Tanga. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Tanga imevuka lengo la makusanyo ya kodi kwa asilimia 139 baada ya kukusanya Sh252.8 bilioni katika kipindi cha miezi sita ya kwanza ya mwaka wa fedha 2025/2026, kuanzia Julai hadi Desemba 2025.
Kiasi hicho ni zaidi ya lengo la Sh181.9 bilioni walilopangiwa kukusanya katika kipindi hicho.
Kauli hiyo imetolewa leo na Meneja wa TRA Mkoa wa Tanga, Thomas Masese, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano wa kutangaza mafanikio ya makusanyo ya kodi kwa robo ya pili ya mwaka wa fedha unaoishia Desemba 2025.
Masese amesema kwa mwaka wa fedha 2025/2026, Mkoa wa Tanga umepewa lengo la kukusanya jumla ya Sh373 bilioni.
Ameeleza kuwa makusanyo ya Julai hadi Desemba 2025 yameonesha ongezeko kubwa ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka uliopita.
“Katika kipindi cha Julai hadi Desemba 2024 tulipangiwa kukusanya Sh162.9 bilioni, lakini tulikusanya Sh178.3 bilioni, sawa na ufanisi wa asilimia 109,” amesema Masese.
Amesema ukuaji wa makusanyo ya kodi umeongezeka kwa Sh74.5 bilioni, sawa na asilimia 42, ikilinganishwa na vipindi hivyo viwili, akieleza kuwa mafanikio hayo yanatokana na kuongezeka kwa uzalendo wa walipakodi pamoja na ufanisi wa mifumo ya ukusanyaji wa kodi.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Wadogo Tanzania, Ismail Masood, amewataka watumishi wa TRA kuendelea kubuni na kuboresha mifumo rafiki kwa wafanyabiashara wapya ili kuwahamasisha kulipa kodi kwa hiari.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara Wanawake, Aziza Ramadhani, amewahamasisha wananchi kudai risiti kila wanaponunua bidhaa, akisisitiza kuwa kodi ni nguzo muhimu ya maendeleo ya Taifa.
Pia, amewataka wafanyabiashara kuwa mstari wa mbele katika kutoa risiti kwa wateja wao.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chemba ya Taifa ya Biashara, Rashedi Mwanyoka, ameishauri TRA kuendelea kuchukua hatua zitakazoongeza makusanyo ya mapato, akibainisha kuwa maboresho yaliyofanyika katika Bandari ya Tanga yamechangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa makusanyo ya kodi mkoani humo.
Mafanikio ya kuvuka lengo la makusanyo kwa asilimia 139 yanaonesha umuhimu wa ushirikiano kati ya TRA, wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla katika kuongeza mapato ya Serikali na kuchochea maendeleo ya Mkoa wa Tanga.
