Kampala. Kukamatwa na kisha kuwekwa rumande kwa Sarah Bireete, mtetezi mashuhuri wa haki za binadamu na mtaalamu wa masuala ya utawala, kumesababisha mshtuko mkubwa ndani ya jumuiya ya kiraia nchini Uganda.
Mwanaharakati huyo amekamatwa zikiwa zimebaki takribani siku 10 kuelekea uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika Januari 15, 2026, huku Rais Yoweri Museveni akikabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa mgombea wa NUP, Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine.
Kwa miaka mingi, Bireete amekuwa mkosoaji wa wazi wa vitendo vya kupindukia vya Serikali, mtetezi asiyechoka na nguzo ya kulinda uhuru wa kiraia.
Kukamatwa kwake ghafla hakujawatikisa tu wenzake, bali pia kumeacha kivuli cha hofu juu ya nafasi finyu ya demokrasia nchini humo.
Katika siku zilizofuata baada ya kukamatwa kwake, minong’ono ilisambaa kwa kasi miongoni mwa wanaharakati, wanahabari na wataalamu wa utawala. Ujumbe ulikuwa wazi: kama mtu mashuhuri na anayeheshimika kama Bireete anaweza kukamatwa, basi hakuna aliye salama.
Watetezi wa haki za binadamu walianza kuzungumza kwa sauti ya chini, kuepuka mikusanyiko ya hadhara, na kupunguza uwepo wao mtandaoni.
“Tunaogopa,” alikiri mwanaharakati mmoja aliyeomba utotajwa jina. “Tunajua kamatakamata zaidi inakuja. Wanataka kututisha ili tunyamaze.”
Hofu hiyo si ya kubuni. Vyanzo vya karibu na mashirika ya kiraia vimeeleza kuwa vyombo vya usalama vimeandaa orodha ya wakosoaji wenye sauti kali, hususan wale wanaotumia mitandao ya kijamii.
Watu hao wanatuhumiwa kwa “kuhujumu uthabiti wa taifa” au “kusambaza taarifa za uongo,” mashtaka ambayo wakosoaji wanasema ni ya jumla na yanachochewa kisiasa.
Yusuf Sserukuma, mhadhiri wa chuo kikuu, amesema lengo kuu la kukamatwa kwa Bireete ni kuwatisha wanaharakati wa haki za kiraia na kuwafanya wanyamaze kwa kuwalenga watu mashuhuri zaidi miongoni mwao.
“Uganda si nchi ya kidemokrasia, licha ya kudai kuwa ina demokrasia. Kukamatwa kwake hakuonyeshi nguvu ya demokrasia ya Uganda, bali kunasisitiza tena kwamba madai hayo si chochote zaidi ya kujifanya,” alisema Sserukuma.
Winnie Kiiza, aliyewahi kuwa Kiongozi wa Upinzani Bungeni (LoP), amesema kupitia chapisho la mitandao ya kijamii kuwa ana “wasiwasi mkubwa na wa dhati kuhusu mwelekeo ambao nchi yetu inaelekea.”
Hakuwa peke yake. Ndebesa Mwambutsya, mhadhiri wa sayansi za jamii katika Chuo Kikuu cha Makerere, amesema kukamatwa kwa Bireete na sauti nyingine za ukosoaji ni jambo linalotia doa kubwa.
“Huwezi kudai unaendesha demokrasia halafu ukakataa uwepo wa upinzani wa kisiasa. Ama ukubali kile kinachoitwa Ukomunisti wa Kidemokrasia (Democratic Centralism) kama ilivyo China, ambako upinzani unaharamishwa na raia kulazimishwa kunyamaza, au ufungue nafasi kwa sauti tofauti,” ameeleza Mwambutsya.
“Kuhusu haki za binadamu na utu wa mwanadamu, Serikali inavunja vyote viwili. Fikiria kuwapiga watu kama ambavyo jeshi linafanya, na hivyo kudhalilisha utu wao. Madhara yake yako wazi: raia wanateseka, lakini pia dola inapoteza uhalali mbele ya wananchi wake na katika jamii ya kimataifa. Uhalali unapodhoofika na imani kati ya raia na taasisi za dola inapovunjika, dola huwa dhaifu,” ameongeza.
Kukamatwa kwa Bireete kunaashiria hatua mpya katika mapambano ya kiraia nchini Uganda na awamu mpya ya ukandamizaji, inayowalenga viongozi wa kimaadili na kiakili wa jumuiya ya kiraia. Kwa wataalamu wa utawala, changamoto ni kubwa. Wanalazimika kutafuta njia za kuendelea na kazi yao chini ya ufuatiliaji, vitisho na hatari ya kukamatwa.
Kwa watetezi wa haki za binadamu, jukumu ni gumu zaidi, kulinda uhuru wakati wao wenyewe wanashambuliwa. Safari iliyo mbele haijulikani, lakini jambo moja liko wazi, mapambano ya kulinda nafasi ya kiraia nchini Uganda bado hayajaisha. Kadiri sauti zinavyoendelea kusikika, hata kama ni dhaifu, mapambano yataendelea.
Wataalamu wa masuala ya utawala wamesema kukamatwa kwa Bireete kunachukuliwa kama sehemu ya mkakati mpana wa kuwatisha wale wanaotumia majukwaa ya kidijitali kuikosoa mamlaka.
“Kuanzia manyanyaso dhidi ya wanasiasa wa upinzani hadi kupigwa kwa wanahabari, mara nyingi dola imekuwa ikitumia mbinu kali. Hata hivyo, wimbi la sasa la kukamatwa linaonekana kuwa tofauti.”
Safari hii, mkazo uko wazi kwa watetezi wa haki za binadamu na wataalamu wa utawala, watu wanaotoa msingi wa kiakili wa upinzani wa kiraia. Kuondolewa kwao katika anga ya umma kunadhoofisha uwezo wa raia kudai uwajibikaji. Waangalizi wanaonya kuwa mwenendo huu unaweza kudhoofisha zaidi taasisi za kidemokrasia, na kuwaacha wananchi na njia chache za kueleza malalamiko au kutafuta haki.
Mtaalamu wa siasa, Charity Aketch, amesema kukamatwa huko hakujapita bila kutambuliwa nje ya mipaka ya Uganda. Mashirika ya kimataifa ya haki za binadamu yameeleza wasiwasi wao, yakitaka aachiliwe mara moja na kuhimiza serikali kuheshimu uhuru wa kiraia.
