Dar es Salaam. Serikali imetenga Sh125 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa mabwawa saba katika mikoa ya Morogoro na Dodoma baada ya upembuzi yakinifu kukamilika.
Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo amesema hayo alipopewa nafasi na Waziri Mkuu, Mwigulu Nchemba kuwasalimia wakazi wa Gulwe, Mpwapwa mkoani Dodoma.
Dk Mwigulu jana Januari 2, 2026 alifanya ukaguzi wa athari za mafuriko kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha nchini.
Akieleza mikakati ya Serikali, Chongolo amesema kazi inayofanyika kwa sasa ni kutafuta namna ya kuhifadhi maji ili yatumike kwa shughuli za kilimo katika wilaya za Mpwapwa na Kilosa.
“Awamu ya kwanza ya ujenzi wa bwawa la Msagali umekamilika, kazi inayofuata ni ujenzi wa mifereji na miundombinu ya umwagiliaji. Awamu ya pili itakuwa na kazi ya upanuzi wa bwawa ili tuweze kuhifadhi maji mengi zaidi,” amesema Chongolo katika taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu.
“Serikali imetoa Sh125 bilioni. Ndani ya miezi mitatu hadi minne, tukikamilisha kazi ya upembuzi yakinifu, tunaanza kazi ya ujenzi wa mabwawa ya Kidete, Kimagai, Buigiri, Ikoa, Hombolo, Dabalo na kukamilisha hili la Msagali. Kazi iliyo mbele yetu ni kuimarisha kilimo cha umwagiliaji katika bonde linalounganisha Mpwapwa, Kilosa na Mvomero.”
Wakati huohuo, Waziri wa Fedha, Balozi Khamisi Omari amesema Serikali imeshatoa Sh5.3 bilioni ambazo ni gharama za awali za ujenzi wa barabara ya lami kutoka Mpwapwa hadi barabara kuu ya Dodoma – Morogoro.
Amesema gharama zote za ujenzi wa barabara hiyo ni Sh53 bilioni.
Katika hatua nyingine, Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, amesema Reli ya Kisasa (SGR) ipo salama na Shirika la Reli Tanzania (TRC) litaendelea kuchukua tahadhari kwa ajili ya usalama wa abiria wanaotumia huduma hiyo.
Akigusia hilo, Dk Mwigulu amesema jambo linalofanywa na TRC kwa kushirikiana na Wizara ya Uchukuzi ni la msingi ili kujiridhisha na usalama wa reli hiyo.
Akizungumza kwa nyakati tofauti na wananchi wakati akikagua athari za mvua katika maeneo ya Tindiga, Kidete, Godegode mkoani Morogoro na Gulwe mkoani Dodoma, Dk Mwigulu amesema ujenzi wa mabwawa aliyoleza Chongolo utakuwa suluhisho la kudumu la mafuriko katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Morogoro.
Amesema uamuzi wa Serikali wa kujenga mabwawa katika eneo la Kidete ni uthibitisho kuwa ipo makini katika kuhakikisha inakabiliana na changamoto za wananchi na imeshachukua hatua kupata suluhisho la kudumu.
