‘RAHA ya mpira bao’. Ni kauli ya Kocha Mkuu wa Mbeya City, Mecky Maxime akielezea mipango yake akiahidi mambo mazuri pale Ligi Kuu Bara itakaporejea mapema mwezi huu.
Maxime alitambulishwa kikosini hapo Desemba 16, mwaka jana, akichukua mikoba ya Malale Hmasin, ambapo tayari ameshaanza kibarua huku akisubiri kurejea kwa ligi ambayo imesimama kwa muda kupisha fainali za Afcon 2025 zinazoendelea Morocco.
Kocha huyo mwenye misimamo nje na ndani ya uwanja, anasifika kwa uwezo na uzoefu katika mechi za ushindani akipita timu kadhaa ikiwamo Kagera Sugar, Mtibwa Sugar na KMC na sasa Mbeya City.
Ligi Kuu Bara inatarajia kurejea Januari 22, huku Mbeya City wakianzia ugenini dhidi ya Mtibwa Sugar.
Maxime amesema falsafa yake ni kutoa burudani kwa mashabiki wakishuhudia mabao yakiingia nyavuni, akieleza kuwa makosa aliyoyaona kikosini anayafanyia kazi ili kuhakikisha City inarudi na nguvu mpya.
Amesema kwa sasa mpira umebadilika na katika kuweka kikosi hicho kwenye ubora, hatategemea mchezaji mmoja badala yake anatengeneza msingi wa timu nzima kwa ajili ya kupata matokeo mazuri.
“Ligi ndio inaanza kwetu. Januari itakuwa kama Agosti mwanzo wa ligi, hivyo nitakaa na vijana kusahihisha makosa yaliyoonekana na falsafa yangu ni kutoa burudani uwanjani, huku mabao yanaingia wavuni.
“Sitegemei mchezaji mmoja. Mpira unabadilika yeyote anaweza kufunga na siyo kumuangalia straika. Matarajio yangu ni kuona City ikirejea kwa nguvu mpya ili kuhakikisha tunafanya vizuri,” amesema Maxime.
Hadi sasa Mbeya City inaendelea na mazoezi kujiandaa na mwendelezo wa ligi baada ya kucheza mechi 10 na kukusanya pointi nane na kukamata nafasi ya 13, matokeo ambayo si mazuri sana kwa sasa.
