Patashika wanafunzi wakirejea shuleni | Mwananchi

Dar/Moshi. Maandalizi ya wanafunzi kurejea shuleni yakipamba moto, imeelezwa kuwapo shida ya kupata vitabu vya mtalaa mpya.

Kwa mujibu wa ratiba, shule za msingi na sekondari nchini zitafunguliwa Januari 13, 2026.

Ufuatiliaji uliofanywa na Mwananchi Januari 2, 2026 katika baadhi ya maeneo ya Kariakoo, Karume na Mbezi Mwisho unaonyesha uwepo wa idadi kubwa ya watu wanaofanya ununuzi wa bidhaa za shule.

Katika Mtaa wa Congo na Uhuru ambako kuna maduka mengi yanayouza vifaa vya shule, kulikuwa na msongamano wa watu baadhi wakiambatana na watoto wao ambao wamekuwa wakijaribishwa nguo na viatu.

Said Mohammed, mmiliki wa duka la Miftah linalouza vifaa vya shule kwa bei ya jumla na rejareja katika Mtaa wa Tandamti, Kariakoo, Dar es Salaam, amesema kuna ahueni katika upatikanji wa vifaa hivyo na hata bei haijabadilika.

Amesema hali hiyo inachangiwa na utokaji wa mizigo bandarini kwa urahisi tofauti na zamani ilipokuwa ikichelewa na kusababisha waagizaji wakubwa kuongeza bei ili kulipia gharama ya mizigo kukaa muda mrefu bandarini.

Mbali ya hayo, amesema vitabu ya mtalaa mpya vinapatikana kwa shida, vikiwamo vya darasa la tano na kidato cha pili.

“Kwa kidato cha pili vitabu mpaka sasa vinavyopatikana havizidi vitano ambavyo ni vya masomo ya Hesabu, Biolojia, Kiingereza, Biashara na Historia na Maadili,” amesema.

Kwa upande wa darasa la tano amesema vinavyopatikana ni vya Hesabu, Sayansi na Kiswahili pekee.

Hata hivyo, Serikali imesema tayari imeshasambaza vitabu vya mitalaa mipya takribani kwa shule zake zote nchini.

Imesema ifikapo Januari 5, vitabu hivyo vitakuwa vimeshafika madukani ili kurahisisha upatikanaji wake.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, alieleza hayo alipoulizwa na Mwananchi kuhusu changamoto iliyoelezwa na wafanyabiasha kuhusu upatikanaji wa vitabu hivyo.

“Mpaka kufikia Januari 5, mwaka huu, Serikali itakuwa imeshakamilisha kusambaza vitabu vyote sokoni ili kurahisisha upatikanaji wake,” amesema na kuongeza:

“Takribani shule zote za Serikali zimeshapewa vitabu na ikifika Januari 5, tutakuwa tumeshagawa vitabu vyote. Vile vya kuingia madukani kuuzwa tutahakikisha vimefika Januari 5, mwaka huu.”

Hamza Shukrani, mkazi wa jijini Dar es Salaam, akiwa Mtaa wa Congo, Kariakoo  amesema analazimika kununua vifaa mapema ili kuepuka changamoto za kufanya ununuzi mwishoni.

Kwa upande wake, Waziri Ally, amesema amekwenda kununua madaftari kwa bei ya jumla Kariakoo ili akayauze mtaani hatua itakayomwongezea kipato.

“Ukisema ununue daftari mojamoja inakula kwako, ndiyo maana napambana nipate kwa bei ya jumla kwenye boksi,” amesema.

Agatha Mshana, mkazi wa Mabibo, yeye anasema akinunua vifaa kwa bei ya jumla inamrahisishia kwa kuwa ana watoto wanne ambao wote wanahitaji madaftari.

“Si kila anayekuja huku anapenda kuja kukanyagana, bali tunafuata urahisi kwa kuwa mtaani lazima waongeze bei,” amesema.

Mnunuzi aliyejitambulisha kwa jina moja la Rose amesema ananunua madaftari na vitabu kwa ajili ya shule.

“Kuna wazazi muda wa kwenda kununua vitabu hawana, ila tukiwa navyo shuleni tunawarahisihia kuvipata. Nimekuja kukusanya vifaa vya darasa la kwanza hadi la saba,” amesema na kuongeza:

“Kwa kuwa ni mradi wa shule, ukinunua vingi kuna punguzo unalipata tofauti na ukinunua kimojakimoja. Kitabu cha Sh15,000 unaweza kuuziwa Sh13,000 hadi Sh12,000,” amesema.

Hali ikiwa hivyo, baadhi ya wafanyabiashara wamebadilisha biashara walizokuwa wakifanya na kuhamia kuuza bidhaa za shule.

“Nilikuwa nikiuza nguo za watoto lakini tangu nimalize mzigo wiki moja kabla ya Januari, nimeamua nichukue vifaa vya shule na ninashukuru vinauzika,” anasema mfanyabiashara aliyejitambulisha kwa jina moja la Hussein.

Kwa upande wake, Amani John, anayefanya kazi za uwinga (dalali) anasema hivi sasa biashara ipo kwenye vifaa vya shule.

Kwa upande wake, Ashura Lekule, aliyekuwa akiuza vinywaji, anasema kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya vifaa vya shule ameongeza bidhaa hizo dukani kwake.