RAUNDI ya 13 ya Ligi ya Championship inaendelea tena wikiendi hii kwa mechi kali na za kuvutia, ambapo macho na masikio ya wapenzi wa soka nchini yataelekezwa katika mechi ya kesho Jumapili kati ya wenyeji, KenGold na Kagera Sugar.
Mechi hiyo inasubiriwa kwa hamu kutokana na timu zote mbili kushuka daraja msimu wa 2024-2025, zikitokea Ligi Kuu Bara hadi Championship, baada ya mwenendo mbaya uliochangia pia kwa kiasi kikubwa kumaliza kwenye nafasi ya 15 na 16 katika msimamo.
KenGold iliyotwaa ubingwa wa Championship msimu wa 2023-2024, msimu wa 2024-2025, ulikuwa mchungu kwa timu hiyo, baada ya kuburuza mkiani kwa pointi 16, kufuatia kushinda mechi tatu, sare saba na kupoteza 20, kati ya 30 ilizocheza.
Timu hiyo iko nafasi ya nane kwa pointi 17, baada ya kikosi hicho cha jijini Mbeya kucheza mechi 12 pia, ambapo kati yake imeshinda nne, sare tano na kupoteza tatu, huku ikifunga mabao 13 na kuruhusu 12.
Kwa upande wa Kagera iliyodumu katika Ligi Kuu kwa miaka 20 tangu iliposhiriki 2005, ilishuka daraja msimu wa 2024-2025, baada ya kushinda mechi tano tu, ikitoka sare nane na kupoteza 17, ikiwa nafasi ya 15, kufuatia kukusanya pointi 23.
Timu hiyo inayonolewa na aliyekuwa nyota wa Simba, Yanga na timu ya Taifa Stars, Juma Kaseja aliyeitumikia pia Kagera akiwa mchezaji na kocha wa makipa, iko nafasi ya pili kwa pointi 30, sawa na vinara Geita Gold ila zinatofautiana mabao.
Kagera iliyo nafasi ya pili kwa pointi 30, ambazo ni sawa na za vinara Geita Gold zikitofautiana kwa mabao ya kufunga na kufungwa, katika mechi 12 ilizozicheza imeshinda tisa na kutoka sare tatu, ikifunga mabao 23 na kuruhusu sita.
Mechi hiyo itakayopigwa Kwenye Uwanja wa Halmashauri ya Chunya, inazikutanisha timu hizo zikiwa na kumbukumbu ya kutoka sare wiki iliyopita, ambapo KenGold ilifungana 2-2 na Geita Gold, huku Kagera Sugar ikifungana pia 2-2 na Songea United.
Mara ya mwisho kwa timu hizo kukutana ilikuwa katika Ligi Kuu Bara, ambapo KenGold ilishinda bao 1-0, kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, Februari 18, 2025, lililofungwa na nyota, Mishamo Michael, aliyepo kwa sasa Singida Black Stars.
Mechi hiyo ilikuwa ni ya kisasi kwa KenGold baada ya raundi ya kwanza kuchapwa ugenini kwenye Uwanja wa Kaitaba mabao 2-0, Septemba 20, 2024, yaliyofungwa yote na kiungo mshambuliaji, Mganda Peter Lwasa, anayeichezea Pamba Jiji msimu huu.
Kocha wa KenGold, Jumanne Challe, amesema mechi na Kagera Sugar itakuwa ni ngumu kutokana na ubora wa nyota walio katika kikosi hicho, japo amejipanga vizuri kukabiliana nao, kama alivyofanya wiki iliyopita ugenini alipocheza na Geita Gold.
“Moja ya changamoto kubwa kwetu ni kukosa tu balansi kwa sababu timu inafunga ila inaruhusu pia mabao kwa wingi, hii sio dalili nzuri, ila jambo tunalozingatia kwa sasa ni kupata pointi tatu licha ya ushindani mkubwa uliopo,” amesema Challe.
Mechi nyingine za Jumapili, zitaikutanisha B19 (zamani Tanesco) iliyochapwa mabao 3-2 na Transit Camp, ikiwa kwenye Uwanja wa Kituo cha TFF Kigamboni kucheza na Barberian, ambayo hadi sasa ndio timu pekee kati ya 16 haijaonja ladha ya ushindi.
Barberian zamani Kiluvya United, katika mechi 12 ilizocheza hadi sasa kikosi hicho hakijashinda mechi yoyote, baada ya kutoka sare tatu na kupoteza tisa, huku ikifunga mabao sita na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 23.
Kwenye Uwanja wa CCM Kambarage Shinyanga, Stand United ‘Chama la Wana’, iliyofungwa mabao 2-1 na Bigman, itakuwa na kibarua kigumu cha kupambana na timu ya Mbeya Kwanza, kwani hadi sasa kikosi hicho kimeshinda mechi tisa mfululizo.
Mbeya Kwanza tangu ilipopoteza mechi tatu za mwanzoni mwa msimu huu, hadi sasa imeshinda tisa mfululizo ikiwa ni kiwango kizuri, kwani kikosi hicho kinachonolewa na kocha Maka Mwalwisi kinashika nafasi ya tatu katika msimamo na pointi 27.
Timu hiyo iliyouzwa kwa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora ikitokea Mkoa wa Lindi ilipoweka kambi kwa msimu wa 2024-2025, ilishuka daraja msimu wa 2021-2022, baada ya kikosi hicho kumaliza kikiwa mkiani mwa Ligi Kuu Bara kwa pointi 25.
Msimu huo, Mbeya Kwanza ilishinda mechi tano tu, sare 10 na kupoteza 15, ikifunga mabao 22 na kuruhusu 39, ikiungana na Biashara United iliyomaliza katika nafasi ya 15 kwa pointi 28, hivyo ina kazi kubwa ya kupambana ili kurejea tena Ligi Kuu Bara.
Mechi nyingine tatu zitapigwa leo Jumamosi, ambapo Songea United iliyotoka sare ya kufungana mabao 2-2 na Kagera Sugar, itakuwa kwenye Uwanja wa Majimaji kucheza na Geita Gold, iliyolazimishwa pia sare ya 2-2 na kikosi cha KenGold ya Mbeya. Transit Camp iliyoifunga B19 mabao 3-2, itakuwa kwenye Kituo cha TFF Kigamboni kucheza na Hausung iliyoifunga Barberian 2-1, huku African Sports iliyochapwa na Mbuni 2-0, itacheza na TMA ya Arusha iliyofungwa na maafande wa Polisi Tanzania 2-1.
