Uharibifu SGR waibua maswali | Mwananchi

Dar/Dodoma. Wakati baadhi ya wananchi wakikosoa usanifu na ujenzi wa mradi wa Reli ya Kisasa (SGR) baada ya kusimama kwa huduma kutokana na athari za mvua, Shirika la Reli Tanzania (TRC), limesema sababu za kusimamishwa hazihusiani na kasoro zinazotajwa.

Akizungumza na Mwananchi Januari 2, 2026, Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Machibya Masanja, amesema kilichotokea ni kumomonyoka kwa kingo za mto lilikopita daraja la reli hiyo.

Kwa hatua za tahadhari amesema wameona wasimamishe huduma kuimarisha kingo hizo.

Desemba 31, 2025 TRC ilitangaza kusitisha safari za SGR kati ya Morogoro-Dodoma na Dodoma-Morogoro, ikitaja sababu ni uharibifu wa miundombinu uliosababishwa na mvua katika maeneo ya Kidete wilayani Kilosa mkoani Morogoro na Godegode, wilayani Mpwapwa, mkoani Dodoma.

Taarifa hiyo iliibua ukosoaji wa usanifu na ujenzi wa mradi huo kutoka kwa baadhi ya wananchi na wanasiasa, wakihoji inawezekanaje reli iliyojengwa ndani ya mwaka mmoja ianze kuwa na hitilafu.

Kupitia ukurasa wa mtandao wa X, Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, John Heche amekosoa ujenzi huo akiuhusisha na uhujumu wa nchi.

“Mradi mkubwa wa matrilioni ya fedha kama huu, haujamaliza hata mwaka… Infact (kwa kweli) haujafika hata Mwanza. Kwa nini haukufanyika upembuzi yakinifu, detail design (usanifu wa kina), kwenye miradi mikubwa fedha zinalipwa nyingi mno kwa sababu ya mambo kama hayo,” ameandika Heche.

Hoja inayowiana na hiyo imetolewa na mwananchi mwingine kupitia WhatsApp, akisema Taifa lisikubali kuingia gharama kwa kuwa mradi upo katika hatua ya uangalizi.

Amehusisha kilichotokea na uwezo duni wa mkandarasi, akisema huo ndio mradi wake wa kwanza, hivyo alikuwa anajifunza.

“Huu ndio mradi wao wa kwanza kuufanya mkubwa… so (hivyo) lazima ukubali kuwa it was a learning trail (ilikuwa kujifunza),” ameandika.

Amesema itakuwa kosa iwapo fedha za walipakodi ndizo zitakazotumika kurekebisha mradi na aajiriwe mkandarasi binafsi kupitia mradi wote na kama kuna kasoro zirekebishwe.

Kwa upande wake, Martin Masese kupitia ukurasa wake wa X, ameandika uharibifu wowote kwa sasa ni jukumu la mkandarasi na anapaswa kulipa fidia.

Vilevile amekosoa usanifu wa mradi huo, akidai kuna upigaji uliofanyika ndiyo sababu yametokea yaliyotokea.

Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Masanja amesema kilichotokea hakina uhusiano na kasoro za usanifu wala upembuzi yakinifu wa mradi wa SGR, kwani hata reli haijakatika kama inavyodaiwa.

Anaeleza kilichotokea ni kumomonyoka kwa kingo za mto lilipo daraja, jambo lililosababishwa na maji ya mvua yaliyoambatana na uchafu na mchanga ambao ni matokeo ya shughuli za binadamu.

“Reli haijakatika, ambacho kimetokea ni kwamba kuna mto kingo zake zimemomonyoka, kwa ajili ya usalama wa wananchi na vifaa tukasema tusimamishe huduma ili turekebishe na kuepusha hatari,” amesema.

Uamuzi wa kusimamisha huduma amesema umelenga kuwaepusha wananchi na treni husika dhidi ya hatari za kiusalama kwa kuwa kingo zimeanza kumomonyoka hasa kutokana na shughuli zinazoharibu usalama wa mto huo.

“Si kwamba treni haiwezi kupita, lakini unachukua tahadhari kwa kufanya marekebisho ya kingo za mto, kuziimarisha. Mimi mwenyewe kichwa cha treni niliyopanda kimepita hapo sasa hivi,” amesema alipozungumza na Mwananchi saa 6:51 mchana wa Januari 2.

Baada ya kumomonyoka kwa kingo hizo, amesema wanaangalia uwezekano wa kurekebisha ili kuepusha hatari tarajiwa na si kwamba reli imekatika.

“Anayesema upembuzi yakinifu haukufanyika sisi ni wahandisi tunafanya kazi kwa vitendo siyo maneno maneno, daraja limejengwa kuhimili miaka 120 ijayo kwa hiyo haliwezi kukatika,” amesema.

Amesema msingi wa daraja hilo umejengwa mita 30 kwenda chini sawa na nyumba ya ghorofa 10 au zaidi, huku nguzo zikienda chini kati ya mita 30 hadi 40, hivyo hakuna namna zitakatika kabla ya miaka 120.

Ameeleza hata madaraja ya reli ya zamani (MGR) yanayoonekana kuathirika sasa, yalisanifiwa miaka 100 iliyopita, hivyo muda wake wa kudumu ulishapita.

Masanja amesisitiza reli haijachukuliwa na maji, bali wamesimamisha huduma kuimarisha kingo za mto lilikopita daraja na haihusiani na upembuzi yakinifu wala usanifu wa mradi.

Katika stadi ya upembuzi yakinifu, ameeleza walibaini hatari ya mito kukumbwa na athari kutokana na ukataji miti, hivyo kumekuwa na mpango wa muda mrefu wa ujenzi wa bwawa ili maji yawe yanaingia huko.

Amesema bwawa hilo litasababisha mtiririko wa maji mzuri kwenye mto na kufanya kingo ziendelee kuwa imara bila kuathiriwa na mafuriko.

Akizungumza katika ziara eneo lililoathirika Januari 2, Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, amesema si jambo la ajabu kuona safari za SGR zinaahirishwa, akisisitiza ni hatua nzuri kuwa na taarifa za mapema kabla hatari haijatokea kwa kuwa inanusuru wananchi.

“Ikitokea mvua ya upepo inayotikisa nyaya, mtiririko wa umeme hautakuwa wa kawaida. Wale wanaoitakia mabaya Tanzania wanataka watu waendelee kupita. Hata viazi mviringo usingevipeleka unataka watu wapite na mvua ya upepo inanyesha kwenye treni inayotumia umeme,” amesema.

Dk Mwigulu amesema vivyo hivyo hata mashirika makubwa ya ndege ya kimataifa ikitokea mvua kubwa ya upepo huahirisha safari na imeshatokea mara kadhaa.

“Kwenye masuala yanayohusisha usalama wala tusigombane, tusilaumiane, hiyo shughuli tunayoiwahi tutaifanya tu tukiwa hai,” amesema.

Ametaka wataalamu wakamilishe masuala ya kitaalamu ili ujenzi wa mabwawa uanze na kupatikana suluhu ya kudumu ya kuhifadhi maji.

Waziri mkuu amesema ujenzi utaanza Kidete ambako tayari fedha zipo na kisha utatumika utaratibu kupata fedha za kukamilisha mabwawa mengine saba na kupatikana suluhu ya kudumu.

“Wapo ambao wanafurahia watu wakipata matatizo na kusherehekea na kukejeli. Nataka niwaambie, Serikali haijalala. Kwa sasa yanafanyika masuala ya kitaalamu na kumpata mkandarasi wa kuanza kujenga,” amesema.

Amewahakikishia wananchi kuwa Serikali imeshachukua hatua za kupata suluhu ya kudumu, akieleza zimeshatolewa Sh23 milioni kwa ajili ya kuongezea fedha za kuwahamisha na kuwapatia waathirika misaada ya kibinadamu.

Ameeleza ziliombwa Sh63 milioni kwa ajili ya kuchukuliwa kwa hatua hizo, utaratibu unafanyika kukamilisha upatikanaji wa fedha zote.

Dk Mwigulu ameonya tabia ya baadhi ya Watanzania kuonyesha furaha inapotokea mwenzao amepatwa na tatizo.

Sambamba na hayo, ametaka wananchi watakaopewa viwanja katika maeneo yasiyokumbwa na athari za mafuriko wasiviuze na kurudi kule kwenye hatari.

“Imekuwa kawaida, mtu akipewa kiwanja, kule kukikauka anasahau anauza alichopewa anarudi kukaa kwenye maeneo hatari,” amesema.

Vilevile, ametaka Serikali hasa za mitaa kuweka wazi kwa wananchi kuhusu maeneo hatarishi kwa ujenzi, badala ya kumwacha mtu anajenga na anaweka umeme ndipo aondolewe.

Katika hatua nyingine. Baadhi ya abiria wameeleza ugumu wa kupata tiketi za SGR wanapozihitaji ndani ya saa 24, malalamiko ambayo TRC limekiri kuwapo kwa changamoto hiyo, likipanga kuimaliza kwa kuongeza ruti kuanzia wiki ya tatu ya mwezi huu.

“Usafiri wa SGR haikupaswa kuwa hivi kwa ruti ya Morogoro hata Dodoma ilipaswa muda wote ukihitaji usafiri unaupata, hivi safari ya Morogoro kilomita hata 300 hazifiki unakata tiketi siku mbili kabla?” amehoji abiria Gervas Mathayo.

Abiria mwingine, Neema Uledi, amesema uhaba wa tiketi za SGR umekuwa ukijitokeza zaidi nyakati za sikukuu na mwishoni mwa wiki.

“Unaweza kukata tiketi kupitia mfumo wa mtandao siku mbili kabla ya safari na usiipate, wengi tulitegemea SGR ni suluhisho, lakini ni kama mahitaji yamekuwa makubwa kuliko huduma,” amesema.

Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Masanja akizungumza na Mwananchi Januari Mosi, 2026 kuhusu malalamiko hayo amekiri kuwapo mahitaji makubwa ya usafiri kulinganisha na idadi ya ruti za treni hiyo.

“Ni kweli mahitaji ni makubwa, hata hivyo TRC tumeanza kulifanyia kazi, tuko katika hatua za mwisho mwisho za kiufundi ili kuongeza ruti kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma na kutoka Dodoma kwenda Dar es Salaam,” amesema.

Amesema wiki ya tatu ya Januari mchakato huo utakuwa umekamilika na kuanzia wiki ya nne wataongeza ruti.

Amesema Shirika lina treni za kutosha katika kipande cha Dodoma, hivyo wanapokwenda kuongeza ruti, badala ya treni moja kufika na kisha kupakia abiria na kugeuka, zitakuwa zinapishana hivyo kusafirisha idadi kubwa ya abiria kwa siku.