Dodoma. “Miezi minane usiku na mchana niliishi na minyororo miguuni, leo naona mwanga. Ahsanteni Kampuni ya Mwananchi na vyombo vingine mlivyokuwa wa kwanza kupaza sauti,” anasema Juma Maganga kwa sauti ya kutetemeka huku akifuta machozi.
Ni simulizi ya huzuni, matumaini na ushindi baada ya mateso ya dereva Juma, raia wa Tanzania ambaye amerejea nyumbani baada ya kukaa siku 357 nje ya familia yake akiwa gerezani nchini Sudan Kusini.
Katika kipindi chote hicho hakumuona mkewe, watoto wala wazazi wake na hakuwa na uhakika kama angeona tena mwanga wa jua.
Maganga alikamatwa na kufungwa kwa kosa la usalama barabarani baada ya kugonga pikipiki iliyokuwa ikiendeshwa na mwanajeshi wa nchi hiyo, tukio lililosababisha kifo cha mwanajeshi huyo.
Mazungumzo na Maganga yamechukua muda mrefu kutokana na hali yake ya kihisia; mara kwa mara alilazimika kufuta machozi.
Aidha, ndugu, jamaa na majirani waliendelea kumzingira, wakimkumbatia na kumfariji baada ya kurejea salama.
Katika simulizi yake, Maganga anavitaja vyombo vya habari ikiwamo Kampuni ya Mwananchi kuwa miongoni mwa vilivyokuwa vya kwanza kupaza sauti kuhusu masaibu yake, ingawa anakiri hakufahamu hilo akiwa gerezani, bali alisimuliwa na mkewe baada ya kurejea nyumbani.
“Maisha kule yalikuwa magumu sana. Kwanza sikujua Kiarabu na sikuwa na mtu wa kunisaidia. Bahati nzuri nilikutana na mmoja wa askari aliyesoma Kenya, yeye alikuwa anaelewa kidogo,” anasema.
Maganga anasema alianza safari yake Jumatatu ya Januari 13, 2025 akitokea Dodoma akipeleka mzigo Sudan Kusini.
Aliingia Sudan Kusini Januari 31, 2025 baada ya kukwama njiani kwa muda mrefu akisubiri ukamilishwaji wa vibali.
Hakujua kuwa safari hiyo ingegeuka shubiri katika maisha yake, anasema kama angejua, huenda asingesafiri, lakini wahenga hawakukosea waliposema, “ulisilolijua ni sawa na usiku wa giza.”
Mbali na kuchelewa kuingia nchini humo, alikaa kwa takribani wiki mbili akisubiri taratibu nyingine ikiwamo kulipia mizani, jambo analosema ni la kawaida kwa madereva wa masafa marefu wanaoingia Sudan Kusini.
Hata hivyo, Maganga anasema Februari 14, 2025, akiwa amebakiza kilomita chache kukamilisha safari yake alipofika Kijiji cha Pakeli, nchini Sudan Kusini aligongana na mwanajeshi aliyekuwa akiendesha pikipiki.
Ajali hiyo ilisababisha kifo cha mwanajeshi huyo papo hapo.
Anakiri alipigwa sana na raia waliokuwa eneo la tukio kiasi cha mwili wake kufa ganzi, huku wakidhani naye amefariki dunia.
Anasema alipata majeraha makubwa sehemu mbalimbali za mwili wake, ikiwamo kichwani.
Akionesha makovu kichwani anasema, “sijui walinipiga na vitu gani, lakini polisi walitumia nguvu kubwa kuniokoa na kunirudisha kituo cha polisi.”
Maganga anasema siku iliyofuata alianza kupata fahamu kisha polisi wakampeleka hospitali kwa matibabu na alipata nafuu kidogo, ndipo akawasiliana na mkewe.
Anasema baada ya mawasiliano hayo,mkewe alianza kusambaza taarifa za kukamatwa kwake, hali iliyowezesha wadau mbalimbali kuanza kufuatilia suala hilo, wakiwamo Watanzania wanaoishi Sudan, Serikali ya Tanzania na Umoja wa Madereva wa Masafa Marefu.
Maganga anakumbuka kutembelewa na mchungaji Mtanzania anayeishi Sudan, aliyempa faraja na akamkabidhi kwa binti yake awe anamsaidia chakula na masuala ya matibabu.
“Maisha kule bila pesa ni magumu sana, hata ukiwa mfungwa pesa ni lazima. Watanzania wenzangu walinibeba sana,” anasema huku akiinua mikono na kufuta machozi.
Dereva huyo anasema baada ya kuangaika kwa muda mrefu, Desemba 29, 2025, alipokea simu kutoka kwa mbunge wa Mtumba, Anthony Mavunde akimtaka ajiandae kurejea nyumbani.
Anasema Mavunde alimwambia Sh8 milioni pamoja na nauli ya kurejea Tanzania, zilikuwa zimepatikana.
Juma Maganga (kushoto) akisalimiana na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde mara baada ya kuwasili stendi ya mabasi ya Mkoa wa Dodoma.
Dereva huyo anasema awali alikuwa akidaiwa Sh51 milioni za Kitanzania.
Desemba 31, 2025, aliitwa ndani ya gereza na kukutana na meya wa mji huo, aliyemweleza kuwa Serikali ya Sudan Kusini kwa kushirikiana na ubalozi wa Tanzania, ilikuwa imeandaa ulinzi wa kumsindikiza hadi mpakani kwa usalama.
Maganga amesharejea nyumbani na tayari amekutana na mkewe, watoto, wazazi, ndugu na majirani, wengi wao wakimwaga machozi ya furaha.
“Maisha yangu sasa siyo kuangalia nyuma, bali kuanzia hapa na kusonga mbele kwa ujasiri,” ameiambia Mwananchi aliyofanya naye mahojiano jana Jumamosi, Januari 3, 2026 baada ya kupokelewa.
Mke wake, Rehema Mongi anasema mwaka mmoja alioupitia ulikuwa wa mateso hali iliyomlazimisha kuuza mali mbalimbali kwa lengo la kumsaidia mumewe kutoka gerezani.
Anasema yeye na watoto walipitia maisha magumu ikiwa ni pamoja na kulala njaa mara kadhaa, hali iliyowafanya muda mwingine waombe misaada katika misikiti na makanisa.
“Tulipata mchungaji kule aliyekuwa anawasiliana na familia ya yule mwanajeshi. Kwa sheria zao, marehemu alikuwa na wake watatu na watoto saba, ilibidi tulipe ng’ombe 51, sawa na takribani Sh110 milioni za Tanzania,” anasema Rehema.
Anasema kiwango hicho cha fedha kiligawanya kati yake na mmiliki wa gari. “Kila mtu alitakiwa kulipa nusu ya hela hiyo Sh110 milioni,” anafafanua mkewe.
Anasema mbali na michango hiyo, ilikuwa lazima kutuma angalau Sh200,000 kila wiki, hali iliyomlazimu kuuza samani, kiwanja na hata nguo, huku akiwashukuru viongozi na watu binafsi waliompa moyo.
Anasema hakuna siku ngumu kama Januari 3, 2026, alipokutana tena na mumewe. “Nilipomuona, sikuamini. Ni Mungu tu,” anasema.
Anakiri kuwa, mumewe bado anahitaji msaada wa kisaikolojia ili kumsaidia kupona kiakili na kuanza maisha mapya.
Baba yake mzazi, Mzee Ali Maganga anasema hakuwahi kufikiria kama angemuona mwanaye akiwa hai tena.
“Kwangu ni Mungu tu. Namshukuru Mavunde na Serikali yote. Kazi hii watalipwa na Mungu,” anasema huku akirudia maneno hayo mara kwa mara.
Akizungumza katika mapokezi nyumbani kwa Maganga, Mtaa wa Nzuguni B, Mbunge wa Mtumba ambaye pia ni Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, anasema hana mengi ya kusema zaidi ya kumshukuru Mungu.
Anasema alishirikiana kwa karibu na Wizara ya Mambo ya Nje kuhakikisha suala hilo linafuatiliwa hadi mwisho.
“Nilipitia wakati mgumu sana, hadi kukosa usingizi kutokana na kilio cha familia hii. Namshukuru Mungu jambo hili limekamilika salama,” anasema.