Waziri Kombo: Kuna haja ya kuwa na viongozi wenye ujuzi wa kuzungumza

Unguja. Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo, amesema kutokana na mabadiliko ya ulimwengu, kuna haja ya kuwa na viongozi wenye maarifa ya kisiasa na ujuzi wa kuzungumza, watakaosimama imara kuilinda nchi na kuitetea kwa maslahi ya Taifa.

Balozi Kombo ameasema hayo leo, Januari 4, 2026, katika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la jengo la mafunzo kwa watumishi wa Chuo Kikuu cha Utawala wa Umma (IPA), iliyofanyika Wilaya ya Kati, mkoani Kusini Unguja.

Amesema baada ya kutokea mambo yasiyoridhisha kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, Tanzania ilichafuka duniani, hivyo bila kuwa na ujuzi na maarifa ya uongozi, wangeshindwa kuisafisha na kuifikisha ilipo kwa sasa.

“Baada ya uchaguzi, Tanzania ilichafuka duniani kote kwa kuenea kwa taarifa ambazo hazikuwa na ukweli ndani yake, zikieleza kuwa nchi inawaka moto na kuteketea,” amesema waziri huyo.

Ameeleza kuwa mambo yote yaliyotokea Oktoba 2025 yamedhoofisha uchumi wa nchi na kutia hasara iliyokwenda kuwaumiza zaidi wananchi wanyonge.

Hivyo, amesema alipotumwa akiwa waziri mwenye dhamana, alijifunza mambo matatu, ikiwemo namna ya kuzungumza na viongozi wa nchi tofauti, namna ya kuzungumza na vyama vya siasa, na kukabiliana na serikali za umoja wa kimataifa na zisizo na umoja huo.

Balozi huyo amesisitiza kuwa amani na utulivu uliopo nchini si jambo la bahati, bali ni matokeo ya uongozi wenye dira na sera sahihi kutoka kwa viongozi wakuu wa nchi.

Amesema kupitia ujenzi wa jengo hilo, chuo hicho kitaendelea kuandaa viongozi wenye uwezo katika nyanja mbalimbali, ikiwemo uongozi wa kimkakati na kimaadili, utekelezaji wa mageuzi ya utumishi wa umma, usimamizi bora wa rasilimali za umma, na thamani ya fedha.

Pia, amesema chuo hicho kitatoa uimarishaji wa uwajibikaji na utawala bora, matumizi ya ubunifu na teknolojia ya serikali mtandao, pamoja na maandalizi ya viongozi wa kizazi kijacho.

“Hatua hizi zote zina uhusiano wa moja kwa moja wa kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi. Kwa msingi huo, nawasihi sote tuendelee kushirikiana kwa karibu na viongozi wetu katika kusimamia na kuhakikisha utekelezaji wenye ufanisi wa shughuli zote za umma kwa maslahi mapana ya Taifa,” amesema.

Sambamba na hilo, amesema mageuzi ya utumishi wa umma si hiari bali ni lazima, na mageuzi hayo yanahitaji mabadiliko ya mifumo, taratibu na mienendo ya kifikra kwa viongozi.

Aidha, amesema kukamilika kwa jengo hilo kutatoa fursa mbalimbali kwa sekta zote, zikiwemo binafsi, ili kuwajengea uwezo wa kiutendaji katika sekta zao.

Kwa upande wake, mkuu wa chuo hicho, Dk Shaaban Mwichum Suleiman, amesema jengo hilo limegharimu Sh4.8 bilioni, ambapo Sh3 bilioni zimeshalipwa kwa mkandarasi anayejenga jengo hilo.

Amesema sababu ya kujengwa kwa jengo hilo ni kuwa chuo hicho kilikuwa kikitumia kumbi za vyuo vingine kutoa mafunzo kwa watumishi wa umma, jambo lililowalazimu kulipia.

Pia, amesema jengo hilo litaondoa changamoto hiyo kwa watumishi kupata mafunzo hayo chuoni hapo na kuimarisha miundombinu.

Dk Shaaban ameiomba wizara hiyo kukiweka chuo hicho kwenye majadiliano ya kutafuta ufadhili kwa lengo la kuchochea ufanisi wa chuo.

Naye, mwenyekiti wa baraza la chuo hicho, Abdulhamid Yahya Mzee, amesema jengo hilo ni miongoni mwa matunda ya Mapinduzi, hivyo chuo hicho kipo kutoa huduma kwa wanafunzi na viongozi.

Mwenyekiti huyo ametoa wito kwa taasisi za Serikali na binafsi kukitumia chuo hicho kupata mafunzo kwa lengo la kuwa waadilifu na weledi katika kazi zao.