Rais wa zamani wa Brazil Aruhusiwa Hospitali, Arudishwa Gerezani



Rais wa zamani wa Brazil Jair Bolsonaro ameondoka hospitalini katika Mji Mkuu wa Brasilia, wiki moja baada ya kufanyiwa upasuaji wa Ngiri mara mbili, na kurudishwa Gerezani chini ya ulinzi wa Polisi wa Shirikisho kuendelea kutumikia kifungo chake cha miaka 27 jela.

Gari lilimsafirisha Bolsonaro kutoka hospitali ya DF Star hadi Makao Makuu ya Polisi, ambako anazuiliwa baada ya kukutwa na hatia ya kuongoza jaribio la Mapinduzi lililolenga kumweka ofisini.

Hospitali ilithibitisha kuwa Bolsonaro aliruhusiwa kufuatia taratibu za ziada za matibabu, ikisema upasuaji ulikuwa umekamilika bila matatizo.

Mahakama ya juu ya Brazil ilikuwa imeidhinisha kuachiliwa kwa Bolsonaro kwa muda kutoka Gerezani ili kufanyiwa operesheni hiyo.

Hata hivyo, Jaji wa Mahakama ya juu Alexandre de Moraes, ambaye alimhukumu, alikataa ombi la kuhukumiwa kifungo cha nyumbani.