Zaidi ya Wananchi 1,000 Wanufaika na Kambi ya Uchunguzi wa Moyo Arusha

Na Pamela Mollel,Arusha

Kambi maalum ya uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo inayofanyika katika Hospitali ya Rufaa ya Mount Meru (ALMC) jijini Arusha, kwa ushirikiano kati ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na ALMC, imeendelea kuwafikia wananchi wengi wa Mkoa wa Arusha na maeneo ya jirani kwa kutoa huduma za kibingwa kwa watu wazima na watoto.

Akizungumza jijini Arusha, Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Onesmo Mkude, amewahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kuchangamkia fursa ya upimaji wa magonjwa ya moyo unaotolewa kupitia kambi hiyo, akisisitiza kuwa uchunguzi wa mapema ni hatua muhimu katika kuokoa maisha na kupunguza gharama za matibabu.

Tangu kuanza kwa kambi hiyo Desemba 29, 2025 hadi Januari 4, 2026, zaidi ya wananchi 1,000 wamepata huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo katika hospitali hiyo. Kati yao, watu wazima zaidi ya 700 na watoto zaidi ya 100 wamehudumiwa, sawa na wastani wa wagonjwa 155 hadi 200 kwa siku.

Huduma za kibingwa zikiwemo vipimo vya ECHO na ECG zimefanyika, huku wagonjwa 53 wakifanyiwa tathmini kwa ajili ya upasuaji wa moyo. Kati ya wagonjwa hao, upasuaji mkubwa wa moyo kwa wagonjwa watano tayari umefanikiwa kufanyika.

Aidha, wagonjwa 45 wamepewa rufaa kwenda Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dar es Salaam kwa matibabu zaidi, wakiwemo watu wazima 37 na watoto 8, hatua inayolenga kuhakikisha wanapata huduma za kibingwa za kiwango cha juu.

Mkude aliwataka waandishi wa habari na wadau wa mawasiliano kuhakikisha taarifa sahihi zinawafikia wananchi wengi zaidi, ikizingatiwa kuwa kambi hiyo itaendelea hadi Januari 9, 2026, ili wananchi wengi wajitokeze kunufaika na huduma hizo muhimu za afya ya moyo.

Kwa ujumla, tathmini ya awali inaonesha kambi hiyo imefanikiwa kubaini wagonjwa wanaohitaji ushauri wa kitaalamu, tiba na upasuaji wa moyo kwa watu wazima na watoto, huku ikiongeza uelewa wa jamii kuhusu huduma zinazotolewa katika ALMC na JKCI, sambamba na maandalizi ya Mkoa wa Arusha kuelekea AFCON na kukuza utalii wa tiba nchini.