WIKIENDI ya moto kwelikweli. Huko Ulaya zitapigwa mechi za ligi England, Hispania, Italia na Ufaransa. Mashabiki wanataka kujua timu wanazozishabikia zitatoboa mbele ya wapinzani.
Achana na mechi hizo, Afrika kuna kazi nzito wakati mechi za 16 Bora ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2025 inaanza leo Jumamosi zikipigiwa mbili kabla ya kesho Jumapili kupigwa mbili.
Kwa mujibu wa ratiba ya michuano hiyo ya 35 inayofanyikia Morocco, leo Senegal itakuwa na kibarua dhidi ya Sudan kuanzia saa 1:00 usiku kwenye Uwanja wa Tangier Grand na saa 4:00 usiku itakuwa Mali na Tunisia kwenye Uwanja wa Mohamed V, Casablanca kila moja ikiwania tiketi ya kwenda robo fainali.
Hata hivyo, mashabiki na wapenzi wa soka nchini akili zao zipo kesho kuanzia saa 1:00 usiku wakati Taifa Stars itashuka kwenye Uwanja wa Prince Moulay Abdellah jijini Rabat kukabiliana na Morocco, kisha kufuatiwa na Afrika Kusini dhidi ya Cameroon saa 4:00 usiku kwenye Uwanja wa Al Medina.
Kwa mara ya kwanza katika historia ya soka la Tanzania, Stars inacheza hatua hiyo baada ya kumaliza ikiwa nafasi ya tatu katika Kundi C lililokuwa na Nigeria, Tunisia na Uganda na kuangukia katika kapu la washindwa bora lililotoa timu nne zilizoungana na 12 zilizomaliza nafasi mbili za juu za makundi sita tofauti.
Tanzania imepenya sambamba na Benin, Sudan na Msumbiji, na imepangwa kuvaana na wenyeji ikizikutanisha timu hizo mara ya tisa kwani tayari zilishakutana mara nane katika michuano mbalimbali ikiwamo kufuzu Kombe la Dunia za 2026.
Kimahesabu ni mechi ngumu kwa Stars kwa kuzingatia Morocco imemaliza kinara wa Kundi A ikishinda mechi mbili na sare moja na kuvuna pointi saba, tofauti na Stars ambayo haijashinda mechi yoyote zaidi sare mbili na kupoteza moja mbele ya Nigeria. Lakini hata rekodi ya mechi nane zilizopita zinaonyesha kuwa Tanzania imekuwa mnyonge kwani imepoteza saba na kushinda moja, kitu kinachofanya mashabiki soka nchini kusubiri kwa hamu kuona vijana wa Miguel Gamondi watatokaje mbele ya wenyeji hao wanaongoza kwa ubora Afrika.
Mara ya mwisho Stars kuifunga Morocco ilikuwa Machi 24, 2013 mechi ya kuwania fainali za Kombe la Dunia 2014 kwa kuwachapa Waarabu hao mabao 3-1 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa ambapo aliyekuwa mshambuliaji wa Morocco, Marouane Chamakh aligoma kubadilishana jezi na Mbwana Samatta aliyewatungua mabao mawili.
Katika mechi ya kesho wachezaji watatu waliokuwa katika kikosi hicho kilichoidhalilisha Morocco, Shomari Kapombe, Simon Msuva na Samatta wapo ili kusaka tiketi ya robo fainali kwa mara ya kwanza Afcon baada ya awali kufanya hivyo katika CHAN 2024.
Presha atika mechi hiyo itakuwa kwa Morocco ambayo hesabu zake ni kutinga fainali na kubeba taji ambalo inalisaka tangu ilipotwaa 1976 na kulikosa katika fainali za 2004, hasa kutokana na kikosi hicho kukosolewa na wadau mbalimbali kutokana na mbinu za kocha Walid Regragui.
Presha kubwa kwa Morocco ni mbinu za Gamondi ambaye ameifanya Stars kuwa ngumu kufungika, ambapo mfumo anaoutumia wa 5-4-1 alioutumia kwa Watunisia katika mechi ya mwisho uliwapa ugumu Waarabu hao kupenya ngome ya Stars na pambano kumalizika kwa sare ya bao 1-1.
Ukuta wa Stars ambao umeruhusu mabao manne katika mechi tatu za makundi utakuwa na kazi ya kuwadhibiti mastaa wawili mshambuliaji Ayoub El Kaabi anayekipiga Olympiacos Piraeus na kiungo Brahim Diaz wa Real Madrid ambao kila mmoja amefunga mabao matatu katika mechi tatu za makundi.
Stars iliyofunga mabao matatu katika mechi za makundi kupitia Charles M’Mombwa, Simon Msuva aliyekwambisha kwa penalti na lingine la Feisal Salum itakuwa na kazi kuipenya safu ya Morocco iliyoruhusu bao moja ilipotoka sare ya 1-1 na Mali. Hata hivyo, pamoja na ukubwa wa Morocco na kuwa wenyeji, Stars imewapa matumaini Watanzania kwa kusema itashuka uwanjani kwa nia ya kutafuta matokeo mazuri na wachezaji wamesema “wacha kipigwe tu”. Katika mechi ya leo Stars itatakiwa kutumia mbinu za Mali za kutokubali kuyumbishwa na kelele za mashabiki wa Morocco ambao wanasifika kwa kuwa na ‘kichaa cha soka’ viwanjani ikizingatiwa ndio wenyeji na wanajua kushangilia kwa vaibu linalochanganya wachezaji kwa kelele na viwanja vyao kuwa karibu na eneo la kuchezea.
Kiungo wa Stars, Fei Toto amesema wachezaji hawana presha na mechi hiyo na kwamba wanaiheshimu Morocco ambao ndio wenyeji lakini haitakuwa mechi rahisi kwa timu zote.
“Watu walidhani tungepoteza vibaya mbele ya Tunisia na haikuwa hivyo, tunajua kwamba Morocco ni timu nzuri ina wachezaji wakubwa, lakini hatutakwenda kinyonge, tutapambana kupata matokeo,” amesema Fei Toto aliyefunga bao lililoivusha Stars dhidi ya Tunisia.
Akizungumzia mechi hiyo, rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia amesema kikosi hicho hakina presha na mchezo huo na kwamba wanaamini watakwenda kuonyesha ubora mbele ya wenyeji wa mashindano hayo makubwa Afrika.
“Timu ipo salama tunafurahishwa na namna wachezaji wetu wamecheza mechi tatu zilizopita, tunafahamu hautakuwa mchezo rahisi lakini niwaambie Watanzania wawaombee vijana wao wametuambia watakwenda kulipigania taifa lao ,” amesema Karia.
