Denis Nkane, TRA United mambo yamejipa

UONGOZI wa TRA United umekamilisha mpango wa kuinasa saini ya winga Denis Nkane kutoka Yanga kwa mkataba wa miezi sita.

TRA United imeshinda vita iliyohusisha pia JKT Tanzania iliyokuwa ikimtaka winga huyo wa zamani wa Biashara United kwa kumsainisha mkataba huo wa mkopo wa miezi sita ulio na kipengele cha kupata nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza.

Taarifa za ndani zililiambia Mwanaspoti, mabosi wa TRA wamefanikisha dili hilo baada ya makubaliano ya pande zote mbili uongozi wa Yanga na mchezaji mwenyewe kuridhia kuitumikia timu hiyo.

“Ni kweli kulikuwa na ofa kutoka timu mbalimbali zinazocheza Ligi Kuu, lakini makubaliano yamefikiwa Nkane kwenda kuitumikia TRA baada ya kufuata taratibu na kufikia makubaliano na mchezaji mwenyewe ambaye alipewa nafasi ya kuchagua ni wapi anataka kwenda,” kilisema chanzo hicho na kuongeza;

“Mkataba ni wa miezi sita hadi mwisho wa msimu mambo yakienda vizuri kunaweza kukawa na makubaliano mengine, lakini katika mkataba huu wa awali ni kwamba mchezaji anatakiwa kupata nafasi ya kucheza ili kuendeleza kipaji chake, kwani sababu ya kumtoa ni kutokana na kukosa nafasi hapa Yanga.”

Mtoa taarifa huyo amesema Nkane ataungana na TRA Zanzibar ambako timu hiyo ilitangulia kufika kutokana na kuwa katika ushiriki wa michuano ya Kombe la Mapinduzi 2026.Timu hiyo sambamba na Yanza zimepangwa kundi moja pamoja na KVZ na zitaumana katika mechi ya kufungia makundi kesho Jumanne.

Nkane alisajiliwa na Yanga misimu mitano iliyopita  akitokea Biashara United, lakini hajawahi kuingia kikosi cha kwanza zaidi ya kupata dakika chache za kucheza katika baadhi ya mechi.