BAADA ya kukaa nje ya uwanja kwa nusu msimu mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Yacouba Songne amekamilisha dili la kuitumikia Mbeya City.
Mshambuliaji huyo aliyepita Ihefu, Tabora United ambayo ameitumikia kwa nusu msimu akijiunga nayo akitokea AS Arta Solar ya Djibouti amerudi tena ligi kuu baada ya kujitibia jeraha lake la goti lililomuweka nje kwa nusu msimu.
Dirisha dogo la usajili limefungwa Alhamisi, Januari Mosi ambapo baadhi ya timu tayari zimeweka wazi usajili wao huku nyingine zikipiga kimyakimya.
Yacouba raia wa Burkina Faso ambaye alikuwa mchezaji huru baada ya kumaliza mkataba wake wa mwaka mmoja na Tabora United imeelezwa kuwa tayari amesaini mkataba wa mwaka mmoja na Mbeya City.
Hata hivyo, habari za uhakika lilizopata Mwanaspoti ni kuwa katika mkataba huo kipo kipengele cha kuongeza muda iwapo ataonyesha uwezo wa kuisaidia timu hiyo kubaki ligi kuu baada ya kurejea mapema msimu huu.
Mwanaspoti lilifanya juhudi ya kumtafuta Yacouba ambaye yupo nchini ili kuthibitisha taarifa hizo, ambapo amesema hayupo tayari kuzungumzia suala hilo kwa sasa na muda muafaka ukifika kila kitu kitawekwa wazi kwani mpira sio mchezo wa kujificha bali unachezwa hadharani.
“Nipo salama naendelea vizuri baada ya matibabu yangu ya goti muda ukifika ni timu gani nitacheza itafahamika kwani mpira ni mchezo wa wazi nikitua hiyo timu au timu nyingine nitaonekana na jukumu la kuthibitisha kama nimemalizana na timu ni uongozi mimi kazi yangu kucheza.”
