Sakata la Yona lachukua sura mpya, afanya uamuzi

WAKATI tetesi za usajili za kunyemelewa na vigogo Simba na Yanga zikizidi kushika kasi, kipa tegemeo wa Pamba Jiji, Yona Amosi inadaiwa hajaripoti kambini jijini Mwanza ambako timu hiyo inaendelea na mazoezi.

Pamba ilirejea kambini tangu Desemba 29, mwaka jana ikijifua kwenye Uwanja wa Nyamagana ikijiandaa na ngwe nyingine ya Ligi Kuu Bara inayorejea upya Januari 21 baada ya kusimama karibu mwezi mzima kupisha fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 inayoendelea huko Morocco.

Yona anayehusishwa na Simba na Yanga zinazosaka makipa kupitia dirisha dogo, alikosekana katika mazoezi ya timu hiyo yaliyofanyika Ijumaa iliyopita akiwa mmoja ya wachezaji ambao hawajaripoti kambi ya timu hiyo hadi sasa, huku kuchelewa kwake kukihusishwa na dili hilo la kutaka kujiunga na vigogo hao waliopo Kombe la Mapinduzi 2026.

YON 01

Akizungumzia sakata hilo, Msemaji wa Pamba Jiji, Moses William alithibitisha, ni kweli nyota huyo ambaye ni nahodha msaidizi wa kikosi hicho hajaripoti kambini pamoja na baadhi ya wachezaji wengine, huku wakiwa na matumaini kwamba ataungana na wenzake hivi karibuni.

“Kimsingi tayari tumeanza mazoezi, ni kweli Yona Amosi hajawasili mazoezini na sio peke yake tu wapo wachezaji wengine ambao hawajafika. Na sisi tunajua hajafika kwa sababu gani yeye na familia yake na mambo mengine,” amesema William na kuongeza;

“Tunachofahamu ni hicho, taarifa nyingine zozote juu ya yeye (Yona) hatuna, lakini tunachofahamu kipa huyo atawasili kambini kwa sababu bado ana mkataba nasi na ataendelea na mazoezi, lini na wapi tutawaambia, lakini atakuja mazoezi kama kawaida.”

YON 01 (1)

William amesema hadi sasa klabu hiyo haijapokea ofa, mazungumzo ama mawasiliano yoyote ya kumhitaji Yona kutoka klabu yoyote ya hapa nchini au nje, huku akisisitiza kuwa nyota huyo bado ana mkataba na Pamba Jiji.

“Hadi ninavyozungumza nawe kupitia kwa CEO na mwenyekiti wangu bado hakuna taarifa rasmi, sio Yona tu za mchezaji yeyote kuhitajika na timu hizo (Simba na Yanga) ama kwenda klabu nyingine zikiwamo za nje, tofauti na wale ambao tumekubaliana kuwaruhusu kuondoka,” amesema William.

Yona aliyewahi kuidakia Tanzania Prisons amekuwa akihusishwa na Yanga tangu msimu uliopita kabla ya kuibukia Pamba Jiji na sasa amerudi katika vichwa vya habari akitakiwa na timu hiyo sambamba na Simba ambayo makipa wake wawili, Yakoub Suleiman na Moussa Camara wote ni majeruhi wa muda mrefu.