Dar es Salaam. Wakati kesi ya uhaini inayomkabili mchungaji Godfrey Malisa ikipangwa kutajwa tena Januari 16,2025, imebainika kuwa upande wa Jamhuri imemfungulia kesi nyingine ya Jinai inayohusiana na makosa ya kimtandao.
Kesi ya uhaini namba 000028333 ya 2025 ilitajwa jana Januari 2,2025 mbele ya Hakimu Mkuu Mkazi Ally Mkama wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi lakini ikaahirishwa hadi Januari 16,2026 kwa kuwa upelelezi wake haujakamilika.
Katika kesi hiyo nyingine namba 000028411 ya 2025, Malisa anatuhumiwa kuchapisha taarifa kwenye mtandao wake wa Youtube, akimdai Rais Samia Suluhu Hassan, anatakiwa kujiuzulu kwa kusimamia mauaji ya maelfu ya watanzania.
Kesi hiyo ambayo nayo imepangwa kutajwa Januari 16,2026 sambamba na kesi ya uhaini, inasikilizwa na Hakimu Mkama na inaangukia katika kifungu namba 16 cha sheria ya makosa ya kimtandao ya mwaka 2015 kama ilivyorejelewa mwaka 2023.
Katika kosa la kwanza, upande wa Mashitaka unadai kuwa mchungaji Malisa alitenda kosa hilo Novemba 15,2025 huko Miembeni katika wilaya ya Moshi na alichapisha maneno hayo katika akaunti ya Youtube yenye jina Godfrey Malisa.
Hati ya mashitaka iliyofunguliwa Novemba 3,2025 inanukuu maneno aliyoyachapisha kuwa alisema: “Samia Suluhu Hassan anatakiwa kujiuzulu mara moja kwa kuwa amekuwa ni Rais aliyesimamia mauaji ya maelfu ya watanzani”.
Upande wa Jamhuri unadai alichapisha maneno hayo akijua fika kuwa taarifa hizo hazikuwa sahihi na zilikuwa na lengo la kupotosha umma wa watanzania.
Katika kosa la pili, anatuhumiwa kufanya uchochezi kinyume na kifungu cha 35 cha Kanuni ya Adhabu sura ya 16 kama kilivyofanyiwa marejeo mwaka 2023.
Maelezo ya kosa ni kuwa Novemba 15,2025 huko Miembeni wilaya ya Moshi, anadaiwa kuchochea umma wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutenda kosa la jinai ambalo ni kufanya mkusanyiko usio halali kinyume cha sheria.
Mbali na kesi hiyo, mchungaji Malisa anakabiliwa na kesi ya uhaini chini ya kifungu 39(2)(d) cha Kanuni ya Adhabu sura ya 16 kama kilivyofanyiwa marejeo na Bunge mwaka 2023, akituhumiwa kuhamasisha mkusanyiko usio halali hapa Tanzania.
Kulingana na hati ya mashitaka, inadaiwa kuwa Novemba 16,2025 huko eneo la Miembeni katika wilaya ya Moshi, akiwa na utii kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na akiwa ndani ya ardhi ya Tanzania, alitenda kosa hilo la uhaini.
Inadaiwa alitengeneza nia ya kuhamasisha umma kushiriki katika kusanyiko lisilo halali kwa lengo la kumtisha mtendaji wa serikali ya Tanzania na alidhihirisha nia hiyo kwa kitendo chake cha kutamka na kuchapisha maneno yafuatayo;-
“Samia Suluhu Hassan…Kabla ya kufika tarehe 9 Desemba uwe umekwishajiuzulu… Kama utang’ang’ania madaraka itakapofika tarehe 9 Desemba kutakuwa na maandamano ambayo hayajawahi kutoka katika bara la Afrika”
Mchungaji Malisa anadaiwa kunukuliwa akisema “Lengo la maandamano ni kumuondoa Samia Suluhu Hassan madarakani na maandamano hayo yatakuwa ni maandamano ya muendelezo mpaka utakapotoka madarakani”
Mshitakiwa huyo hakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa kosa hilo linaloangukia kifungu hicho cha 39(2)(d) ni kosa la uhaini kwa mujibu wa kifungu hicho.
Kifungu hicho kinasema mtu yeyote mwenye utii kwa Tanzania, endapo anaitisha Serikali na kubainisha nia hiyo kwa kuchapisha maandishi or machapisho au kwakitendo chochote cha siri kinachojionyesha cha hali yoyote, atakuwa na hatia ya kosa na endapo atatiwa hatiani atawajibika kwa adhabu ya kifo.
Mchungaji Malisa anaingia katika orodha ya mamia ya watanzania walioshitakiwa kwa kosa la uhaini, iwe kwa kuchapisha maandishi au kushiriki katika maandamano ya Oktoba 29, 2025 ambayo Serikali iliyatangaza ni haramu.
Baadhi ya washitakiwa walifutiwa mashitaka na Mkurugenzi wa Mashitaka Nchini (DPP) baada ya DPP kuwasilisha nia ya kutoendelea na mashitaka dhidi yao chini ya kifungu 91(1) cha sheria ya mwenendo wa makosa ya Jinai (CPA).
Hii ni baada ya Rais Samia kuielekeza ofisi ya DPP, kuwafutia makosa vijana wote walioonekana kushiriki maandamano ya Oktoba 29,2025 kwa kufuata mkumbo, maandamano yaliyosababisha vurugu, vifo na uharibifu wa mali.
Rais alitoa kauli hiyo Novemba 14,2025, alipozungumza katika hotuba yake ya kulifungua bunge la 13 mjini Dodoma akisema ukiangalia video za vurugu hizo, wapo vijana walioingia kwa mkumbo na walikuwa hawajui walitendalo.
Mchungaji Malisa alijitokeza kwenye siasa kwa mara ya kwanza mwaka 2010 alipogombea ubunge Moshi mjini kupitia chama cha Tanzania Labour Party (TLP) na mwaka2015, aligombea urais kupitia CCK na baadae kugombea uspika.
Mwaka 2018 aligombea ubunge Kinondoni kwa chama cha TLP na mwaka 2020 aligombea ubunge jimbo la Moshi Mjini kwa tiketi ya chama cha NCCR Mageuzi na baada ya uchaguzi ule alijiunga na CCM hadi mwaka 2025 alipotimuliwa.
Mwaka 2022 Malisa alijitosa kuchukua fomu na kuwa miongoni mwa makada Tisa waliochukua fomu kugombea uenyekiti wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro.
Hata hivyo, Februari 10,2025 mchungaji Malisa ambaye ni mwanazuoni mwenye shahada ya Uzamivu (PhD), alifukuzwa uanachama wa CCM baada ya kupinga maamuzi ya mkutano mkuu wa CCM uliomteua Rais Samia kuwa mgombea urais.
Maamuzi ya kumfukuza uanachama yalitangazwa na Katibu wa CCM mkoa wa Kilimanjaro, Merce Mollel, akiegemea maamuzi ya Halmashauri Kuu ya CCM mkoa wa Kilimanjaro iliyomuondolea sifa ya kuendelea kuwa mwanachama.
“Malisa amefukuzwa kutokana na kukosa sifa za kuendelea kuwa mwanachama kwa sababu mara kwa mara amekuwa akibeza maamuzi halali yaliyofanywa na mkutano mkuu wa CCM taifa uliofanyika Januari 19,2025,”alieleza Mollel.
Katibu huyo alinukuliwa akidai Malisa amekuwa akitoa matamko ambayo hayaleti umoja na mshikamano ndani ya chama na nchi kutokana na kudai mkutano huo uliomteua Samia kuwa mgombea pekee ulivunja katiba jambo ambalo si la kweli.
Pamoja na kufukuzwa uanachama, bado aliendelea kupinga uteuzi huo kwa kujaribu kufungua kesi mahakamani ambazo hata hivyo hakufanikiwa, ambapo alihamia katika mitandao ya kijamii akiendelea kupinga uteuzi huo.
