Kukamatwa kwa Maduro ni kama walivyokanatwa Noriega, Saddam

Dar es Salaam. Taarifa za kukamatwa kwa kiongozi wa Venezuela, Nicolás Maduro, na kuwekwa chini ya ulinzi wa Marekani zimefufua kumbukumbu za matukio mengine ya kukamatwa viongozi wa Panama, Iraqi na Honduras.

Viongozi walioangushwa madarakani na kutiwa mbaroni ni Manuel Noriega wa Panama na Saddam Hussein wa Iraq, ingawa mazingira ya kisiasa na kijiografia yanatofautiana. Mfanano wa kisheria na kijeshi kati ya visa hivi viwili umeibua mjadala mpana kuhusu mamlaka ya Marekani, sheria za kimataifa na mustakabali wa viongozi wanaokamatwa nje ya mipaka yao.

Kwa mujibu wa maelezo ya waendesha mashtaka wa Marekani, Nicolás Maduro wa Venezuela anakabiliwa na tuhuma za kuhusika na biashara ya dawa za kulevya na kuendesha kile kinachoelezwa kuwa “magenge yanayodhaminiwa na dola.”

Ikiwa kesi itaendelea kama ilivyokuwa kwa Noriega, wachambuzi wa sheria wanaonya kuwa dunia inapaswa kujiandaa kwa mvutano wa muda mrefu wa kisheria, unaohusisha maswali ya haki za binadamu, mamlaka ya mahakama za Marekani na uhalali wa hatua za kijeshi nje ya nchi.

Historia inaonesha Desemba 1989, Marekani iliivamia Panama kwa madai kuwa Manuel Noriega alikuwa amegeuza nchi hiyo kuwa kitovu cha ulanguzi wa dawa za kulevya na kuhatarisha usalama wa raia wa Marekani. Baada ya wiki kadhaa za msako mkali, akiwemo Noriega kujificha katika ubalozi wa Vatican, hatimaye alijisalimisha Januari 1990 na kusafirishwa hadi Marekani kwa ajili ya kushtakiwa.

Tofauti na madai ya sasa kuhusu kukamatwa kwa haraka kwa Maduro, kukamatwa kwa Noriega kulichukua muda na kulihusisha vituko visivyo vya kawaida, ikiwemo wanajeshi wa Marekani kupiga muziki wa sauti kubwa nje ya ubalozi wa Vatican ili kumlazimisha ajisalimishe.

Alipofikishwa Marekani, Noriega alianzisha mapambano ya kisheria ya miaka mingi, akidai atambuliwe kama mfungwa wa vita (POW), si mhalifu wa kawaida.

Hatimaye, mahakama ilikubaliana naye kwa kiwango fulani, ikampa hadhi ya mfungwa wa vita, hali iliyompa haki maalumu gerezani. Hata hivyo, hoja zake za kupinga mamlaka ya mahakama za Marekani, ikiwemo kudai kinga kama mkuu wa nchi, zilikataliwa.

Mwaka 1991 alihukumiwa kifungo cha miaka 40 jela, ingawa baadaye alihamishiwa Ufaransa na kisha kurejeshwa Panama, ambako alifariki dunia mwaka 2017.

Wataalamu wa sheria wanasema endapo Maduro atafungua mapambano ya kisheria kama ya Noriega, huenda yakahusisha hoja mpya za kikatiba na kimataifa.

Hata hivyo, kuna mifano ya kisheria inayoonesha kuwa mahakama za Marekani mara nyingi hukataa kuhoji uhalali wa namna mtuhumiwa alivyoletwa mbele yao, hata kama hatua hiyo ilikiuka sheria za kimataifa.

Kwa mtazamo wa kihistoria, kesi ya Noriega imekuwa rejea muhimu kwa watawala wa Marekani wanaotetea hatua kali dhidi ya viongozi wanaodaiwa kujihusisha na uhalifu wa kimataifa.

Ikiwa madai dhidi ya Maduro yatafikishwa mahakamani, dunia itashuhudia tena mvutano kati ya nguvu za dola kubwa na misingi ya sheria za kimataifa, mjadala ambao haujaisha bali unarudia kujitokeza kwa sura mpya.

Iwapo madai hayo yatathibitishwa, Maduro ataingia kwenye orodha nyeti ya viongozi wachache waliowahi kushikwa moja kwa moja na Marekani, katika operesheni zilizobadili mwelekeo wa siasa za kimataifa.

Historia inawakumbuka kwa namna ya pekee Manuel Noriega wa Panama na Saddam Hussein wa Iraq, wote waliwahi kuwa washirika wa Washington kabla ya kugeuka maadui.

Panama 1989: Kuanguka kwa Noriega

Katikati ya Desemba 1989, chini ya urais wa George H. W. Bush, Marekani ilivamia Panama katika operesheni iliyokuwa kubwa zaidi ya kijeshi tangu Vita vya Vietnam.

Saddam Hussein – Iraq 2003: Mwisho wa Saddam

Desemba 13, 2003, miezi tisa baada ya uvamizi wa Iraq, majeshi ya Marekani yalimkamata Rais wa zamani Saddam Hussein karibu na mji wa Tikrit.

Vita hivyo vilijengwa juu ya madai ya uwepo wa silaha za maangamizi (WMD) ambazo baadaye zilithibitika kutokuwepo.

Saddam, aliyewahi kuungwa mkono na Washington wakati wa vita vya Iraq na Iran miaka ya 1980, alihukumiwa na mahakama ya Iraq kwa uhalifu dhidi ya ubinadamu na kunyongwa Desemba 30, 2006.

Tukio hilo lilibaki kuwa moja ya vielelezo vya mabadiliko makubwa ya mkakati wa sera za kigeni za Marekani.

Honduras 2022: Kesi ya Hernández

Mfano mwingine wa kisasa ni wa aliyekuwa Rais wa Honduras, Juan Orlando Hernández, aliyekamatwa Februari 2022 muda mfupi baada ya kuondoka madarakani.

Alisafirishwa hadi Marekani, kuhukumiwa kifungo cha miaka 45 kwa makosa ya rushwa na biashara ya dawa za kulevya, kabla ya kusamehewa na Rais Trump Desemba 2025, hatua iliyozua ukosoaji mkubwa na maswali ya misimamo miwili.

Imeandikwa na Noor Shija kwa msaada wa mtandao.