Yanga yamganda winga Mkongomani, yatajiwa bei

MABOSI wa Yanga wameendelea kumganda winga mmoja matata kutoka DR Congo kwa kutaka ashuke mapema ili awahi michuano ya Kombe la Mapinduzi 2026 inayoendelea Zanzibar.

Uongozi unafanya hivyo kwa lengo la kutekeleza mapendekezo ya kocha Pedro Goncalves anayetaka kuletewa mashine za maana kabla ya kurejea katika mechi za Ligi Kuu Bara na Ligi ya Mabingwa Afrika zilizosimama kupisha fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2025 zinazoendelea Morocco.

Mezani kwa mabosi wa Yanga kuna majina mawili ya Ibrahim Matobo kutoka Les Aigles Du Congo na Wilfrid Nkya wa FC Lupopo, ambapo kila mmoja akiwa na sifa ya kutengeneza nafasi na kufunga huku mmoja kati yao hajatumika kabisa katika michuno ya CAF msimu huu, na Yanga inataka kuona mmoja wao anatua mapema klabuni.

Inadaiwa Yanga imeamua kunyooka zaidi kwa Matobo bila masihara kwani ina uhakika atakuwa msaada mkubwa akiwa pia hajatumika katika mechi za CAF msimu huu tofauti na Nkya, japo kwa sasa sheria za usajili wa dirisha dogo zimelegeza kanuni ya mchezaji kwa kuruhusiwa kutumiwa na timu mbili ndani ya msimu mmoja.

Taarifa kutoka ndani ya Yanga zimeliambia Mwanaspoti, hata hivyo klabu hiyo italazimika kuvunja benki kwa kiwango cha fedha ambazo mchezaji huyo ataitoboa na hata klabu yake imegundua hilo na kutaka mzigo wa maana kwa kutambua Jangwani wameshaona umuhimu wa winga huyo ndani ya kikosi chao.

“Wamewawekea Yanga dau kubwa la kumpata Matobo. Kwanza kuna pesa ya kumpa mchezaji na klabu pia, jambo ambalo litawalazimisha kutoa pesa nyingi ili kupata saini yake kwa sababu bado ana mkataba wa miaka miwili,” kilisema chanzo.

“Kwa hiyo klabu inamuuza kwa Dola 150,000 na mchezaji ametaka 100,000 hivyo Yanga itawalizimu kutoa 250,000.”

Mpango uliopo sasa ni kumuondoa Moussa Balla Conte ambaye kiwango chake hakijamridhisha kocha Pedro na viongozi. Licha ya kusaini mkataba wa miaka miwili, lakini wanajipanga kumtoa kwa mkopo.

Tangu Conte atue Yanga amefanikiwa kuanza kwenye mchezo mmoja wa mashindano ambapo ilicheza nyumbani dhidi ya Pamba Jiji ikishinda kwa mabao 3-0 wakati huo ikifundishwa na kocha Romain Folz.

Hivi karibuni Mwanaspoti lilieleza mipango ya kuwatoa kwa mkopo Doumbia na Conte kwenda Singida Black Stars kwamba huenda ikagonga mwamba, kwani wamegoma na kuitaka Yanga ivunje mikataba yao, na tayari Mohammed Damaro ametua Jangwani akitokea Singida, huku Marouf Tchakei aliyekuwa katika dili hilo akidaiwa naye kugoma kuondoka Singida.

Tayari Yanga ipo katika hatua za mwisho za kumrejesha straika Andy Boyeli katika timu ya Sekhukhune United ya Afrika Kusini ili kuruhusu beki wa kulia aliyekuwa majeruhi, Yao Kouassi, aliyepo na kikosi Zanzibar kwa sasa kuingizwa ndani ya mfumo.