MBEYA City inajipima na mechi za kirafiki kujiandaa na Ligi Kuu Bara, huku ikiwa tayari imeshacheza dhidi ya Ken Gold iliyowafunga mabao 2-1 na kushinda dhidi ya Kombaini ya Mbeya kwa bao 1-0.
Kipa wa Mbeya City, Beno Kakolanya amesema mechi hizo zimewasaidia kuwaweka fiti na kocha kujua pa kufanya marekebisho.
“Ni kipimo kizuri kwetu kujiweka sawa kabla ya kuanza kwa ratiba za Ligi Kuu, ambapo tutakuwa ugenini kucheza na Mtibwa Sugar, Januari 21. Ni lazima tujipange kukabiliana na ushindani wa wapinzani wetu,” amesema Kakolanya.
“Ukiangalia katika msimamo wa ligi Mtibwa (Sugar) ipo nafasi ya saba kwa pointi 10, sisi tupo nafasi ya 13 na pointi nane, hivyo lazima kujiandaa kuhakikisha tunakwenda kupata pointi tatu ili kuanza kujiondoa katika nafasi mbaya.”
Kakolanya amesema msimu huu unahitaji mbinu bora na za kisasa ili kupata matokeo ya ushindi kutokana na ugumu wa ligi ambao hakuna timu yenye uhakika wa kupata matokeo mechi za nyumbani au ugenini.
“Ukiangalia mechi tulizoshinda ni ugenini, sisi pia tumefungwa nyumbani. Ndiyo maana nasema ligi ni ngumu haina mechi za nyumbani wala ugenini,” alisisitiza.
Mechi waliyocheza na matokeo yake ni dhidi ya Simba 3-0 City, Mbeya City 0-1 Namungo, Coastal Union 2-0 Mbeya City, Mashujaa 1-0 Mbeya City, Mbeya City 2-2 JKT Tanzania, Mbeya City 1-2 Tanzania Prisons, KMC 0-3 Mbeya City, Mbeya City 0-0 Yanga, Azam 2-0 Mbeya City na Fountain Gate 0-1 Mbeya City.
