Mlandege yaivaa Azam bila kupiga tizi

JANA Ijumaa, ilipigwa mechi moja ya Kombe la Mapinduzi 2026 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Unguja mabingwa watetezi Mlandege dhidi ya Azam, lakini kuna kitu kilitokea kabla ya mechi hiyo iliyoanza saa 2:15 usiku.

Mlandege iliyopoteza mechi mbili za kwanza ilifungwa 3-1 na Singida Black Stars kisha ikalamba 1-0 na URA, imekuwa ya kwanza kuaga mashindano ikitokea Kundi A.

Kutokana na hali hiyo, uongozi na benchi la ufundi la Mlandege waliamua kusitisha mazoezi kujiandaa na mechi hiyo.

Taarifa kutoka ndani ya Mlandege zinabainisha, baada ya Jumatano iliyopita kufungwa 1-0 na URA wachezaji waliambiwa kesho yake Alhamisi hakuna mazoezi, hivyo watakutana Ijumaa siku ya mechi. “Tuliambiwa hakutakuwa na mazoezi ya aina yoyote kuelekea mechi na Azam, hivyo ratiba ilikuwa ni kukutana siku ya mechi. Hatukuambiwa sababu ni nini,” amesema mmoja wa wachezaji wa timu hiyo.

Mmoja wa viongozi wa Mlandege, amesema uamuzi huo ulifanyika kwa sababu timu haikuwa na nafasi tena ya kusonga mbele, hivyo wakaona hakuna sababu ya kuingia gharama zisizo za lazima.

“Kuna mambo yanaendelea kwenye timu si vizuri kila mmoja kuyafahamu, lakini kiukweli hali sio nzuri. Kuna kama mgomo fulani hivi kwenye timu kwa sababu kuna wachezaji waliletwa kucheza Kombe la Mapinduzi, wapo wanaopata nafasi na wengine hawapati inavyotakiwa. Sasa wale waliokuwepo ni kama hawafurahishwi na hilo wa sababu wamekuja kuchukua nafasi zao. Hiyo imechangia matokeo mabaya,” amesema kiongozi huyo.