15 wapata ushemasi Moshi, Askofu Minde awapa ujumbe wao na wazazi

Moshi. Wakati mafrateri 15 wakipata sakramenti ya ushemasi katika Jimbo Katoliki la Moshi, Askofu wa Jimbo hilo, Ludovick Minde amewataka wazazi na walezi kuwaombea mashemasi hao kujiepusha na vishawishi vya dunia ili kutimiza ndoto zao za daraja la upadre.

Askofu Minde amesema hayo leo Jumatatu, Januari 5, 2026 wakati wa ibada ya misa takatifu ya kuwaweka wakfu mashemasi hao katika ibada ambayo imefanyika Parokia ya Kristu Mfalme, Moshi, mkoani Kilimanjaro.

“Nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa baraka hii ya pekee ambayo ameitoa kwenye kanisa siku hii ya leo kwa kutupatia vijana katika jimbo hili, hii ni baraka kubwa sana na  heshima ya pekee kwa kanisa letu,” amesema Askofu Minde.

Aidha, amewashukuru wazazi na walezi kwa kuwatoa vijana hao kwa kanisa na kuwapa malezi mazuri na kufikia katika hatua hiyo kubwa.

“Niwaombe pia muwaombee sana, mnafahamu tupo katika ulimwengu gani, lakini kama nilivyowasisitiza miaka ya leo kama tukiwa waadilifu kwa Yesu na kuwa  watu wa sala na sadaka. Katika utumishi sio rahisi kuingiwa na yule muovu, jizamisheni kabisa katika roho ya sala, sadaka na utumishi, kama mkiwa hivyo mtapiga hatua,” amesema Askofu Minde.

“Wazazi hawa ambao mmetupa hawa vijana 15 nawapongeza sana, mmeshiriki kwa kiasi kikubwa katika malezi ya hawa vijana, nasema asanteni wote wazazi, mapadre na makatekista wote na walimu wote, watawa wa kike na wakiume kwa kuwafikisha vijana wetu hapa walipofika,” amesema Askofu Minde.

Amesema mashemasi hao wapo vizuri kielimu na kwamba mpaka hapo walipofikia wameonesha jitihada kubwa kwa kanisa na wamepiga hatua kubwa.

“Sasa Yesu ameshawachukua watu wake, kwa hiyo vijana tunawashukuru kwa kumchagua Yesu na mkashinda vishawishi vyote, lakini vyote mmevikataa, hivyo mbakie wakristu kweli,” amesema Askofu Minde.

Askofu Minde amesema: “Katika jimbo letu leo tumepata vijana mashemasi 15, baada ya kumalizika hapa watarudi seminarini kwenda kumalizia, Januari 8, Mungu akipenda tutakuwa na vijana 17 ambao ni mashemasi sasa lakini kuna vijana wa mashirika vijana 7,  hivyo tutakuwa na vijana 24 ambao ni mashemasi watakaopata sakramenti ya  upadre katika kanisa hili siku hiyo.”

Aidha, amewataka mashemasi hao kuendelea kuwa waadilifu katika kanisa na kwa jamii kwa jumla ili kutimiza ndoto zao za kuitumikia jamii.

“Niwaombe, wakubali tu kwamba sasa wao ni mashemasi na kesho kutwa tu wataingia kwenye upadri, kuanzia leo muwe wadilifu katika hicho ambacho mmekipata kwa ajili ya kuwahudumia watu katika kanisa,”amesema Askofu Minde.

 Mkurugenzi wa miito wa jimbo hilo,  August Ndepatanisho, amewapongeza mashemasi hao akisema ni zawadi kwa kanisa na kuwataka waumini kuendelea kuwaombea ili wakamilishe miito yao ya upadri.

“Namshukuru Mungu kwa zawadi ya wito kwa mashemasi wetu hawa, pamoja na kanisa kwa malezi bora kwa hawa ndugu zetu, hivyo tuendelee kuwaombea kwa Mungu wakamilishe ndoto zao,” amesema Ndepatanisho