Dar es Salaam. Wakati Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kikitoa msimamo wake ikiwemo kutaka mwenyekiti wake, Tundu Lissu, kuachiwa huru bila masharti, wachambuzi wa siasa nchini wamesema ni muhimu wanasiasa kukaa meza moja kuzungumza na kutanguliza maslahi ya Taifa mbele.
Kauli ya wachambuzi hao inakuja siku moja tangu Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bara), John Heche, kutoa salamu za mwaka mpya 2026, akisema mwaka 2025 haukuwa wa kawaida kwa Watanzania.
Jana, Januari 3, 2026, Heche alisema wanataka Lissu aachiwe bila masharti kwa kuwa si mhaini, hajasema uongo na wala hajafanya uchochezi wowote, bali aliyoyasema ni kweli.
Alisema tangu Lissu alipokamatwa na kuwekwa mahabusu kwa kesi aliyodai kuwa ni ya uongo, batili na yenye uonevu, siku 269 zimepita.
Misimamo mingine ni chama hicho kutaka mageuzi ya kimfumo ya Tume Huru ya Uchaguzi (INEC), Katiba mpya, uchunguzi huru wa kimataifa kuhusu matukio ya mauaji na utekaji, pamoja na kufutwa kwa kesi ya kusitisha shughuli za chama hicho.
Wakizungumzia mapendekezo ya Chadema, leo Januari 4, 2026 wachambuzi wa siasa nchini wametoa maoni tofauti, baadhi wakipinga hatua ya chama hicho kudai mambo makubwa ndani ya muda mfupi, huku wengine wakikiunga mkono na kuhimiza maridhiano.
Mchambuzi wa masuala ya siasa, Profesa Ali Makame, amesema kama kuna la kuwaweka wanasiasa meza moja ili kuzungumza, basi hilo lifanyike.
Hata hivyo, amekumbusha kuwa kabla ya kutokea kwa mambo yaliyobainishwa na Chadema, katika awamu iliyopita hawakuwa wakiruhusiwa kufanya siasa, lakini waliporuhusiwa walitenda makosa yaliyobainika kuwa ni kinyume cha sheria.
Katika kujenga taifa moja, Profesa Makame amesema ni muhimu wanasiasa kukaa na kujadiliana badala ya kutoa kauli zisizojenga taifa.
Kuhusu Katiba mpya, amesema: “Tayari kuna utayari wa kufanya mageuzi kwenye katiba na mengine yataingia humo, ikiwemo mabadiliko ya INEC na kuleta ushirikiano nchini. Sasa kuharakisha viwepo leo badala ya kesho ni kauli za kisiasa ambazo zinaweza zisilete mustakabali mzuri kwenye taifa,” amesema.
Kwa ujumla, Profesa Makame amesema tamko la Chadema limegeukia zaidi kwenye chama kuliko mustakabali wa taifa na mpango wa nchi kuleta mageuzi yanayohitajika.
Amesema mabadiliko yanayotajwa na chama hicho tayari mwanga umeoneshwa na wakuu wa nchi kupitia ahadi zao ndani ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), kwamba changamoto walizotaja zitafanyiwa kazi ndani ya miaka mitano ya utekelezaji.
“Mabadiliko yameshazungumzwa na yameshaahidiwa na viongozi wakuu na yameingizwa kwenye utekelezaji wa Ilani ya CCM kwamba yatafanyika ndani ya miaka mitano. Hii haitoi uhuru wa kukiuka taratibu zilizopo na mipango inayokwenda kuleta mageuzi, katiba ni mchakato mrefu na hakuna anayeweza kuleta katiba kwa siku moja,” amesema.
Kwa upande wake, mchambuzi wa masuala ya siasa, Prince Mwaihojo, amezungumzia takwa la Chadema la uchunguzi wa masuala ya utekaji na mauaji, akisema sio lazima uchunguzi huo uwe wa kimataifa.
“Tunaweza kuwa na tume yetu, lakini watu wakawa na imani nayo. Kilichoipotezea imani tume yetu ya sasa ni kupewa maelekezo na muundo, na maelekezo yaliyotolewa ndio yanaipa nguvu Chadema.
“Tungewajibishana pia, kabla ya kuunda tume, nayo ingekuwa njia nzuri ya kuleta imani kwa watu kuhusu utendaji wa tume husika,” amesema mwanazuoni huyo.
Kuhusu kesi zinazokikabili chama hicho na viongozi wake, Mwaihojo amesema ni muhimu Serikali ikaangalia upya mfumo wa utoaji haki, kwani sio sahihi mtu kukamatwa na baadaye uchunguzi ufanyike.
Amesema jambo hilo linatumika kuumiza na kuwanyamazisha watu, kwani mtu anaweza kukamatwa, kukaa ndani muda mrefu, na baadaye kesi yake kufutwa bila maelezo yoyote.
Mchambuzi wa masuala ya siasa nchini, Dk Matrona Kabyemela, amesema mambo waliyoyaweka Chadema kwenye salamu za mwaka mpya, wamekuwa yakiyapigia kelele kwa mwaka mzima, huku mamlaka zimekuwa kimya kujibu.
“Kwa sasa tulipo, tunahitaji kuwepo kwa engagement (ushirikishwaji) wa wadau wote ili tutoke hapa tulipo. Mambo wanayoyaomba yanahitaji kufikiriwa, kufanyiwa tathmini na kuona yapi yatekelezwe katika mwaka huu ili kuondoa mtanziko wa kisiasa uliopo,” amesema.
Kwa upande wake, mwalimu Samson Sombi amesema kauli ya Chadema katika salamu za mwaka mpya 2026 inaakisi kwa kina hali ya siasa za Tanzania na mwelekeo wa mapambano ya upinzani katika mazingira yenye changamoto za kidemokrasia.
“Msingi wa kauli hiyo ni madai ya kuachiwa huru kwa mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu, jambo ambalo Chadema inaliona kama si suala la mtu mmoja, bali kama kielelezo cha hali ya utawala wa sheria na haki za kisiasa nchini,” amesema.
