Ungependa kukutana na nani mwanzo wa mwaka

Bwana Yesu asifiwe! Ni matumaini yangu mmeupokea Mwaka Mpya wa 2026 kwa amani na utulivu na neema ya Mungu ikae nawe msomaji wangu kwa mwaka mzima kila hatua uso wa Mungu uwe nawe.

Mwanzo wa mwaka mpya huja na matarajio mapya, maamuzi mapya na ndoto mpya.

Watu wengi hujiuliza: Nitakutana na nini mwaka huu? Nitapata mafanikio gani? Lakini swali la muhimu zaidi kwa muumini ni hili: Ungempendelea kukutana na nani mwanzo wa mwaka mpya?

Jibu la swali hili linaweza kuamua mwelekeo mzima wa maisha yako ya kiroho na hata ya kimwili.

Biblia inatuonyesha wazi kwamba kukutana na Yesu Kristo hubadilisha historia ya maisha ya mtu kabisa.

Katika Biblia tunakutana na watu waliokuwa na shauku kubwa ya kukutana na Yesu.

Mfano wa kwanza ni Zakayo, aliyekuwa mkuu wa watoza ushuru (Luka 19:1–10). Zakayo alikuwa tajiri, lakini moyo wake haukuwa na amani.

Aliposikia Yesu anapita Yeriko, alitamani sana kumuona. Ingawa alikuwa mfupi wa kimo na umati ulikuwa mkubwa, hakukata tamaa. Alipanda mtini ili aweze kumuona Yesu.

Juhudi zake zilionyesha kiu ya ndani ya moyo wake. Yesu alipofika pale, alimwita Zakayo kwa jina na kusema, “Imempasa leo kushuka, kwa kuwa leo imenipasa kukaa nyumbani mwako.”

Kukutana huko kulibadilisha maisha ya Zakayo: alitubu, akarejesha aliyodhulumu, na wokovu ukaingia nyumbani mwake.

Hii inatufundisha kwamba anayetamani kwa dhati kukutana na Yesu hatabaki vilevile.

Mfano wa pili ni Paulo (Saulo wa Tarso). Kabla ya kukutana na Yesu, Paulo alikuwa adui wa kanisa, akiwatesa waumini kwa bidii (Matendo ya Mitume 9).

Alidhani anamtumikia Mungu, kumbe alikuwa mbali na mapenzi ya Mungu. Lakini katika safari yake kwenda Dameski, alikutana na Yesu kwa namna ya ajabu. 

Mwangaza kutoka mbinguni ulimuangazia, akasikia sauti ya Bwana ikisema, “Saulo, Saulo, mbona wanitesa?” Kukutana huko kulimgeuza kabisa.

 Kutoka kuwa mtesaji wa kanisa, akawa mtume mkuu wa Injili. Maisha yake, malengo yake na mwelekeo wake vyote vilibadilika kwa sababu ya kukutana na Yesu.Zaidi ya hapo, Paulo mwenyewe anaonyesha thamani ya mahusiano ya kiroho katika maandiko yake. Katika 2 Timotheo 1:4, anasema: “Nikiikumbuka machozi yako, ninatamani sana kukuona, nipate kujazwa furaha.”

 Maneno haya yanaonyesha hamu ya ndani ya kukutana, si kwa faida ya kimwili, bali kwa ajili ya faraja, upendo na kuimarishana kiroho.

Hivyo, kukutana na Yesu hutujaza furaha ya kweli, amani ya moyo na nguvu mpya ya kuendelea na safari ya maisha.

Mwanzo wa mwaka mpya ni wakati mzuri wa kufanya uamuzi wa kiroho: kumweka Yesu mbele ya mipango yetu yote.

Tunaweza kukutana na watu wengi, fursa nyingi na changamoto nyingi, lakini hakuna kukutana kuliko muhimu kama kukutana na Yesu.

Yeye ndiye anajua jana yetu, leo yetu na kesho yetu. Kukutana naye hutupa msamaha, mwelekeo na tumaini jipya.

Mtume Paulo alitamani sana kumwona Timotheo kwa sababu ya aina ya tabia yake ya kipekee ya huruma na maombi ya machozi.

Kuna watu tabia zao zinakutamanisha kuwaona au kukutana nao.

Zakayo alitamani kumwona Bwana Yesu au kukutana naye kwa sababu ya taarifa nyingi alizosikia zilizomuhusu Bwana Yesu.

Herode alitamani kumwona Bwana Yesu kwa sababu alisikia kuwa alikuwa anafanya miujiza mingi.

Je una tabia ambayo watu inawavutia kutaka kukuona au kukutana nawe?

Kuna watu kukutana nao ni baraka kubwa mwanzo wa mwaka  mpya.

 Tamani kukutana na watu wenye hekima mwanzo wa mwaka mpya.

Pia tamani kukutana na watu waombaji wa kina mwanzo wa mwaka mpya. Tamani kukutana na watu wanaoweza kukushauri cha kufanya mwanzo mwaka mpya

Tamani kukutana na mashujaa wa imani mwanzo wa mwaka mpya.

Vilevile tamani kukutana na watu waliofanikiwa katika maisha kipindi hiki cha mwanzo wa mwaka mpya.

Mungu akukutanishe na mtu ambaye una shauku ya kumwona na kukutana naye atakayekuwa msaada kwenye maisha yako kuanzia Januari hadi Desemba 31 mwaka huu.

Uwe tayari kufanya juhudi. Kama Paulo, uwe tayari kubadilishwa.

 Jambo kubwa na la muhimu tamani kukutana na Yesu, mwaka wako hautakuwa wa kawaida, bali utakuwa mwaka wa mabadiliko, wokovu na kusudi jipya kutoka kwa Mungu. Wengi wanaumiza vicha kuhusu ada, kodi na mambo mbalimbali, mshirikishe Yesu Kristo aliyehai ukutane naye katika shida zako.