BAADA ya kukaa nje ya uwanja kwa takribani miezi minne, aliyekuwa mshambuliaji nyota wa Pamba Jiji, Abalkassim Suleiman, amekamilisha usajili wa kujiunga na Mbeya City ya jijini Mbeya, kwa dili la hadi mwisho wa msimu.
Nyota huyo amekamilisha usajili huo akiwa mchezaji huru baada ya kuachana na Pamba Jiji katika dirisha kubwa la usajili akitokea Fountain Gate, ambapo kwa sasa atakitumikia kikosi hicho cha City kinachonolewa na kocha Mecky Maxime.
Akizungumza na Mwanaspoti, Abalkassim amesema kuna baadhi ya timu ambazo hadi sasa anaendelea kufanya nazo mazungumzo ili kujiunga na mojawapo katika dirisha hili dogo, ingawa ni mapema kuziweka wazi kwa sababu dili hizo hazijakamilika.
“Mashabiki wangu watambue dirisha hili dogo la Januari wataanza kuniona tena uwanjani baada ya kukaa nje kwa muda mrefu, malengo yangu makubwa ni kufanya vizuri katika timu nitakayoenda, licha ya ushindani mkubwa uliopo,” amesema Abalkassim.
Licha ya kauli ya Abalkassim, Mwanaspoti linatambua mshambuliaji huyo amekamilisha usajili wa kujiunga na Mbeya City na muda wowote kuanzia sasa atatambulishwa kwa ajili ya kukitumikia kikosi hicho cha Mbeya kwa mkataba wa miezi sita.
Mbali na Abalkassim, wachezaji wengine waliosajiliwa na Mbeya City ni aliyekuwa kiungo wa Fountain Gate, Abdallah Kulandana na Hijjah Shamte aliyeachana na kikosi cha MFK Karvina B ya Jamhuri ya Czech iliyomsajili kutoka Kagera Sugar.
Mwingine ni aliyekuwa mshambuliaji wa Yanga, Yacouba Songne raia wa Burkina Faso, ambaye anakaribia kujiunga na kikosi hicho pia, baada ya msimu wa 2024-2025 kuachana na TRA United (zamani Tabora Utd) aliyoifungia mabao manne ya Ligi Kuu.
