Makusanyo TRA ni zaidi ya matarajio, wachumi wasema…

Dar es Salaam. Baada ya uchaguzi wa Oktoba 29, mwaka jana uliohusisha vurugu katika baadhi ya maeneo, shughuli za kiuchumi zilisimama au kupungua kwa takribani wiki moja.

Biashara nyingi zilifungwa, usafiri ulipungua, na wananchi walijifungia nyumbani wakihofia usalama wao. Kwa wachumi na watunga sera, matarajio yalikuwa wazi, makusanyo ya kodi yangeporomoka, na hivyo kuhatarisha utekelezaji wa bajeti ya Sh56.5 trilioni iliyoidhinishwa na Bunge Juni 2025 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na miradi ya maendeleo.

Kwa uzoefu wa nyuma, misukosuko ya kisiasa ya aina hiyo imekuwa ikisababisha kushuka kwa matumizi ya wananchi, kuchelewa kwa malipo na kudorora kwa shughuli za biashara, hali inayopunguza mapato ya Serikali. Safari hii, imekuwa tofauti.

Licha ya mtikisiko wa baada ya uchaguzi, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilivunja rekodi Desemba kwa kukusanya Sh4.13 trilioni dhidi ya lengo la Sh4.01 trilioni. Haya yalikuwa makusanyo ya juu zaidi kuwahi kushuhudiwa kwa mwezi mmoja katika historia ya nchi, yakionesha kuwa uchumi ulihimili mshtuko wa kisiasa kuliko ilivyotarajiwa.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Januari mosi, 2026, Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda, alisema mafanikio hayo yalikuwa ya kipekee hasa ikizingatiwa mazingira magumu ya kiutendaji yaliyokuwapo.

“Kipindi cha baada ya uchaguzi hakikuwa rahisi… Hata hivyo, uchumi umeonesha uimara wake, na walipa kodi waliendelea kutimiza wajibu wao,” alisema.

Kwa kipindi cha Oktoba hadi Desemba 2025, TRA ilikusanya Sh9.8 trilioni, ikizidi lengo la Sh9.66 trilioni. Kiasi hicho ni ongezeko la asilimia 12.26 ikilinganishwa na Sh8.73 trilioni zilizokusanywa katika kipindi kama hicho mwaka wa fedha uliopita.

Mwenda alisema matokeo hayo yanavutia zaidi ikizingatiwa sehemu ya robo hiyo ya mwaka ilikumbwa na hali ya sintofahamu, kupungua kwa shughuli za biashara na uhuru mdogo wa wananchi kusafiri katika baadhi ya miji.

“Kuendelea kuvuka malengo katika mazingira kama haya kunaonesha uimara wa mifumo yetu ya ukusanyaji mapato na uthabiti wa uchumi kwa ujumla,” alisema.

Alieleza kuwa mafanikio hayo yamechangiwa na shughuli kubwa za kiuchumi kabla ya uchaguzi, kuimarika kwa ulipaji kodi kwa hiari na mageuzi yaliyofanywa chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, yaliyoongeza uwezo wa taasisi za umma.

“Hata pale kulipokuwapo na vurugu, mifumo ya ukusanyaji mapato iliendelea kufanya kazi. Biashara zilijirekebisha, na walipa kodi waliendelea kutimiza wajibu wao,” aliongeza.

Kwa kipindi cha Julai hadi Desemba, makusanyo ya wastani ya kila mwezi yalifikia Sh3.13 trilioni, ikilinganishwa na Sh2.75 trilioni katika kipindi kama hicho mwaka mmoja uliopita.

Kwa wachambuzi wa uchumi, mwenendo huo unaashiria kuwa uchumi wa Tanzania umejenga uwezo mkubwa zaidi wa kustahimili mishtuko ya muda mfupi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti wa Sera za Umma (Repoa), Dk Donald Mmari, amesema matokeo ya baada ya uchaguzi yanaonesha kuwa ukusanyaji mapato hauathiriki kwa kiwango kikubwa na misukosuko ya kisiasa ya muda mfupi.

“Hapo zamani, tukio kama hili lingesababisha kushuka kwa mapato kwa kiwango kikubwa. Safari hii athari imekuwa ndogo, jambo linaloonesha kuimarika kwa uwezo wa taasisi na uthabiti wa uchumi,” amesema.

Dk Mmari amehusisha hali hiyo na mageuzi endelevu katika usimamizi wa kodi, matumizi ya teknolojia ya kidijitali na ushirikiano mzuri zaidi kati ya Serikali na sekta binafsi, mambo ambayo yamejenga imani hata wakati wa sintofahamu.

Kwa mtazamo wa kitaaluma, mhadhiri wa Taasisi ya Uhasibu Arusha (IAA), Dk Dorence Kalemile, amesema licha ya vurugu kuathiri kwa muda biashara na usafiri, msingi mpana wa uchumi uliendelea kusimama.

“Watu walikaa majumbani na biashara zilipungua, lakini mfumo haukuporomoka. Kuendelea kukua kwa makusanyo kunaonesha kuwa uchumi umejitanua na hautegemei tena miamala ya ana kwa ana pekee,” amesema.

Ameongeza kuwa matumizi ya mifumo ya kielektroniki, ikiwemo malipo ya kidijitali na mashine za kielektroniki za kodi (EFD), yamepunguza athari za matumizi ya mifumo ya kawaida.

Kwa upande wake, Dk Isack Safari wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine Tanzania (SAUT), amesema hali hiyo inaonesha kukomaa kwa mfumo wa fedha wa Taifa.

“Uimara hupimwa wakati wa msongo. Kuendelea kufanya vizuri kwa mapato licha ya vurugu kunaonesha kuwa uchumi wetu si dhaifu kama ilivyokuwa zamani,” amesema.

Ameongeza kuwa kudumisha mtiririko wa mapato katika kipindi nyeti kisiasa kunatuma ujumbe chanya kwa wawekezaji kuwa Tanzania inaweza kustahimili mishtuko bila kuathiri mwelekeo wa maendeleo.

Mchumi mwingine, Samson Rutashobya wa Chuo Kikuu cha Iringa, amesema tukio hilo linaonesha kuimarika kwa imani kati ya walipa kodi na Serikali.

“Wananchi wanapoendelea kulipa kodi hata katika mazingira magumu, inaonesha imani kwa taasisi za umma na mwelekeo wa nchi,” amesema.

Amesema maboresho katika mawasiliano kati ya TRA na walipa kodi pamoja na mifumo bora ya kushughulikia migogoro yamepunguza upinzani na kuongeza utii wa kodi.

Kwa mwaka wa fedha wa sasa, bajeti ya Sh56.5 trilioni inahitaji TRA kukusanya Sh36.06 trilioni. Endapo lengo hilo litafikiwa, uwiano wa kodi kwa Pato la Taifa (GDP) utaongezeka hadi zaidi ya asilimia 14.1 kutoka asilimia 13.7 mwaka 2024/25.

Mwenda alisema TRA ina matumaini kuwa lengo hilo linawezekana endapo uthabiti wa kiuchumi utaendelea.

“Funzo kutoka kipindi cha baada ya uchaguzi ni wazi. Hata katika shinikizo, mifumo yetu inaweza kufanya kazi. Kipaumbele sasa ni kudumisha kasi hii ili mapato yaendelee kuhimili maendeleo ya Taifa,” alisema.

Mbali na mapato ya kodi, viashiria vya jumla vya uchumi vinaonesha pia uimara licha ya athari za uchaguzi.

Kwa mujibu wa takwimu za Benki Kuu ya Tanzania (BoT), mauzo ya nje ya bidhaa na huduma yalifikia Dola bilioni 17.05 katika mwaka ulioishia Oktoba 2025, yakiongezeka kutoka Dola bilioni 15.13 mwaka 2024.

Katika tathmini ya uchumi ya Novemba 2025, BoT iliripoti kuwa mauzo ya nje ya bidhaa pekee yalifikia Dola bilioni 10.14 kutoka Dola bilioni 8.46 mwaka mmoja kabla, yakichangiwa na ongezeko la mauzo ya dhahabu, bidhaa za viwandani, tumbaku, korosho na kahawa.

Mauzo ya dhahabu yaliongezeka kwa asilimia 38.9 hadi Dola bilioni 4.6 kutokana na kupanda kwa bei katika soko la dunia. Mazao ya jadi yaliongezeka kwa asilimia 25.2 hadi Dola bilioni 1.44, yakiongozwa na tumbaku na korosho.

Sekta ya huduma pia iliendelea kufanya vizuri, huku mapato yakiongezeka hadi Dola bilioni 6.91 kutoka Dola bilioni 6.67, yakichangiwa zaidi na utalii na usafirishaji.

Kwa ujumla, ongezeko hili la mapato linaashiria kwamba hata chini ya shinikizo la kisiasa, uchumi wa Tanzania umeonesha uwezo wa kusimama imara na wakati mwingine hata kukua.