Kidia One yapata ajali Kilimanjaro, abiria wanusurika

Moshi. Abiria kadhaa wamenusurika  baada ya basi la Kampuni ya Kidia One lililokuwa likitoka Dar es Salaam kwenda Nairobi nchini Kenya kugongana na lori lililokuwa likitoka Arusha kwenda Moshi katika eneo la Kwasadala, Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro.

Katika ajali hiyo, watu wawili wamejeruhiwa, akiwemo kondakta wa basi la Kidia One na abiria mmoja, ambao walipelekwa Hospitali ya Wilaya ya Hai kwa ajili ya matibabu.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa, amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kusema ilitokea leo asubuhi baada ya dereva wa lori kupoteza uelekeo na kuligonga basi hilo upande wa ubavuni.

Kamanda Maigwa amesema kwa sasa dereva wa lori hilo, Kamombi Habibu Omari, anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kusababisha ajali hiyo.

“Leo Januari 3, majira ya saa 11 alfajiri, kulitokea ajali ya kugongana kwa magari mawili eneo la Kwasadala, Wilaya ya Hai, na kusababisha majeruhi wawili pamoja na uharibifu wa magari,” amesema Kamanda Maigwa.

Ameeleza kuwa lori lililokuwa likitoka Arusha kwenda Moshi lilihama upande wake wa barabara na kuligonga basi la Kidia One lililokuwa likitoka Dar es Salaam kwenda Nairobi nchini Kenya.

Kamanda Maigwa amewataja majeruhi kuwa ni Aisha Raymond (35), mfanyabiashara na mkazi wa Nairobi, aliyeumia paja la mguu wa kushoto, pamoja na kondakta wa basi hilo, Mussa Sumari (29), ambao wote wanapatiwa matibabu Hospitali ya Wilaya ya Hai.

Amesema chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa lori aliyeshindwa kuzingatia sheria za usalama barabarani, huku jitihada za kuondoa magari hayo barabarani zikiendelea.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro limewataka madereva kuendelea kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kuepuka ajali zinazoweza kuzuilika.