New York. Rais wa Venezuela, Nicolás Maduro, huenda akafikishwa mahakamani jijini New York, Marekani, kesho Jumatatu, Januari 5, 2026, baada ya kukamatwa na mamlaka za Marekani katika shambulizi la kushtukiza alfajiri ya jana na kumsafirisha kwa ndege hadi nchini humo, imeripoti NBC News.
Maduro na mkewe, Cilia Flores, wanakabiliwa na mashtaka nchini Marekani ya kula njama ya ugaidi wa mihadarati, kula njama ya kuingiza dawa za kulevya (kokeini) nchini humo pamoja na makosa yanayohusiana na silaha.
Jana, Januari 3, 2026, katika mkutano wake na waandishi wa habari, Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema Marekani “itaisimamia” Venezuela kwa muda usiojulikana na itatumia akiba yake ya mafuta.
Trump hajaondoa uwezekano wa kupeleka wanajeshi wa Marekani nchini Venezuela. Makamu wa Rais wa Venezuela, Delcy Rodríguez, amesisitiza kuwa Venezuela italinda rasilimali zake kwa ajili ya wananchi wake.
Mahakama ya Juu ya Venezuela, jana, iliamuru Rodríguez achukue nafasi ya Rais wa mpito mara moja kufuatia Maduro kuwa kizuizini nchini Marekani.
Hatua ya kushangaza ya Serikali ya Marekani kumuondoa madarakani na kumkamata kiongozi wa nchi ya kigeni imepokelewa kwa pongezi kutoka kwa wafuasi wa Trump, lakini pia imekumbwa na ukosoaji kutoka pande zote mbili za kisiasa.
Baadhi ya wabunge wa Marekani wanahoji uhalali wa shambulio hilo na kueleza hofu kuwa linaweza kuingiza Marekani katika vita vingine vya gharama kubwa na vya muda mrefu.
Trump amesifu kile alichokiita operesheni “iliyopangwa kwa ustadi” wa kijeshi iliyodaiwa kusababisha kukamatwa kwa Rais wa Venezuela, Nicolás Maduro, na mkewe, Cilia Flores, huku Serikali ya Venezuela ikitaka ithibitishiwe uhai wa viongozi hao na kulaani hatua za Marekani.
Akizungumza na gazeti la The New York Times saa chache baada ya kutangaza operesheni hiyo kupitia mtandao wake wa Truth Social mapema Jumamosi, Trump amesema operesheni hiyo ilihusisha mipango mizuri na vikosi bora vya kijeshi.
Wakati Mahakama ya Juu ya Venezuela ikiamuru Makamu wa Rais, Delcy Rodríguez, kuchukua madaraka ya urais kwa muda, Rais Trump ametangaza kuwa Marekani itaiongoza nchi hiyo kwa muda.
Operesheni ya kumkamata Maduro na mkewe wakiwa wamelala chumbani kwao ilifanywa na majeshi ya Marekani kwa kutumia zaidi ya helikopta za kijeshi 150 zilizovamia makazi ya Maduro.
Kufuatia kukamatwa kwa Maduro na kusafirishwa jijini New York kwa mashtaka, Venezuela imebaki bila Rais, na Mahakama ya Juu ilisema kuwa Makamu wa Rais Rodríguez lazima “achukue na kutekeleza mamlaka na majukumu yote ya urais kwa hadhi ya kaimu, ili kuhakikisha mwendelezo wa uendeshaji wa Serikali na ulinzi wa taifa kwa ujumla.”
Katiba ya Venezuela inaeleza kuwa endapo Rais atashindwa kutekeleza majukumu yake kwa muda au kabisa, makamu wa rais ndiye anayepaswa kuchukua nafasi hiyo.
Hata hivyo, mahakama haikutangaza rasmi kuwa Rais Maduro hana uwezo wa kudumu wa kuendelea na majukumu yake.
Mahakama hiyo pia ilitangaza kuwa itaendelea kujadili suala hilo ili “kubaini mfumo wa kisheria unaopaswa kutumika kuhakikisha mwendelezo wa dola, uendeshaji wa serikali, na ulinzi wa mamlaka ya kitaifa, katika mazingira ambayo Rais hayupo kwa kulazimishwa.”
Wakati Mahakama ikitoa uamuzi huo, Trump naye katika mkutano na waandishi wa habari amesema kuwa Marekani itakuwa “ikiisimamia Venezuela kwa muda mfupi ili kuleta utulivu, hadi pale kutakapokuwa na uhamishaji wa madaraka kwa amani.”
Katika mahojiano mengine ya vyombo vya habari, Trump amesisitiza kuwa hakutakuwa na uwepo wa wanajeshi wa Marekani nchini Venezuela iwapo uongozi wa upande wa Venezuela “utazingatia matakwa ya Marekani.”
Katika mahojiano ya kipekee na New York Post, Trump alipoulizwa iwapo wanajeshi wa Marekani watasaidia kuendesha nchi moja kwa moja, amejibu, “Hapana,” akiongeza kuwa, “Iwapo Makamu wa Rais wa Maduro atafanya tunavyotaka, hakutakuwa na haja ya kufanya hivyo.”
Amedai pia amekuwa na mawasiliano ya mara kwa mara na Makamu wa Rais Rodríguez na kwamba “anaelewa hali ilivyo.”
Hata hivyo, Makamu wa Rais Rodríguez alitoa msimamo tofauti katika kikao cha dharura cha baraza la mawaziri, akisema, “Venezuela, kuna Rais mmoja tu, Maduro,” na kusisitiza kuwa, “Rais Maduro ndiye kiongozi wetu na kamanda mkuu wa majeshi.”
Hali hiyo imezua mvutano mkubwa wa kisiasa na kikatiba nchini Venezuela, huku jamii ya kimataifa ikiendelea kufuatilia kwa karibu mwelekeo wa uongozi na mustakabali wa nchi hiyo.
