ZRA yavuka lengo la makusanyo Desemba, sababu zatajwa

Unguja. Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA) imefanikiwa kuvuka lengo la makusanyo ya mapato kwa Desemba 2025 baada ya kukusanya Sh90.873 bilioni kati ya Sh90.524 bilioni iliyokadiriwa, sawa na ufanisi wa asilimia 100.39.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari Januari 2, 2026 na Mkuu wa Kitengo cha Habari, Uhusiano na Huduma kwa Wateja wa ZRA, Makame Khamis Moh’d, makusanyo hayo yanaonesha ongezeko kubwa ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka uliopita.

Taarifa hiyo imesema kuwa makusanyo halisi ya Desemba katika mwaka wa fedha 2024/2025 yalikuwa Sh75.583 bilioni, hali inayoonesha ukuaji wa makusanyo kwa asilimia 20.23 ikilinganishwa na Desemba ya mwaka wa fedha 2025/2026.

Kwa upande wa robo ya pili ya mwaka wa fedha 2025/2026 (Oktoba hadi Desemba 2025), ZRA ilikadiriwa kukusanya Sh286.813 bilioni, lakini ilifanikiwa kukusanya Sh273.772 bilioni, sawa na ufanisi wa asilimia 95.45.

Ikilinganishwa na makusanyo ya robo ya pili ya mwaka wa fedha 2024/2025 ya Sh228.098 bilioni, makusanyo ya mwaka huu yanaonesha ongezeko la Sh45.67 bilioni, sawa na ukuaji wa asilimia 20.02.

Akieleza sababu za kuvuka lengo la makusanyo ya Desemba, Makame amesema ni pamoja na kuimarika na kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi kati ya Zanzibar na Tanzania Bara, hali inayotokana na sera thabiti na uongozi imara ulioimarisha mazingira ya biashara kwa pande zote za Muungano.

Ameongeza kuwa uwekezaji mkubwa katika ujenzi wa miundombinu na huduma za kijamii, pamoja na kuimarika kwa shughuli za kiuchumi Zanzibar kunakotokana na utekelezaji wa sera bora za kiuchumi za Serikali ya Awamu ya Nane, kumechangia ongezeko la mapato.

Sababu nyingine ni kuongezeka kwa uelewa wa walipakodi kutokana na kuimarika kwa utoaji wa elimu ya kodi, pamoja na kuongezeka kwa ulipaji wa kodi kwa hiari baada ya walipakodi kushuhudia matumizi chanya ya kodi wanazolipa.

Pia, taarifa hiyo imetaja mchango wa msamaha wa adhabu na riba kwa walipakodi wenye madeni ya muda mrefu (Tax Amnesty) uliotolewa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Itakumbukwa kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilitoa msamaha wa adhabu na riba kwa asilimia 100 kwa walipakodi wenye madeni ya muda mrefu kuanzia Julai hadi Novemba 2025, hatua iliyolenga kutoa fursa ya kuanza upya na kuondoa hofu ya kuendesha biashara.

Hata hivyo, kiwango cha mapato kilichopatikana kutokana na msamaha huo bado hakijatolewa rasmi.

Aidha, kuimarika kwa ushirikiano kati ya ZRA na taasisi nyingine za Serikali, ikiwemo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), pamoja na kuongezeka kwa ushirikiano kati ya ZRA na wafanyabiashara, kumetajwa kuchangia kuongezeka kwa ulipaji wa kodi kwa hiari.

Akizungumzia mikakati ya robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2025/2026 (Januari hadi Machi 2026), ZRA imesema itaendelea kuhakikisha mifumo ya kibiashara ya walipakodi inaunganishwa na Mfumo wa Kutolea Risiti za Kielektroniki (VFMS).

Pia, itaendelea kutoa huduma za kodi moja kwa moja katika maeneo ya biashara kwa kuweka kambi maalumu ili kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa walipakodi.

ZRA imesema itaendelea kuhamasisha ulipaji wa kodi kwa hiari na kuchukua hatua za kisheria dhidi ya walipakodi watakaokiuka sheria.

Kwa upande wa wananchi, maoni yamekuwa tofauti kuhusu ongezeko la makusanyo ya kodi.

Mfanyabiashara wa Darajani, Khamis Ali Ali, amesema ushirikiano mzuri kati ya Serikali na wafanyabiashara umechangia wengi kuacha kukwepa kodi.

“Mazingira yamebadilika na sasa kuna ukaribu mkubwa kati ya wafanyabiashara na mamlaka za kodi,” amesema.

Hata hivyo, baadhi ya wananchi wamesema bado kuna changamoto ya ukwepaji wa kodi.

Mkazi wa Mombasa, Jabir Mussa, amesema bado wafanyabiashara wengi hawatoi risiti za kielektroniki, hali inayopunguza makusanyo yanayoweza kupatikana.

“Mapato yameongezeka, lakini bado kuna wafanyabiashara hawatoi risiti au wanatoa risiti zenye viwango tofauti na bidhaa zilizonunuliwa,” amesema.