Mwanengo aanza na mguu mzuri Yanga ikiichapa KVZ

MSHAMBULIAJI Emmanuel Mwanengo, ameanza na mguu mzuri ndani ya Yanga baada ya kuwa sehemu ya mchango wa ushindi wa mabao 3-0 ilioupata timu hiyo dhidi ya KVZ.

Yanga imepata ushindi huo katika mechi yake ya kwanza kundi C kunako Kombe la Mapinduzi 2026 iliyochezwa leo Januari 4, 2026 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Unguja.

Yanga imepata ushindi huo kupitia mabao ya Pacome Zouzoua dakika ya 32, Celestine Ecua (dk 54) na beki wa KVZ, Juma Shaaban kuusindikiza mpira nyavuni wakati akipambana kuokoa mpiraa uliopigwa na Mwanengo dakika ya 75.

Katika mechi hiyo, Kocha wa Yanga, Pedro Goncalves alimuanzisha Mwanengo eneo la mshambuliaji wa mwisho ambapo nyota huyo aliyetua kikosini hapo hivi karibuni akitokea TRA United alicheza dakika zote tisini.

Mbali na Mwanengo, Mohamed Damaro na Marouf Tchakei, nao walipata nafasi ya kucheza wakiingia kipindi cha pili.
Alianza Damaro kuingia dakika ya 61 akichukua nafasi ya Duke Abuya, kisha dakika ya 76, Ecua akampisha Tchakei.

Nyota hao wapya ndani ya Yanga walionyesha mchezo mzuri kila mmoja kwa nafasi yake kutokana na muda waliopewa.

Ushindi huo unaifanya Yanga sasa kukaa kileleni mwa kundi C la Kombe la Mapinduzi 2026, inahitaji sare au ushindi mechi ya mwisho dhidi ya TRA United itakayochezwa Jumanne Januari 6, 2026 ili kujihakikishia kufuzu nusu fainali.

Endapo Yanga itafuzu nusu fainali, itakwenda kucheza na timu itakayoshika nafasi ya pili kutoka kundi A ambapo Singida Black Stars imeshatangulia ikiwa na pointi tano, Azam na URA zinazocheza kesho, yeyote atakayeshinda atakaa kileleni na Singida ikibaki nafasi ya pili kwani timu hizo hivi sasa zina pointi nne kila moja.