Meya Ahimiza Usafi Jijini Arusha

Na Pamela Mollel,Arusha

Meya wa Jiji la Arusha, Maximilian Iranghe, ametoa wito wa kuimarisha ushirikiano kati ya Halmashauri na mawakala wa ukusanyaji wa taka, hatua inayolenga kuhakikisha Jiji la Arusha linabaki safi, lenye afya na tayari kukaribisha biashara na watalii.

Akizungumza wakati wa muendelezo wa zoezi la “Ng’arisha Jiji la Arusha” lililofanyika katika Soko la Mbauda, Kata ya Sombetini, ambapo Meya Iranghe alisisitiza kuwa kila sehemu ya jiji inapaswa kudumishwa kwa usafi, huku akisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kila siku kati ya mawakala wa taka na Halmashauri.

“Jiji linapokuwa safi, kila mmoja anafaidika. Ushirikiano ni ufunguo wa mafanikio,” alisema Meya Iranghe.

Aidha, Meya alielekeza kuwa utaratibu wa kupiga faini kwa wanaokiuka sheria za usafi uendelee kutekelezwa ipasavyo, na biashara yoyote isifunguliwe kabla ya kuhakikisha eneo lao limepangwa na safi, hatua inayolenga kudumisha hali ya usafi kwa wote.

Diwani wa Viti Maalum na Mratibu wa zoezi la Ng’arisha Jiji, Aminata Toure, aliwashukuru wananchi na wafanyabiashara waliojitokeza kushiriki katika zoezi hilo.

Aliwahimiza kuwa mabalozi wa usafi katika maeneo yao, kuhakikisha mazingira yanabaki salama, safi na yenye afya kwa jamii nzima.

Zoezi la Ng’arisha Jiji la Arusha limeonyesha kuwa mabadiliko madogo ya kila siku, kama kushirikiana na mawakala wa taka, yanaweza kuleta athari kubwa katika maisha ya kila mmoja, huku likiimarisha mshikamano kati ya Halmashauri na wananchi.