Unguja. Mikoa ya Morogoro, Manyara na Zanzibar imebainisha fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo katika maeneo yao na kuwahimiza wawekezaji kuwekeza katika sekta za kilimo, ufugaji, viwanda na uchumi wa buluu.
Inaelezwa kuwa lengo ni kukuza biashara na kuchochea maendeleo ya kiuchumi ya maeneo husika na taifa kwa ujumla.
Fursa hizo zimewasilishwa katika mdahalo uliofanyika leo, Januari 4, 2026, katika viwanja vya maonesho ya Nyamanzi, ambako Maonesho ya Biashara ya Kimataifa Zanzibar (ZITF) yanaendelea.
Mdahalo huo umewakutanisha wafanyabiashara, wataalamu pamoja na taasisi za Serikali na binafsi kutoka Zanzibar na Tanzania Bara.
Akizungumza katika mdahalo huo, Katibu Tawala Msaidizi wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mkoa wa Morogoro, Beatrice Njawa, amesema mkoa huo una jumla ya hekta milioni 2.3 zinazofaa kwa kilimo, lakini hadi sasa ni takribani ekari laki tatu pekee ndizo zimeendelezwa.
“Tunahitaji uwekezaji mkubwa katika zana za kisasa za kilimo. Wakulima ni wengi, lakini bado wanatumia zana duni, hivyo hii ni fursa kubwa kwa wawekezaji, ikiwemo kuanzisha vituo vya zana za kilimo kwa ajili ya kuwahudumia wakulima,” amesema Njawa.
Ameongeza kuwa Morogoro ina zaidi ya viwanda 3,400, kati ya hivyo, vikubwa ni 34, vya kati 64, na vidogo zaidi ya 2,000, hali inayoonesha uhitaji mkubwa wa uwekezaji katika uendelezaji wa viwanda hivyo.
“Tunalima mazao ya kimkakati kwa ajili ya kuvilisha viwanda, hivyo tunahitaji wawekezaji wakubwa ili kuongeza tija na thamani ya mazao,” amesema.
Aidha, amesema yapo mashamba makubwa yaliyochukuliwa na wawekezaji, lakini hayajaendelezwa ipasavyo, pamoja na uhaba wa miundombinu ya kuhifadhi mazao, hali inayofungua fursa kwa uwekezaji katika sekta hiyo.
Kwa upande wake, ofisa biashara mkuu kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Ally Mokiwa, amesema mkoa huo una fursa kubwa katika kilimo cha alizeti, ngano, dengu, mtama, mbaazi pamoja na uchimbaji wa madini ya Tanzanite.
Amesema fursa kubwa zaidi ni kuanzishwa kwa viwanda vya kuchakata mazao hayo, kwa sababu mkoa una hekta milioni 1.3 zinazofaa kwa kilimo, na asilimia 63 tayari zinatumika kwa kilimo, huku hekta 25,000 zikiwa na miundombinu ya umwagiliaji.
“Bado kuna maeneo mengi yanayohitaji miundombinu ya umwagiliaji ili kuongeza uzalishaji wa chakula. Hii ni fursa kubwa kwa wawekezaji,” amesema Mokiwa, akiongeza kuwa mkoa huzalisha takribani tani 637,000 za chakula kwa mwaka.
Naye Mratibu wa Maendeleo ya Uchumi wa Buluu Zanzibar, Mwalimu Nahoda Issa, amesema Zanzibar ina fursa kubwa katika uchumi wa buluu, hususan kwenye maeneo matano makuu ambayo ni uvuvi na mazao ya baharini, utalii, uhifadhi wa bahari, usafiri na usafirishaji pamoja na nishati mbadala.
Amesema kwa muda mrefu Zanzibar imejikita katika uvuvi wa maji ya karibu, lakini sasa inaelekeza nguvu kwenye uvuvi wa maji marefu, jambo linalohitaji uwekezaji mkubwa.
“Tunazalisha dagaa kwa wingi, lakini tunalenga kuongeza thamani kwa kuchakata badala ya kuuza kama malighafi. Tayari tumeanza kujenga viwanda, lakini bado tunahitaji wawekezaji zaidi,” amesema Issa.
Ameongeza kuwa kuna uhitaji mkubwa wa miundombinu ya kuchakata chakula cha samaki, hasa ikizingatiwa kuwa mwelekeo wa dunia unaelekea zaidi kwenye ufugaji wa samaki.
Kwa upande wake, Ofisa Biashara kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara Tanzania Bara, Ramadhan Sizyaa, amesema upotevu wa mazao baada ya kuvuna ni changamoto kubwa inayohitaji mikakati madhubuti ya kudhibiti.
Amesema kati ya asilimia 30 hadi 40 ya mazao nchini hupotea baada ya kuvunwa, huku kwa upande wa matunda pekee asilimia 50 huharibika, mtama na uwele hupotea kati ya asilimia 20 hadi 40, na dagaa hupotea hadi asilimia 60.
“Hali hii inatokana na uhaba wa miundombinu ya vyumba baridi na uhifadhi wa mazao. Kuna haja ya kufanya tafiti na kuwekeza katika miundombinu hiyo ili kudhibiti upotevu,” amesema Sizyaa.
Akihitimisha mdahalo huo, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara Tanzania Bara, Sempeho Manongi, amesema muingiliano wa kibiashara kati ya Zanzibar na Tanzania Bara unaendelea kukua mwaka hadi mwaka.
Amesema mwaka 2022 mauzo ya bidhaa kati ya pande hizo yalifikia Sh37.6 bilioni, ikilinganishwa na Sh33.6 bilioni mwaka 2021. Kwa mwaka 2023/24 mauzo yalifikia Sh95.7 bilioni, huku mwaka 2024/25 yakifikia Sh106 bilioni.
“Muingiliano wa kibiashara ni muhimu kwa maendeleo ya uchumi wetu, na kuna umuhimu wa kuendelea kuimarisha ushirikiano huu kati ya Zanzibar na Tanzania Bara,” amesema Manongi.
