Stars yatolewa kwa mbinde Afcon 2025

RABAT, MOROCCO: HATUWADAI wanetu. Walisikika mashabiki wa Taifa Stars jijini Dar es Salaam usiku wa Jumapili baada ya kuishuhudia timu yao ya soka ikitupwa nje ya mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 kwa mbinde kwa kufunga bao 1-0 na wenyeji Morocco huko jijini Rabat.

Tanzania chini ya kocha Miguel Gamondi ilicheza kwa nidhamu kubwa katika mchezo huo na kuitishia Morocco mara kadhaa kwa mashambulizi ya kushtukiza, huku ikinyimwa penalti katika dakika za majeruhi za mchezo huo.

Baada ya soka matata katika kipindi cha kwanza na kufanya ubao wa matokeo usomeke 0-0, mambo yaliendelea kuwa magumu kwenye kipindi cha pili, hadi hapo nahodha wa Morocco, Achraf Hakimi, alipopiga pasi ya mwisho kwa Brahim Diaz, ambaye alimlamba chenga beki wa Stars kabla ya kupiga shuti lililomshinda kipa Hussein Masalanga na kutinga nyavuni.

Akianza kwa mara ya kwanza baada ya zaidi ya miezi miwili kufuatia majeraha ya kifundo cha mguu, beki wa kulia wa Paris Saint-Germain, Hakimi, alimpatia Diaz pasi nzuri iliyomruhusu kufunga kwa shuti lililopita kipa Masalanga, aliyekuwa ameshindwa kuziba goli lake vyema.

Bao hilo limemfanya Diaz kuwa Mmorocco wa kwanza kufunga mabao katika mechi nne mfululizo kwenye mashindano ya Afcon, huku alikuwa pia mfungaji bora wa michuano hiyo katika kipindi cha mechi za kufuzu wakati alipotikisa nyavuni mara saba.

Hakimi alipiga faulo kali iliyogonga mwamba wa juu wa lango ikiwa ni sehemu ya mashambulizi mfululizo ya Morocco baada ya mapumziko, huku Masalanga akiokoa kwa ustadi mkubwa kichwa cha karibu cha Abde Ezzalzouli, na Ayoub El Kaabi akakosa kwa kichwa baada ya mpira wa krosi kutoka kwa Hakimi.

Feisal Salum alipata nafasi bora zaidi kwa Tanzania muda mfupi kabla ya bao la Diaz, alipoinua mpira uliorudi baada ya golikipa wa Morocco, Yassine Bounou kushindwa kudhibiti shuti la beki wa kushoto wa Stars, Mohamed Hussein lililopigwa kutoka mbali.

Stars pia ilipoteza nafasi ya kufunga mwanzoni mwa kipindi cha kwanza wakati Simon Msuva kushindwa kuunganisha vyema kwa kichwa krosi maridadi iliyochongwa na Selemani Mwalimu.

Dakika za majeruhi, Tanzania ilistahili kupewa penalti baada ya Iddy Suleiman Nado kuangushwa ndani ya boksi, lakini mwamuzi Boubou Traore kutoka Mali hakutaka kujishughulisha na chochote ikiwamo kwenda kuangalia picha za marejeo ya tukio hilo kwenye VAR.

Morocco, ambao ni wenyeji wa mashindano ya Afcon 2025 sasa wametinga robo na watakipiga na mshindi baina ya Afrika Kusini na Cameroon, ambazo zilitarajia kumenyana usiku huo wa Jumamosi. Mechi ya robo fainali itafanyika Ijumaa wiki hii.