YANGA imetua Zanzibar na kiungo mpya kutoka Singida Black Stars, Marouf Tchakei, huku kiungo wa kikosi hicho Mohamed Doumbia akizua gumzo jipya.
Yanga ipo kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi ikiwa inataka kuchukua ubingwa baada ya mwanzo wa msimu huu kutwaa Ngao Jamii, lakini ikiwa inafanya vizuri kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kukusanya pointi nne kwenye michezo miwili, ikiwa pia haijapoteza mchezo hata mmoja kwenye Ligi Kuu Bara baada ya kucheza michezo sita.
Tchakei ambaye ameichezea Singida kwa misimu mitatu amefunga mabao 10, huku akifunga matano akiwa na Fountain Gate ambayo ameichezea mwaka mmoja.
Hesabu za Yanga kwenye eneo hilo la kiungo ni kwamba, Anapotua Tchakei basi Doumbia anatakiwa kutolewa kwa haraka ili kupisha usajili huo kwa kuwa Yanga tayari itakuwa na wachezaji 12 wanaotakiwa kikanuni.
Hii ni baada ya kiwango cha kiungo huyo kutowaridhisha makocha wote waliofundisha kikosi hicho kuanzia Romain Folz mpaka Pedro Goncalves ambaye yupo na kikosi hicho kwa sasa.
Hivyo, uwepo wa Tchakei Zanzibar unaonyesha kwamba, safari ya Doumbia ndani ya kikosi cha Yanga imefika mwisho na wakati wowote kuanzia sasa huenda atasepa.
Chanzo kinaeleza kuwa Doumbia hataki kabisa kukubaliana na ishu ya yeye kutolewa kwa mkopo, anachotaka kwa sasa ni kumalizana na klabu hiyo ili aweze kuondoka jumla.
Wakati hayo yakiendelea taarifa za ndani zililiambia Mwanaspoti kwamba; “Doumbia aliondoka mazoezini siku moja kabla ya safari ya kwenda Zanzibar.
“Lakini hakuishia hapo tu hata alipotafutwa na baadhi ya mabosi wa timu hiyo hakupatikani hivyo hayupo na haijajulikana sababu hasa ni zipi.”
Yanga imeshachukua mastaa wawili kutoka Singida, Mohamed Damaro pamoja na Tchakei ambaye anaweza kutumika kwenye mchezo wa leo dhidi ya KVZ kuanzia saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa Amaan.
