliwa alimtafuta akiwa na wenzake ili kumsaidia.

“Walitafuta mwanasheria lakini kila aliyepatikana alitishiwa kuuawa, ikafika mahali tukakata tamaa. Wa pili alitafutwa na Umoja wa Mataifa akawa analipwa Dola 100 za Marekani (zaidi ya Sh200, 000) kila siku ya kesi,” anasema.

Anasema hadi alipotoka zimelipwa Dola 14,500 (Sh35.887 milioni) zikiwa ni fidia na gharama za mazishi.

Kwa upande wake, Waziri Mavunde aliyeisaidia familia ya Maganga inayoishi jijini Dodoma pamoja na Maganga akiwa Sudan, amesema alifahamu suala hilo Septemba 2025 akiwa kwenye kampeni Mtaa wa Sogeambele, Kata ya Chihanga-Dodoma.

Amesema akiwa hapo, mama mmoja aliomba kuuliza swali na alipopewa fursa hakuuliza badala yake aliangua kilio akimwomba mwanaye Juma Maganga aliye gerezani Juba, Sudan Kusini asaidiwe arejee uraiani na kuungana na familia yake.

Amesema wakati anapokea malalamiko hayo, taratibu za kuchangishana ziliendelea na kupitia Watanzania walio Juba na nchini ili kumaliza changamoto hiyo lakini fedha hazikufika lengo, hivyo aliendelea kusota gerezani kwa miezi 10 akiwa amefungwa minyororo muda wote.

“Sikujua kama yule ni mama mzazi wa Juma lakini nikamjulisha mama kwamba nalifahamu tatizo la mwanaye na tunaendelea kumsaidia, nikampa taarifa tu kwamba kwa muda wote akiwa gerezani, nilikuwa mamsaidia chakula chake kule Sudan. Naisaidia familia yake iliyopo hapa Dodoma kupata mahitaji muhimu,” amesema.

Mavunde amesema kwa wakati huo alimtia moyo mama wa Juma kuwa mwanaye atatoka na kupitia ushirikiano wa Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje.

“Wiki iliyopita Mtanzania aitwaye Nickson alinipigia simu na kunijulisha wamejiridhisha kwamba zikipatikana Dola 1,500 ziada ya zile za awali (Dola 2,000) Juma ataachiwa. Tulifanya malipo ya Dola 1,500 kule Mahakama ya Juba, Sudan Desemba 29, 2025 na aliachiwa Desemba 31, 2025,” amesema.