Mmoja pekee ajitokeza kupima DNA kutambua miili ajali ya Morogoro

Morogoro. Uongozi wa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Morogoro umesema hadi saa 5:13 asubuhi ya leo Januari 3, 2026 ni mtu mmoja pekee aliyejitokeza kuchukuliwa sampuli za vinasaba (DNA) kwa ajili ya utambuzi wa mwili wa ndugu yake anayeamini ni miongoni mwa waliokufa katika ajali ya basi lililogongana na lori na kisha kuwaka moto Desemba 31, 2025.

Kaimu Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk Joseph Kway, amesema miili mitano kati ya tisa iliyopokewa hospitalini hapo bado haijatambuliwa.

Mwili mmoja ulihifadhiwa Kituo cha Afya Mikese na tayari ulishatambuliwa.

Dk Kway amesema licha ya kuwapo wataalamu kutoka ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, mwamko wa watu kufika kwa ajili ya vipimo hivyo umekuwa mdogo.

“Wataalamu kutoka ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali bado wapo kama kuna mtu anamtafuta ndugu yake na anaamini Desemba 31 alikuwa safarini kupitia barabara ya Morogoro -Dar es Salaam, tunaomba aje achukuliwe sampuli ya vinasaba ajiridhishe kama ndugu yake ni miongoni mwa waliofariki,” amesema.

Kuhusu majeruhi, amesema waliobaki hospitalini ni wawili na wanaendelea na matibabu, huku mmoja amehamishiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa ajili ya matibabu ya kibingwa bobezi.

Amesema idadi ya rufaa zilizotolewa kwa majeruhi wa ajali hiyo ni tatu.

“Majeruhi 14 tuliwaruhusu kurudi nyumbani baada ya kuona hali zao zinaendelea vizuri, hata hawa wawili waliobaki wanaendelea vizuri,” amesema.

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima jana Januari 2, 2026 alikwenda hospitalini hapo kuwajulia hali majeruhi wa ajali hiyo na kutoa maelekezo kama miili hiyo itakaa zaidi ya siku 14 bila ya kutambuliwa na ndugu zao, uongezwe muda kwa ajili ya kutoa fursa kwa ndugu kujitokeza kuitambua.

“Niwaombe wananchi kujitokeza kufanya utambuzi wa DNA huenda ndugu zetu walisafiri bila sisi kujua, hili basi lilianzia safari hapa Morogoro, hivyo kuna uwezekano abiria kutoka mikoa mingine walipanda, wasafiri wakati mwingine wamekuwa wakiungaunga mabasi,” alisema.

Ajali hiyo ilitokea jioni ya Desemba 31, 2025, katika Kijiji cha Maseyu, Kata ya Gwata, Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, barabara kuu ya Morogoro – Dar es Salaam.

Taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi ilisema mbali ya vifo vya watu 10, watu 23 walijeruhiwa katika ajali hiyo iliyohusisha basi la abiria aina ya Mitsubishi Fuso, mali ya Kampuni ya Bill Mawio na lori la mizigo aina ya Howo lenye tela, mali ya Kampuni ya Kikori. Magari yote mawili yaliteketea kwa moto baada ya ajali hiyo.

Basi la abiria lilikuwa likiendeshwa na Swalehe Adamzi, likitokea kituo cha mabasi yaendayo mikoani Msamvu, Morogoro, kuelekea mkoani Tanga, huku lori likiwa na shehena ya mbolea likitokea Dar es Salaam kuelekea mkoani Mbeya.