Dar es Salaam. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Uhusiano, Deus Sangu ametembelea Ofisi za Makao Makuu ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) jijini Dar es Salaam kwa lengo la kujitambulisha kwa viongozi wa Baraza hilo pamoja na kulitambulisha jukumu jipya la uhusiano ambalo Wizara yake imekabidhiwa kuratibu.
Sangu alipokelewa na Mufti na Mwenyekiti wa Bakwata, Sheikh Abubakar Zubeir bin Ally, pamoja na wajumbe wa Baraza hilo, kala ya kufanya kikao cha pamoja cha kujadili masuala mbalimbali yenye maslahi kwa taifa.
Akizungumza katika kikao hicho jana Jumamosi Januari 3, 2026, Waziri Sangu amepongeza kazi zinazofanywa na baraza hilo alizosema kuwa zina mchango mkubwa katika kuimarisha amani, umoja na mshikamano nchini.
Amesema Bakwata limeendelea kuwa nguzo muhimu ya maadili na mshikamano wa kijamii kwa kuhimiza mazungumzo ya amani, kuvumiliana na uhusiano mzuri kati ya waumini wa dini ya Kiislam na nyingine.
“Juhudi hizi zimechangia kwa kiasi kikubwa kudumisha utulivu na mshikamano wa kitaifa,” amesema Sangu.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na taasisi za dini katika kukabiliana na changamoto za kijamii, kiuchumi na kisiasa, pamoja na masuala ya kikanda na kimataifa, akitaja malezi bora na maadili kuwa msingi wa maendeleo ya jamii.
Pia, ameihakikishia Bakwata kuwa Serikali ya itaendelea kushirikiana na taasisi za dini, ikiwamo Bakwata, katika kuendeleza agenda ya amani, mshikamano na maendeleo jumuishi.
Awali akizungumza wakati anamkaribisha waziri huyo, Mufti Mkuu wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir, alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutambua umuhimu wa masuala ya uhusiano na kuanzisha Wizara mahsusi inayosimamia eneo hilo.
Aidha, aliishukuru Serikali kwa kutambua na kuthamini mchango wa Bakwata, akiahidi kuwa Baraza hilo litaendelea kushirikiana kwa karibu na Serikali katika kuimarisha umoja wa kitaifa, amani na mshikamano nchini.