WAKATI taarifa zikienea kuhusu kuondoka kwa mmoja kati ya viungo wa Simba mambo yamebadilika ghafla, huku mabosi wakitaka abaki hadi mwishoni mwa msimu huu.
Simba imekuwa na wakati mgumu msimu huu ikiwa imeshapoteza michezo miwili ya Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini ikipoteza pia mechi moja ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Azam baada ya kucheza michezo mitano.
Iko hivi, hapo awali Simba ilikuwa kwenye mipango ya kumtoa kwa mkopo kiungo wake Awesu Awesu kwenda klabu ya Mbeya City, ila hivi karibuni mambo yamebadilika.
Sababu za Simba kufungua mlango wa mazungumzo na Mbeya City ni kutokana na ugumu wa namba ambao Awesu alianza kuupitia tangu wakati wa kocha Fadlu Davids akiwa alijiunga na timu hiyo akitokea KMC kama mmoja kati ya wachezaji mahiri wa timu hiyo.
Taarifa za ndani kutoka Simba zimelieleza Mwanaspoti kuwa, timu hiyo imeshindwa kufikia makubaliano kati yake na Mbeya City na changamoto kubwa ilikuwa ishu ya maslahi.
“Pande zote mbili zimeshindwa kukubaliana hivyo Awesu ataendelea kusalia Simba, huo ndio mpango uliopo kwa sasa na tayari Mbeya City imeshatafuta mbadala wake mapema tu.
“Simba ilikuwa inataka kumtoa kwa mkopo Awesu kutokana na ugumu wa namba aliokuwa akiupitia ila wameshindwa kufikia makubaliano kutokana na ishu za kimaslahi ambayo mchezaji mwenyewe hakuyaridhia, lakini Simba wenyewe wanaonekana kuwa wanataka mchezaji huyo abaki klabuni mwalimu amwangalie kwanza,” kilisema chanzo.
Hata hivyo, inaelezwa kuwa Mbeya City imeshapata mbadala wake ambao ni Omary Omary kutoka Mashujaa ambaye tayari wameshaanza mazungumzo naye ili aweze kuchukua nafasi hiyo.
Simba iko Zanzibar na jana iliingia uwanjani kuvaana na Muembe Makumbi kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi inayoendelea visiwani humo ukiwa ni mchezo wa kwanza wa kocha mpya wa timu hiyo Steve Barker.
