Korti yatupilia mbali pingamizi shauri la uchaguzi Tunduru Kusini

Arusha. Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Songea imetupilia mbali pingamizi la awali lililowasilishwa na Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Tunduru Kusini  na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), katika shauri la uchaguzi linalohusu matokeo ya ubunge.

Katika shauri hilo la uchaguzi namba  29982/2025, linalohusu matokeo ya uchaguzi wa ubunge wa Tunduru Kusini, limefunguliwa na Mohamed Rais na Odax John.

Walalamikaji hao wamefungua shauri hilo dhidi ya Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Tunduru Kusini, Fadhili Chilombe na AG.

Uamuzi huo umetolewa Desemba 29, 2025, na Jaji James Karayemaha anayesikiliza shauri hilo lililofunguliwa Novemba 26, 2025.

Shauri hilo limetokana na matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 wa Rais, wabunge na madiwani huku Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) ikimtangaza Fadhili (mlalamikiwa wa pili) kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) kuwa mshindi.

Mahakama hiyo baada ya kusikiliza na kuchambua kwa kina hoja za kisheria zilizotolewa na mawakili wa pande zote mbili, imejiridhisha kuwa walalamikaji hawakupaswa kuwasilisha maombi ya dhamana ya gharama.

Kutokana na sababu hiyo, Mahakama hiyo ilitupilia mbali pingamizi hilo lililoibuliwa na mlalamikiwa wa kwanza na wa tatu kwa sababu halina mashiko na kuamuru kila upande utabeba gharama zake.

Walalamikaji hawakuridhika na matokeo hayo na wakaamua kuyapinga mahakamani wakidai kuwa, uchaguzi haukuwa huru na wa haki na kupitia shauri hilo hilo, wanaomba Mahakama itoe nafuu nne.

Nafuu hizo ni kutamka kuwa uchaguzi wa ubunge katika Jimbo la Tunduru Kusini ni batili, uteuzi wa Fadhili kama mbunge haukuwa halali, kufanyika kwa uchaguzi wa kura ili kuthibitisha Fadhili hakuwa mgombea aliyepata kura nyingi katika jimbo hilo, hivyo hakustahili kutangazwa na nafuu nyingine Mahakama itakayoona inafaa.

Kabla ya kuanza kusikilizwa kwa hoja za msingi za shauri hilo, walalamikiwa wa kwanza na wa tatu waliwasilisha pingamizi la awali wakidai shauri hilo halina nguvu ya kisheria.

Walidai walalamikaji walishindwa kuwasilisha dhamana ya gharama au kuomba kusamehewa dhamana hiyo ndani ya siku 14 tangu kufunguliwa kwa shauri.

Walieleza kuwa, shauri hilo linakosa nguvu ya kisheria kwa sababu walalamikaji walishindwa kuwasilisha maombi hayo kinyume na kifungu cha 140 (3) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani ya mwaka 2025.

Walidai kifungu hicho kikisomwa sambamba na kanuni ya 11 (1) ya Kanuni ya Mashauri ya Uchaguzi wa Wabunge Tangazo la Serikali namba 431 la Julai 11, 2025.

Shauri hilo lilipoenda kwa ajili ya usikilizwaji wa pingamizi la awali, walalamikiwa wa kwanza na wa tatu waliwakilishwa na Wakili Edwin Webiro, mlalamikiwa wa pili akiwakilishwa na Wakili Gilbert Godfrey huku walalamikaji wakiwakilishwa na Wakili John Seka.

Wakili Webiro aliieleza Mahakama kuwa kifungu  tajwa juu, kinamtaka mlalamikaji kulipa dhamana ya gharama ya kesi mahakamani isiyopungua Sh5 milioni na iwapo hawezi kulipa, anapaswa kuwasilisha mahakamani maombi kwa ajili ya kupunguziwa au kusamehewa kabisa dhamana hiyo.

Alieleza kabla ya Mahakama kutoa amri, ilipaswa kumpa mlalamikiwa haki ya kusikilizwa akirejea kifungu cha 140(6) cha Sheria ya Uchaguzi na kuongeza kuwa shauri halipaswi kusikilizwa hadi dhamana ya gharama zitakapokuwa zimelipwa.

Webiro alieleza kuwa, mpaka siku 14 zinamalizika pingamizi linasikilizwa, huku walalamikaji wakiwa hawajalipa dhamana ya gharama au kuwasilisha maombi ya dhamana ya gharama mahakamani, jambo ambalo ni kinyume na kifungu cha 140 (2) cha Sheria ya uchaguzi.

Wakili huyo alidai kuwa, licha ya kuwepo kwa hati kutoka Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) na kanuni ya 11 (4) ya kanuni za uchaguzi inayotoa nafuu kwa wenye huduma ya kisheria kutolipa gharama, walalamikaji walipaswa kupeleka maombi ya dhamana ya gharama mahakamani kwa sababu ni sharti la mazima.

Wakili huyo alifafanua kuwa, lengo la msingi la kufanya hivyo ni kukidhi takwa la kifungu cha 140(6) kinachosema; amri yoyote ya kusamehewa kulipa dhamana isitolewe bila walalamikiwa kusikilizwa na kwamba, kinaipa Mahakama na walalamikaji nafasi ya kujiridhisha na huduma hiyo na kuzuia wenye uwezo wa kulipa, lakini wanajificha nyuma ya huduma hiyo.

Wakili Gilbert Godfrey aliunga mkono hoja za Wakili Webiro kuwa takwa la kisheria halikufuatwa, hivyo Mahakama iamue kwa masilahi mapana ya haki.

Akijibu pingamizi hilo, wakili Seka aliieleza Mahakama kwamba, walalamikaji walikuwa wamepewa msaada wa kisheria na TLS na hawapaswi kulipa dhamana ya gharama akirejea mashauri mbalimbali kujenga hoja yake.

Katika hoja ya pili, wakili huyo alieleza kuhusu ukuu wa Sheria ya Msaada wa Kisheria sura ya 21 na Sheria ya Uchaguzi, inayosema; masuala yanayohusu dhamana ya gharama, sheria mama inayopaswa kutumiwa ni ya msaada wa kisheria na si Sheria ya Uchaguzi.

Wakili huyo alirejea kifungu cha 32 cha Sheria ya Msaada wa Kisheria na kanuni ya 11 (4) ya Kanuni za Uchaguzi, zinazoeleza mtu aliyepewa msaada wa kisheria hapaswi kutoa dhamana ya gharama katika shauri lolote.

Kwa mujibu wake, kifungu cha 32 cha sheria ya msaada wa kisheria, kina nguvu kuliko sheria yoyote ikiwamo ya uchaguzi na kuwa vifungu vya 140 (3), (4) na (5) havizungumzii mtu aliyopewa msaada wa kisheria.

Wakili huyo alidai walalamikaji wana wajibu wa kuwasilisha maombi ya dhamana ya gharama na kusikilizwa na Mahakama hiyo kwa sababu wanayo haki ya moja kwa moja.

Katika uamuzi wake, Jaji Karayemaha amesema amechunguza kwa makini pingamizi la awali na mawasilisho ya pande zote mbili, Mahakama imekubaliana na hoja za walalamikaji.

Amesema Mahakama ilibaini kuwa ni kweli walalamikaji hawakulipa dhamana ya gharama wala kuwasilisha maombi ya dhamana hiyo, lakini pia ilithibitisha kuwa walalamikaji walikuwa wamepewa msaada wa kisheria halali kwa mujibu wa hati ya TLS.

“Kwenye shauri hili, sheria imesema kuwa mtu aliyepewa msaada wa kisheria hatotakiwa kutoa dhamana ya gharama ya shauri. Msimamo wangu unatokana na ukweli kuwa walalamikaji wanaopewa msaada wa kisheria hawaguswi kabisa na kifungu cha 140(3) na (5) cha Sheria ya Uchaguzi,” amesema Jaji Karayemaha.

Amesema  kuhusu hoja ya wakili Webiro iliyoungwa mkono na wakili Gilbert, ni kwamba kifungu cha 32 na kanuni 11 (4) havijawaondolea walalamikaji takwa lililopo kifungu cha 140 (3) cha sheria ya uchaguzi.

“Binafsi natofautiana nao kwa sababu kifungu cha 32 cha sheria ya msaada wa kisheria na kanuni ya 11 (4) ya kanuni za mashauri ya uchaguzi havipo.

“Mahakama  hii haina mamlaka kisheria kuamua kama walalamikaji kwenye shauri hili wana sifa za kupewa msaada wa kisheria au la. Ninachokiona ni kasoro ya kisheria ya sheria ya msaada wa kisheria na kanuni zake,”amesema Jaji Karayemaha.

“Hizi hazisemi kuwa maombi yanapowasilishwa na TLS ili yachunguzwe na kuhakikiwa kujiridhisha kama muombaji anakidhi vigezo. Kwa muktadha huo nakubaliana na wakili Seka kuwa walalamikaji hawana jukumu kisheria kuleta maombi ya dhamana ya gharama kwa sababu wanayo haki kisheri kwa kuleta shauri la uchaguzi mahakamani,” amesema.

Amehitimisha kuwa, baada ya kujiridhisha walalamikaji hawakupaswa kuwasilisha maombi ya dhamana ya gharama, anaona pingamizi lililoibuliwa na walalamikiwa wa kwanza na wa tatu halina mashiko, hivyo kutupilia mbali na kila upande utabeba gharama zake.