Mbeya. Wakati watu wanne wakiripotiwa kufariki dunia kwa kusombwa na maji jijini Mbeya, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoani humo limewaomba wananchi kuendelea kuchukua tahadhari juu ya mvua zinazoendelea kunyesha na kuweka ulinzi kwa watoto, wazee na wenye ulemavu.
Pia, limewaomba kuendelea kutoa taarifa za majanga popote kwa Jeshi hilo ili kuweza kuokoa maisha ya wananchi, huku likisisitiza kuwa Zimamoto imejipanga kwa kipindi chote kutoa huduma wakati wowote.
Jana Januari 2 mwaka huu, Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA) ilitangaza uwapo wa mvua kubwa kwa siku 10 zitakazoambatana na ngurumo za radi, na Mbeya ikiwa miongoni mwa mikoa hiyo.
Akizungumza na Mwananchi leo Januari 3, Mrakibu Mwanadamizi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoani humo, Malumbo Ngata amesema hadi sasa watu wanne wamepoteza maisha kwa kusombwa maji kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha.
Ngata, amesema matukio ya kusombwa na maji yalianza Desemba 25 mwaka jana, huku wanaume watatu wakipoteza maisha, akiwemo mmoja aliyesombwa jana Januari 2 na bado hajapatikana.
Amesema Jeshi la Zimamoto linaendelea na juhudi za kumtafuta mtu huyo katika mito mbalimbali akiwemo mwanamke mmoja wa Mtaa wa Makunguru.
“Tunaendelea kumtafuta huyu aliyesombwa na maji jana, tangu Desemba 25 ni wanne waliosombwa kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha, kuna aliyekutwa pale Mkulu inapojengwa barabara baada ya kudumbukia, mwingine alikuwa mwendesha pikipiki,” amesema Ngata.
Kamanda huyo ameongeza kuwa kutokana na hali hiyo, wananchi wanapaswa kuchukua tahadhari wakati wote, na kufuatilia taarifa za mamlaka ya hali ya hewa juu ya utabiri wa mvua.
Amesema tahadhari hizo ziendane sambamba na ulinzi kwa watoto, wazee na wenye ulemavu kuhakikisha wanakuwa salama na kutoa taarifa kwa Jeshi hilo pale inapotokea tatizo kwani Zimamoto iko tayari kutoa huduma wakati wote.
“Tunavyo vifaa vya kisasa kutuwezesha kufika popote, wananchi watoe taarifa inapotokea majanga, lakini kwa kipindi hiki cha mvua wachukue tahadhari na kuwalinda watoto, wazee na wenye ulemavu,” amesema Kamanda huyo.
Benson Msuya mkazi wa Sokomatola amesema tukio la mwanamke kusombwa na maji, ambaye awali alidhani ni mtoto limewashtua wengi, akiomba wazazi na walezi kuzingatia usalama wao na familia kwa ujumla ili kuondokana na matukio hayo.
Naye Judith Methew amelipongeza Jeshi la Zimamoto kwa kuwahi kwenye matukio, akiomba wananchi kuendelea kutoa ushirikiano ili kulinda usalama pale inapotokea majanga yoyote.
