Arusha. Ilianza kama kesi ya mauaji iliyoonekana kumalizika miaka kadhaa iliyopita, lakini Desemba 29, 2025, ukurasa mpya ulifunguliwa katika maisha ya Jackson Wambura.
Siku hiyo, Mahakama ya Rufaa iliyoketi Dar es Salaam ilifuta hukumu ya kunyongwa hadi kufa aliyokuwa amepewa, baada ya kubaini kuwa safari ya kesi yake ilijaa dosari za kisheria zilizovunja msingi wa haki.
Wambura alihukumiwa Aprili 25, 2024 na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, baada ya kupatikana na hatia ya mauaji ya Amedeus Kilawila.
Tukio hilo lilidaiwa kutokea Mei 28, 2010 katika eneo la Kimara Temboni, Wilaya ya Kinondoni, ambako Kilawila aliuawa kwa kupigwa risasi nje ya nyumba yake.
Katika shtaka hilo, Wambura alishtakiwa pamoja na watu wengine wawili ambao waliachiwa huru, yeye akahukumiwa kunyongwa.
Lakini safari ya haki haikuishia hapo. Wambura aliwasilisha rufaa, akipinga mwenendo mzima wa kesi iliyomhukumu kifo.
Rufaa hiyo ilisikilizwa na jopo la majaji wa Mahakama ya Rufaa, Ferdinand Wambali, Lucia Kairo na Deo Nangela, ambao wamekubaliana kwamba kulikuwa na makosa makubwa ya kisheria yaliyoifanya kesi hiyo kuwa batili.
Majaji walipochambua kumbukumbu za mahakama, walibaini mkanganyiko katika uendeshaji wa kesi.
Shauri hilo lilisikilizwa na mahakimu kadhaa katika hatua tofauti, ambao ni Kwey Rusema, Huruma Shaidi, Cyprian Mkeha na Revocatus Rutatinisibwa. Baadhi yao waliisikiliza kesi hiyo zaidi ya mara moja.
Hata hivyo, kilichokosekana ni jambo la msingi, amri rasmi ya kuhamisha kesi kutoka kwa hakimu mmoja kwenda kwa mwingine, kama inavyotakiwa na sheria.
Jamhuri katika kesi hiyo ilikuwa na mashahidi wanane na vielelezo viwili.
Ilielezwa mrufani na washtakiwa wengine wawili walitambuliwa vyema katika eneo la tukio na shahidi wa kwanza na wa pili na pia wakati wa gwaride za utambuzi zilizofanywa na shahidi wa sita na wa saba. Mrufani na wenzake walikana kutenda kosa hilo.
Wambura alidai Julai 20, 2010, aliitwa na Ofisa wa Polisi Mwakyembe katika Kituo cha Polisi cha Mazizini, kisha akahamishiwa Kituo cha Polisi cha Stakishari na baadaye Kituo cha Polisi Oysterbay. Pia alidai alipigwa akituhumiwa kumuua Amedeus.
Baada ya kutiwa hatiani na kuhukumiwa adhabu ya kifo, huku wenzake wakiachiwa huru, alikata rufaa akiwa na sababu sita za kufanya hivyo.
Miongoni mwa sababu ni ukiukwaji wa sheria katika amri za uhamisho wa shauri hilo ambapo wakili wake aliieleza Mahakama kuwa uhamisho wa kesi ya msingi kwa ajili ya usikilizwaji kwa hakimu aliyeongezewa mamlaka, ulikuwa na ukiukwaji wa sheria.
Alidai hakukuwa na amri rasmi za uhamisho wa kesi kutoka kwa hakimu mmoja kwenda kwa hakimu mkazi mwingine mwenye mamlaka ya nyongeza kusikiliza kesi ya mauaji. Vilevile, hakuna amri ya uhamisho kutoka Mahakama Kuu kama inavyotakiwa kisheria.
Wakili alidai uhamishaji sahihi wa amri ulipaswa kufanywa chini ya masharti ya kifungu cha 256 A (kwa sasa kifungu cha 274) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA). Aliiomba mahakama kubatilisha mwenendo na hukumu iliyokuwa imetolewa.
Wakili alidai kusikilizwa upya shauri hilo la mauaji haifai kwani haitakuwa kwa masilahi ya haki kufanya hivyo, licha ya kuwa amri ya kusikilizwa upya kwa kesi ni hatua ya kawaida kuchukuliwa na mahakama baada ya kufuta kesi iliyokosewa.
Vilevile, alidai mashahidi wa upande wa mashtaka hawakuwa wa kuaminika na kwamba, vielelezo vilivyokubaliwa havikupatikana kwa mujibu wa sheria.
Upande wa Jamhuri ulikubaliana na hoja kuwa uhamisho wa kesi hiyo haukuwa kwa mujibu wa sheria na kuongeza kuwa ukiukwaji huo ulisababisha upotoshaji wa haki.
Ulieleza amri ya kesi mpya itasababisha dhuluma kwa upande wa mrufani kwa sababu hakuna ushahidi wa kutosha kwenye rekodi kuunga mkono kesi ya upande wa mashtaka.
Ulitoa mfano ushahidi kuhusu utambuzi wa mrufani katika eneo la uhalifu uliofanywa na shahidi wa kwanza na wa pili si wa kina kama inavyotakiwa na sheria na kuwa hata utambuzi unaodaiwa wa mrufani wakati wa gwaride la utambuzi hauwezi kutegemewa kuthibitisha kesi kwani ulikuwa na dosari.
Kwa kuzingatia udhaifu katika ushahidi wa shahidi wa kwanza na wa pili pamoja na vielelezo vilivyopo kwenye rekodi, Jamhuri ilieleza madai ya kuwa mrufani alitambuliwa eneo la tukio yalibaki bila kuthibitishwa.
Katika kuunga mkono msimamo huo, ulirejelea uamuzi wa Mahakama ya Rufaa katika kesi mbalimbali na kuomba mahakama iruhusu rufaa hiyo kwa msingi wa uhamisho usiofaa na kumwachia huru mrufani.
Baada ya kusikiliza uwasilishaji wa pande zote, majaji wameeleza kulingana na rekodi ya rufaa ni muhimu kukumbuka kwamba kesi ya mrufani iliongozwa na mahakimu kadhaa wakazi wenye mamlaka ya ziada katika hatua tofauti za kesi hiyo.
Wamesema Hakimu Rutatinisibwa aliyehitimisha kesi hiyo na kumtia hatiani mrufani kwa kosa la mauaji, uamuzi wake ndio unaohusika na rufaa.
Majaji wamesema Mahakama Kuu inapaswa kutoa amri maalumu ya kuhamisha kesi kutoka kwa hakimu mmoja kwenda kwa mwingine na amri hiyo haiwezi kuwa ya jumla au kuruhusu hakimu mwingine kuchukua kesi bila amri mpya.
Amesema kushirikishwa kwa mahakimu ambao hawakuwa na amri halali, kulifanya mwenendo wa kesi kuwa batili kuanzia hatua za awali hadi mwisho.
“Kutokana na hali iliyofichuliwa kuhusu ushiriki wa mahakimu wakazi wanne wenye mamlaka ya ziada wakati wa kesi hiyo, ni wazi kwamba kulikuwa na mkanganyiko kuhusu uhamisho wa kesi hiyo,” amesema Jaji Wambali kwa niaba ya jopo.
Amesema wakizingatia mkanganyiko kuhusu ushiriki wa mahakimu wengine ambao hawakuwa na mamlaka ya kusikiliza kesi kama walivyoonyesha, uhamisho wa kesi haukufanyika kulingana na matakwa ya sheria na kufanya kesi kuwa batili.
Majaji hao wamehitimisha kuwa wanakubaliana na hoja za pande zote kwamba kesi hiyo ikiendelea tena itasababisha upotoshaji wa haki.
Kwa mujibu wa Mahakama ya Rufaa, ni Mahakama Kuu pekee yenye mamlaka ya kutoa amri maalumu ya kuhamisha kesi ya mauaji kutoka kwa hakimu mmoja kwenda kwa mwingine.
Kukosekana kwa amri hizo kulimaanisha kuwa baadhi ya mahakimu walioshiriki hawakuwa na mamlaka halali ya kuisikiliza kesi hiyo.
Dosari hiyo ilifanya mwenendo mzima wa kesi, kuanzia mwanzo hadi mwisho, kuwa batili.
Mbali na hilo, Mahakama ya Rufaa ilikubaliana na hoja za pande zote kwamba ushahidi uliotolewa dhidi ya Wambura haukuwa wa kuaminika.
Mashahidi waliodai kumtambua katika eneo la tukio hawakutoa maelezo ya kina yanayohitajika kisheria, huku taratibu za gwaride la utambuzi zikionekana kuwa na upungufu. Kwa mtazamo wa Mahakama nbya Rufani, madai ya utambuzi yalibaki bila kuthibitishwa ipasavyo.
Katika uamuzi wao, majaji walieleza wazi kuwa kuamuru kesi hiyo isikilizwe upya kungekuwa kinyume cha masilahi ya haki, kutokana na udhaifu wa ushahidi na ukiukwaji wa taratibu za msingi.
Mahakama ya Rufaa ilitumia mamlaka yake chini ya kifungu cha 4(2) cha Sheria ya Mahakama ya Rufaa (AJA) kubatilisha mwenendo mzima wa kesi, kufuta hukumu ya kifo na kuamuru Jackson Wambura aachiliwe huru.
Baada ya zaidi ya muongo mmoja tangu tukio la mauaji kutokea na miaka kadhaa ya kusota gerezani akisubiri hukumu ya mwisho, dosari hizo za kisheria zimemfungulia mlango wa uhuru.
