Trump aishambulia Venezuela, Rais Maduro na mkewe waondolewa nchini

New York. Rais wa Marekani, Donald Trump ametangaza kuwa ameamuru jeshi la nchi hiyo kutekeleza shambulio kubwa la kijeshi nchini Venezuela na kwamba Rais Nicolas Maduro, pamoja na mkewe, wamekamatwa na kuondolewa nchini humo.

Kauli hiyo, iliyotolewa mapema Jumamosi kupitia mtandao wa kijamii wa Truth Social, imezua taharuki na mvutano wa kisiasa na kiusalama katika mji mkuu, Caracas na kuibua wito wa jumuiya ya kimataifa kufuatilia hali hiyo kwa karibu.

Trump amesema operesheni hiyo ilifanywa kwa ushirikiano na vyombo vya sheria vya Marekani na kuthibitisha kuwa ni “shambulio la kijeshi lililofanikiwa kikamilifu.”

“Rais Nicolás Maduro na mkewe wamekamatwa na kuondolewa nchini Venezuela,” aliongeza Trump, akiahidi kutoa maelezo zaidi katika mkutano na waandishi wa habari uliopangwa kufanyika baadaye katika makazi yake ya Mar-a-Lago.

Hata hivyo, hadi sasa hakuna uthibitisho huru kutoka Pentagon, Jeshi la Marekani, au mamlaka za Venezuela kuthibitisha kukamatwa kwa Maduro, huku Serikali ya Venezuela ikilitaja shambulio hilo kama uvamizi wa kijeshi na propaganda za kisiasa.

Mashuhuda walioko Caracas wameripoti kuona milipuko kadhaa, ndege zikizunguka angani na moshi ukipaa kutoka kwenye kambi ya kijeshi mapema alfajiri ya Jumamosi.

CNN iliripoti kuwa mlipuko wa kwanza ulitokea saa 1:50 usiku, ukilenga maeneo mbalimbali ikiwemo Fort Tiuna, ambayo ni makao makuu ya Wizara ya Ulinzi ya Venezuela. Baadhi ya wakazi walikimbilia barabarani wakiwa na hofu kubwa huku ardhi ikitikisika kutokana na milipuko hiyo.

Carmen Hidalgo, mkazi wa Caracas, alisema: “Tulihisi kama hewa inatupiga. Ilikuwa ni hali ya kutisha sana.”

Serikali ya Venezuela, kupitia taarifa rasmi, imekemea mashambulio hayo na kuwataka wananchi wake kujitokeza mitaani kupinga uvamizi huo.

“Serikali ya Mapinduzi ya Bolivarian inawahimiza wananchi wote, vikosi vya kijamii na kisiasa kuhamasika na kupinga shambulio hili la kibeberu,” imesema taarifa hiyo, huku ikiongeza kuwa Rais Maduro ameagiza mipango yote ya ulinzi wa taifa kuanza kutekelezwa mara moja.

Wizara ya Mawasiliano ya Venezuela pia imelaani vikali kile ilichokiita uchokozi wa kijeshi wa Marekani na kuutaja kama ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa.

Mashambulio haya yanakuja katika kipindi cha mvutano mkali kati ya Marekani na Venezuela, huku Trump akiongeza shinikizo dhidi ya Maduro kwa kile anachodai kuwa ni kushindwa kudhibiti biashara haramu ya dawa za kulevya.

Marekani tayari imeendesha operesheni kadhaa baharini dhidi ya vyombo vinavyodaiwa kuhusika na usafirishaji wa dawa hizo katika Bahari ya Caribbean na Pasifiki.

Desemba mwaka jana, CIA iliripotiwa kufanya shambulio la ndege zisizo na rubani katika bandari moja ya Venezuela, madai ambayo hayajathibitishwa rasmi.

Rais wa Colombia, Gustavo Petro, ametumia mtandao wa X kutoa wito wa dharura kwa Jumuiya ya Nchi za Amerika (OAS) na Umoja wa Mataifa, akisema shambulio hilo ni tishio kwa amani ya kikanda.

Hali ya usalama Caracas na maeneo mengine inaendelea kuwa ya wasiwasi huku jumuiya ya kimataifa ikifuatilia kwa karibu maendeleo ya tukio hili linaloweza kubadilisha kwa kiasi kikubwa mwelekeo wa mahusiano kati ya Marekani na Venezuela.