Madarasa ya mitihani yalivyo mzigo kwa wazazi

Dar es Salaam. Kila saa 11:30 alfajiri, Nicodemas Massawe huwa tayari barabarani. Si kwa sababu ya kazi, bali ni safari ya kuwapeleka watoto wake shuleni ili wafike kwa wakati.

Inamlazimu kufanya hivyo, kwa sababu mtoto mmoja ni mwanafunzi wa darasa la mtihani, anayelazimika kufika shuleni haraka na mapema zaidi ya wengine.

Hatua hiyo, imebadili ratiba na mtindo wa maisha ya Massawe, kama ilivyo kwa maelfu ya wazazi wengine wenye watoto wanaosoma madarasa ya mitihani.

Madarasa ya mitihani la nne na la sita, kimsingi yalipaswa kuwasaidia watoto kujiandaa vizuri kitaaluma, yamegeuka kuwa chanzo cha hekaheka kwa wazazi.

Ratiba za kawaida za familia zinavurugika, gharama zinaongezeka na mzazi na mtoto mwenyewe wanajikuta katika mzigo wa kisaikolojia, huku ushindani wa kitaaluma baina ya shule ukitajwa kuwa kiini cha changamoto hiyo.

Kwa Massawe, changamoto haipo tu kwenye ada za masomo ya ziada, bali pia katika usafiri na upangaji wa muda.

“Katika shule moja nina mtoto wa darasa la mtihani na mwingine darasa la kawaida. Wa darasa la mtihani anatoka saa tisa mchana, lakini wa kawaida anatoka saa 12:30 jioni. Inabidi nimsubiri mmoja kwa saa zaidi ya tatu ili waondoke pamoja,” anasema.

Anasema hali hiyo imemlazimu kubadilisha ratiba za kazi, kupunguza muda wa uzalishaji na wakati mwingine kutumia usafiri usio salama kwa watoto.

“Bodaboda siyo chaguo zuri kwa mtoto mdogo, lakini wakati mwingine sina namna. Nikichelewa kazini na hakuna mtu wa kumsaidia, nalazimika kumchukua kwa bodaboda. Hilo linaniumiza kama mzazi,” anasema.

Mbali na mzigo wa ratiba, wazazi wanasema madarasa ya mitihani yanaongeza gharama zisizopangwa awali. Ada za ziada, fedha za usafiri, chakula cha mchana na wakati mwingine gharama za bweni hufanya mzazi kujikuta anatumia zaidi ya alivyotarajia.

Shadya Kibakaya, mzazi mwingine mkazi wa Dar es Salaam, anasema shule nyingi za kutwa zimeweka utaratibu wa watoto kubaki shuleni hadi jioni kwa ajili ya masomo ya ziada, hali inayowalazimu wazazi kupanga upya usafiri wa watoto wao.

“Mtoto anatoka nje ya muda wa kawaida, hakuna usafiri wa shule, inabidi mzazi ahakikishe anakuwepo au alipie usafiri mwingine. Hapo kuna gharama ya ziada, lakini pia uchovu kwa mtoto,” anasema.

Kwa mtazamo wake, chanzo kikubwa cha hali hiyo ni ushindani uliokithiri baina ya shule binafsi, zinazotumia matokeo ya mitihani kama nyenzo ya kujitangaza na kuvutia wateja wapya.

“Hata Necta (Baraza la Taifa la Mitihani) walipoacha kutangaza shule zilizoshika nafasi za kwanza kitaifa walitambua ushindani huo una madhara, lakini kiuhalisia kwa wazazi mzigo bado upo. Shule zinataka matokeo mazuri kwa gharama yoyote,” anasema.

Kwa baadhi ya wazazi, suluhisho la msongamano wa ratiba limekuwa ni kuwaruhusu watoto kukaa bweni. Hata hivyo, wanasema mara nyingi uamuzi huo si hiari yao bali wa kulazimishwa kimazingira.

Stella Njau anasema baadhi ya shule huanzisha mfumo wa bweni huku zikisisitiza kuwa si lazima mtoto akae, lakini ratiba na mazingira huwalazimisha wazazi kukubali.

“Wanakuambia si lazima, lakini mtoto asiye bweni anakosa vipindi muhimu, anachoka kupita kiasi au anachelewa. Mwishowe mzazi unajikuta huna budi kumpeleka bweni,” anasema.

Njau anasema, hali hiyo imewalazimu baadhi ya wazazi kuhamisha watoto wao shule, hasa pale gharama za bweni na ada zinapozidi uwezo wao wa kifedha.

Sheria inataka watoto wasome karibu

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Serikali, Majid Burhan, anasema miongozo ya elimu nchini inaelekeza watoto kusoma shule zilizo karibu na makazi yao, ikiwezekana bila kuvuka barabara, ili kupunguza adha za usafiri, uchelewaji na uchovu.

“Lakini uhalisia unaonesha wazazi wengi wanawapeleka watoto shule za mbali, hususani za mchepuo wa Kiingereza, wakiamini ndizo zinafanya vizuri zaidi kitaaluma, bila kuzingatia athari kwa mtoto,” anasema Burhan.

Anasema hata madarasa ya mitihani yanapaswa kuzingatia masilahi mapana ya mtoto, ikiwamo afya ya mwili na akili, badala ya kuangalia matokeo pekee.

Kwa upande wake, mwalimu Joyce Samson, anasema Serikali imeweka ratiba na kalenda ya masomo, lakini ratiba maalumu zinaweza kuamuliwa na shule kwa kushirikiana na wazazi pale inapobidi.

“Hii hutokea kama shule iko nyuma kimasomo au ina malengo fulani ya kitaaluma. Lakini lazima kuwe na makubaliano ya pamoja kati ya shule na wazazi,” anasema.

Anaongeza kuwa, gharama zozote zinazotokana na ratiba hizo hulipishwa kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa na si kwa uamuzi wa upande mmoja.

Mdau wa elimu, Patrick Sebastian, anasema mabadiliko ya kijamii na maisha ya mijini yamechangia kuongezeka kwa madarasa ya mitihani.

“Wazazi wengi huondoka nyumbani mapema na kurudi usiku. Usimamizi wa watoto nyumbani unakuwa hafifu. Mtoto anakutana na televisheni, michezo ya video, PlayStation na marafiki wa mtaani,” anasema.

Anasema shule zimeona ni afadhali watoto wabaki shuleni kwa muda mrefu wakijifunza, lakini tatizo hujitokeza pale shule inapokuwa haina bweni na inalazimika kuwa na ratiba ndefu za masomo.

“Hapo mzazi anabeba gharama za ziada za usafiri na usumbufu wa kupanga ratiba,” anasema, akiwashauri wazazi kufanya utafiti wa kina kabla ya kuchagua shule.

Chama cha shule binafsi chazungumza

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Shule Binafsi na Vyuo nchini (Tamongsco), Mathew Alex, anasema shule zimepewa mwongozo wa kushirikisha wazazi kabla ya kuanzisha programu za masomo ya ziada.

“Taratibu za Serikali zinazitaka shule kuitisha mikutano ya wazazi na kupata ridhaa yao kwa maandishi kabla ya utekelezaji. Pale mzazi anapolalamika bila kushirikishwa, mamlaka huchukua hatua,” anasema.

Anashauri wazazi kushirikiana kwenye masuala ya usafiri, ikiwamo kukodi magari ya pamoja au kupanga zamu za kuwasindikiza watoto.

Kamishna wa Elimu, Dk Lyabwene Mtahabwa, anasema pale wazazi wamekaa kwenye vikao na kukubaliana ratiba, Serikali haiwezi kuingilia.

“Kama kulikuwa na makubaliano ya pande mbili, hatuwezi kuingilia. Lakini kama hakuna makubaliano, hatua huchukuliwa,” anasema.

Kwa upande wake, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, amewataka wakuu wa shule kuzingatia kalenda ya masomo na masaa ya kufundishia yaliyowekwa.

“Kalenda ipo wazi. Kama shule binafsi inasema ina walimu wa kutosha, matarajio ni kufundisha ndani ya saa zilizopangwa,” anasema Profesa Mkenda, akionya kuwa masomo yanayozidi muda uliopangwa yanaweza kuathiri ubora wa elimu.