LEO Jumamosi kuna mechi mbili za Kombe la Mapinduzi 2026 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Unguja ambazo zimebeba matokeo ya kuamua jambo baina ya timu zinazokwenda kukutana.
Saa 10:15 jioni, Singida Black Stars yenye pointi nne, itacheza dhidi ya URA iliyokusanya pointi tatu, ikiwa ni mechi ya Kundi A.
Mechi hii endapo Singida Black Stars ikishinda, itafuzu moja kwa moja nusu fainali kwani itafikisha pointi saba ambazo haziwezi kuitoa nafasi mbili za juu kundi A.
Lakini kama URA itapata ushindi basi nayo itakuwa imefuzu nusu fainali, huku Singida Black Stars huenda ikaumaliza mwendo.
Ipo hivi. Jana Azam yenye pointi moja ilicheza na Mlandege, ushindi kwao maana yake itafikisha pointi nne sawa na Singida ikitokea imepoteza leo.
Singida inamaliza mechi leo, lakini Azam na URA zitabakiwa na moja zitakapomalizana Januari 5, 2026.
Kundi hili linatoa timu mbili kwenda nusu fainali, wakati makundi mengine B na C znapenya mojamoja.
Tayari kocha mkuu wa URA, Mbalangu Hussein, amesema: “Mechi inayofuatia naamini itakuwa nzuri zaidi, tutakuwa tumejiandaa vizuri. Tumekuja hapa kwa ajili ya kushindana na kuwa mabingwa.”
URA iliyowahi kubeba ubingwa wa Kombe la Mapinduzi mwaka 2016, inahitaji kulibeba tena, huku Singida ililisaka kwa mara ya kwanza.
Kocha Msaidizi wa Singida BS, David Ouma amesema: “Mechi iliyopita dhidi ya Azam ilikuwa nzuri sana na kile ambacho wachezaji walikifanya, inatoa morali ya kupata matokeo bora mechi inayofuatia, hicho ndicho makocha huwa tunazingatia.”
URA ilianza na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mlandege, huku Singida BS mechi mbili ilizocheza, imeifunga Mlandege 3-1 kisha sare ya 1-1 dhidi ya Azam FC.
Majira ya saa 2:15 usiku, Simba itashuka dimbani kwa mara ya kwanza katika mashindano hayo kucheza na Muembe Makumbi City ambayo itakuwa mechi ya pili kwao.
Awali Muembe Makumbi City ilitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Fufuni, mechi iliyopigwa Desemba 29, 2025.
Muembe Makumbi inasaka ushindi ili kutengeneza mazingira ya kufuzu nusu fainali ikiwa inashiriki kwa mara ya kwanza. Kumbuka timu hizi zipo kundi B ambapo inapenya moja kwenda nusu fainali.
Simba iliyobeba ubingwa wa Mapinduzi mara nne mwaka 2008, 2011, 2015 na 2022, imepania safari hii kufanya vizuri ili kufikia rekodi ya Azam iliyobeba mara tano ikiwa ndio timu kinara.
Mechi ya leo, Simba kama inataka kufuzu nusu fainali, inailazimu kushinda ili kukusanya pointi tatu na kurahisisha kazi mechi ya mwisho Januari 5, 2026 ikihitaji sare tu dhidi ya Fufuni yenye pointi moja.
Kocha wa Muembe Makumbi, Sheha Khamis Rashid, amesema: “Mechi ya Simba ni ngumu, tunajua Simba kwa Tanzania ni timu kubwa na Afrika pia, tumejipanga ili kushindana nao, zaidi tutakuwa makini sana kwa sababu wenzetu jinsi wanavyocheza, wana wachezaji wazoefu wengi na wanaotoka nje, kikubwa tumejipanga kufanya vizuri.”
